SIMBA YAITWISHA YANGA GUNIA LA MISUMARI
Baada ya kupata ushindi mnono wa mabao 7-0 dhidi ya Horoya na kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, Simba sasa imeitwisha Yanga, wawakilishi wa Tanzania katika Kombe la Shirikisho, gunia la misumari.
Yanga ambayo kesho itaingia Uwanja wa Benjamin Mkapa kumenyana na Monastry, haina hesabu nyingine zaidi ya kushinda.
Endapo Simba ingefungwa leo, kushindwa kwa Yanga kesho isingekua stori, lakini ili mashabiki wa Kata ya Kariakoo, yalipo Makao Makuu ya klabu hizo waende sawa, itawalazimu Wananchi, kwa namna yoyote, waibuke na ushindi kesho.
Hesabu zinaonyesha, endapo Yanga atapata matokeo yasiyo ya ushindi, basi itabidi waombee, TP Mazembe asishinde dhidi ya Real Bamako, kwani endapo atashinda, atafikisha pointi 6.
Na kama mabingwa hao wa kihistoria katika soka la Tanzania watapata labda sare, watafikisha alama 8 ambazo watalazimika kushinda ugenini mjini Lubumbashi katika mechi yao ya mwisho.
Tabiri haziwapi nafasi ya kuipiga TP Mazembe nyumbani, kama ambavyo Simba hatarajiwi kuifunga Raja Casablanca kwao, hivyo namna pekee ya Yanga kesho ni kushinda!

Post a Comment