UFANISI WA EWURA WAIVUTIA MALAWI

 




Kaimu Mkurugenzi wa Udhibiti Uchumi Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) , Bw. George Kabelwa akiwasilisha mada kuhusu Muundo wa utendaji wa EWURA kwa watendaji kutoka MERA wakati wa kikao kazi kati ya taasisi hizo mbili kilichofanyika ofisi za EWURA Makao Makuu leo Novemba 13,2023 jijini Dodoma.

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) leo tarehe 13 Novemba 2023 imepokea watendaji kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati Malawi (MERA)waliokuja kujifunza namna EWURA inavyofanya kwa ufanisi shughuli za udhibiti wa huduma za nishati na maji nchini.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Bw Gerald Maganga, wakati akiwakaribisha watendaji kutoka MERA amesema imekuwa ni desturi ya EWURA kushirikiana na taasisi mbalimbali kwenye masuala ya udhibiti, na kwamba ipo tayari wakati wote kuendelea kutoa ushirikiano kwa taasisi yoyote itakayohitaji kujifunza na kubadilishana uzoefu na EWURA.

“Tumefarijika kuwapokea wenzetu kutoka Malawi kubadilishana uzoefu kwenye utendaji, hii imekuwa desturi yetu na tupo tayari wakati wote kutoa ushirikiano wa hali ya juu, “ anesema Bw. Maganga.

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya MERA, Bw. Charles Kambauwa, ameishukuru EWURA kwa ushirikiano na ameeleza kuwa, ufanisi wa EWURA kwenye udhibiti ndio ulioisukuma Mamlaka hiyo kuendelea kupata uzoefu na kujifunza kutoka kwake.

“Tuna hakika tutajifunza namna EWURA inavyoweka mipango, ufuatiliaji na tathmini ya shughuli za udhibiti na itatusadia kujipanga vyema kwenye majukumu yetu, ni dhahiri tumekuwa tukijifunza mengi kwa EWURA, hilo linajieleza,” amesema Bw. Kambauwa.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Udhibiti Uchumi wa EWURA, Bw. George Kabelwa, amesema pamoja na mambo mengine, EWURA imeijengea uwezo MERA kwenye uandaaji na utekelezaji wa mpango mkakati, mpango kazi na namna ya kufanya ufuatiliaji na tathmini ya shughuli za udhibiti kwenye sekta ya nishati.

Ujumbe kutoka MERA umejumuisha Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya MERA, Bwana Charles Kambauwa, Meneja Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini, Bwana Geoffrey Chilenga, Mtakwimu, Bi. Olive Moja na Mchambuzi wa Hesabu, Bi. Chisomo Mandalasi.

No comments