Mwili wa Mtanzania aliyetekwa na Hamas kuzikwa Jumanne Tanzania

 

Familia ya marehemu Clemence Mtenga, mtanzania aliyekuwa akiishi nchini Israel, imeanza maandalizi ya maziko yanayotarajiwa kufanyika siku ya Jumanne.

Msemaji wa familia, Boniface Mtenga amesema wanashirikiana na mamlaka za serikali katika taratibu mbalimbali za maandalizi ya kuupumzisha mwili wa marehemu Clemence.

Mtenga alisema, "Tunatarajia kuupokea mwili wa Clemence wikendi hii kisha utahifadhiwa mpaka siku ya Jumanne ambapo ndipo tutafanya maziko...

"...familia imefikia maamuzi hayo baada ya mazungumzo na serikali, wakati huu tukisubiri mwili usafirishwe kutoka nchini Israel," alisema Mtenga na kuongeza kuwa uamuzi wa kuzika Jumanne ni kutokana na mipango ya kifamilia.

Kwa Mujibu wa taarifa ya hivi karibuni ya Idara ya Mambo ya Nje ya Tanzania, Mtenga alikuwa nchini Israel kwa ajili ya programu ya mafunzo ya ndani, na alifariki Oktoba 7.

Hata hivyo mamlaka ilieleza kuwa inafuatilia kwa karibu Mtanzania Joshua Mollel ambaye anadaiwa kushikiliwa mateka.

Awali, Mamlaka ya Israel ilithibitisha kuwa Mollel alikuwa miongoni mwa watu zaidi ya 200 wanaoshikiliwa mateka huko Gaza.

No comments