Waziri wa Zambia ajiuzulu kwa madai ya kuonekana kwenye video akipokea fedha

Waziri wa Mambo ya Nje wa Zambia Stanley Kakubo amejiuzulu baada ya kudaiwa kunaswa kwenye video akipokea rundo la fedha kutoka kwa mfanyabiashara wa China.

Hakukana kuwa alikuwa kwenye video. Badala yake, Bw.Kakubo alisema anakabiliwa na "madai mabaya kuhusu shughuli za kibiashara" na amejiuzulu ili serikali "isikengeushwe" na utata huo.

Video hiyo inawaonesha wanaume wawili wakiwa wameketi kando ya meza wakihesabu pesa zilizopangwa vizuri, dola za Marekani na kwacha ya Zambia.

Nyuso zao hazionekani, lakini ilisababisha tetesi kwenye mitandao ya kijamii kwamba watu hao walikuwa Bw Kakubo na mfanyabiashara wa China.

Baadhi ya watu walihoji kwa nini uhamishaji fedha kwa njia ya benki haujafanywa na ikiwa ushuru ulikuwa umelipwa kufuatia muamala huo.

Picha ambazo hazijathibitishwa za noti zilizosainiwa kwa mkono pia zilijitokeza kwenye mitandao ya kijamii.

Mmoja alisema kuwa dola 100,000 "zimebadilishwa" kati ya Mzambia na kampuni ya uchimbaji madini ya China. Mwingine, wa tarehe 8 Julai 2022, alitaja jumla ya $200,000.

Katika barua yake ya kujiuzulu, Bw Kakubo hakupinga uhalisi wa video hiyo au maelezo yaliyoandikwa kwa mkono, badala yake, alisema alikuwa mwathirika wa "madai ovu juu ya shughuli za kibiashara kati ya biashara yangu ya binafsi ya familia na mshirika wetu wa kibiashara ambaye bado tuna uhusiano mzuri naye".

Alisema amejiuzulu uwaziri ili kuhakikisha kuwa serikali "haibabaishwi" na juhudi zake za kuboresha maisha ya Wazambia, lakini atabaki kuwa mbunge.

"Kwa wakati ufaao, tutatoa muktadha sahihi unaozunguka matukio ya hivi karibuni," tovuti ya habari ya Lusaka Times ilimnukuu Bw Kakubo akisema. Bw Hichilema alikubali kujiuzulu kwake, akisema anatambua "kazi na uongozi wa Bw Kakubo unaotukuka".

Hii ni mara ya pili kwa Bw.Kakubo kujipata katikati ya mabishano.

Mwaka jana, alishtakiwa kwa kupokea rushwa baada ya kuonekana akitoka katika ofisi ya kampuni ya saruji inayomilikiwa na Wachina.

Alikanusha kufanya makosa yoyote, huku rais akimtetea akisema amepokea kalenda na shajara.

Kampuni za China ni wawekezaji wakubwa nchini Zambia. Ubalozi wa China ulisema mwaka 2022 kuwa zaidi ya biashara 600 za China zimewekeza zaidi ya $3bn nchini Zambia.

Bw Kakubo ndiye waziri wa kwanza kulazimishwa kujiuzulu tangu Rais Hakainde Hichilema aingie madarakani Agosti 2021. Bw Hichilema aliahidi kupambana na ufisadi, lakini upinzani unamshutumu kwa kuwalenga isivyo haki wanachama wake, jambo ambalo anakanusha.

No comments