KUNA MENGI YA KUJIFUNZA KWA MO
NIMEKUWAkaribu na
soka letu kwa muda mrefu sasa, nikiwa naucheza katika ngazi za shule za msingi
na sekondari na hatua kubwa kabisa kuifikia ni ile ya Ligi Daraja la Tatu,
ngazi ya Mkoa enzi zile.
Bingwa wa Mkoa
miaka ile halikuwa jambo dogo, kwani baada ya ubingwa huo, ilifuata ngazi ya
Kanda, ambako mabingwa wa mikoa na washindi wao wa pili walicheza na washindi
wa hapo, walipanda daraja la Pili Taifa, hatua moja kabla ya kufika Ligi Daraja
la Kwanza, ambalo ndilo lilikuwa hatua ya juu kabisa.
Lakini hata baada
ya kuachana na soka la uwan jani, nimehudumu kwa miaka mingi pia nikiwa kama
mwandishi wa habari za michezo na burudani, kitu kilichonipa fursa ya kufahamu
mambo mengi yanayohusu soka, hasa viongozi na vyama vyake, kuanzia mikoani hadi
Karume pale.
Kwa klabu zetu
kubwa za Simba na Yanga, ambazo ndiyo mfano wa mpira wetu, zingeweza kuwa na
maendeleo makubwa sana kama tungepata aina ya viongozi wenye ndoto za mbali,
kwa sababu tayari zina mtaji mkubwa wa mashabiki, lakini hali imekuwa tofauti
kwa vile siku zote zimekutana na viongozi wanaopenda kukamua maziwa pasipo
kuhakiki malisho bora.
Kama klabu hizi
mbili ziliweza kujenga majengo yao katika miaka ya sabini na baadaye Yanga kuwa
na Uwanja wao, vipi leo hii, mashabiki wao wakiwa wameongezeka pengine mara
tatu ya hapo awali, wanashindwa kuwa na viwanja vyao vyenye hadhi?
Tatizo kubwa lililo
nyuma ya pazia kwa aina ya viongozi wanaopatikana katika miaka ya hivi karibuni
ni kutokuwa na jicho la kutazama maendeleo, badala yake wanaangalia katika
kujinufaisha wao binafsi. Ukitaka kuamini haya, tazama jinsi vita kubwa
inayopiganwa wakati wa uchaguzi.
Watu wanatumbukiza
fedha kuhonga wanachama, wanatumia hila, kampeni chafu na hata kuibuliana
kashfa, ili mradi tu waweze kupata nafasi za uongozi. Unatoa hadi mamilioni ya
shilingi ili ushinde uongozi, utarudishaje pesa zako? Ni kama wale wanasiasa
wanaolia machozi ya Mamba kwenye kampeni, wakionyesha hisia za kuguswa na
matatizo ya wananchi, kumbe ni wanafiki wanaowaza posho, mishahara mikubwa na
hadhi ya kibunge mjengoni.
Klabu hizi ndizo
timu pekee zinazoweza kushawishi wanachama kuzichangia pasipo hata kutumia nguvu.
Leo hii, klabu hizi zinaweza kusafiri kwa msaada kwenda katika kituo chochote
cha mechi zake za Ligi Kuu na huko zikapata hoteli yenye hadhi kwa mkopo,
wachezaji wakala watakacho na bado wakasafiri kurejea Dar es Salaam kwa wakati.
Na wanaweza kufanya
hivyo msimu mzima. Wanachojali sana mashabiki ni matokeo mazuri uwanjani. Kama
timu zina mitaji hii, ni vipi viongozi wanashindwa kutengeneza mfumo wa klabu
kuweza kujiendesha kwa faida?
Lakini hata hivyo,
kushindwa kubuni njia mbadala za kuiendesha klabu yenye mtaji mkubwa wa
mashabiki kwa maendeleo linaweza kuwa tatizo moja, lakini weledi wa uongozi,
ndilo tatizo kubwa zaidi linalozikumba klabu hizi mbili pendwa hapa nchini.
Mtu akishakuwa
kiongozi, Mwenyekiti kwa mfano, anataka yeye ndiye awe kocha wa timu, mtunza
hazina wa klabu, yaani kifupi ni kuwa viongozi wengi wa klabu hizi, hawajui
utendaji kazi wa kitaaluma.
Wakati fulani
nikiwa mwandishi wa michezo, nilisafiri kuelekea Morogoro kwenye moja kati ya
mechi za klabu hizi. Nikiwa njiani, majira ya saa nne asubuhi, simu yangu
ilipokea ujumbe kutoka kwa mmoja wa viongozi wa timu hiyo kunitaarifu juu ya
mapendekezo yake ya kikosi kwa kocha wa timu.
"Tumemwambia
kocha atupangie wachezaji hawa na hawa ndiyo wakae benchi," ilisema sehemu
ya ujumbe huo na kuorodhesha wachezaji hao.
Ni jambo la ajabu
sana, vipi kiongozi atoe mapendekezo ya wachezaji wa kucheza mechi badala ya
kazi hiyo kufanywa na mwalimu? Na hata kocha, hawezi kupanga wachezaji wa
kucheza mechi pasipo kupata ripoti ya daktari wa timu juu ya fitness ya
wachezaji!
Tatizo hili ndilo
hasa linalofanya klabu hizi zinashindwa kusogea. Lakini ujio wa Mo kwa namna ya
Uwekezaji, ni funzo kubwa ambalo linaweza kuwa ni mwarobaini wa kuusaidia mpira
wetu, achana na klabu hizo mbili pekee.
Mo ameibadilisha
Simba ndani na nje ya Uwanja na kuifanya kuwa timu ya kisasa kwa kila namna.
Katika benchi la ufundi, licha ya kocha na msaidizi wake, lakini yupo mwalimu wa
viungo, daktari wa timu, mchambuzi wa mechi ambao kila mmoja anafanya kazi kwa
mujibu wa alichokisomea kwenye eneo husika.
Ni ngumu kufikiria,
kama leo hii Mangungu ana ujasiri wa kupenyeza kikaratasi kwa kocha Didier
Gomes akitaka 'mchezaji' wake apangwe.
Mo amefanya hivyo
pia hadi kwenye bodi. Anajua yeye si fundi sana wa kujua vipaji na biashara ya
wachezaji. Amewaweka watu wa namna hiyo ili wamsaidie. Hao ni kama akina
Magori, Hans Poppe, Kassim Dewji, Mulamu na wenzao, ambao ili kubalance mambo,
wamewekwa chini ya mwanamama Barbara Gonzalez.
Viongozi wanafanya
majukumu yao ili benchi la ufundi na lenyewe lifanye majukumu yake. Matokeo
yake ni kama unavyoona, wachezaji wanajituma, makocha wanajituma na kikosi
chote kina furaha.
Lakini angalia
upande wa pili, kwa Wananchi. Kuna mtu anaitwa Injinia. Yeye ndiye anasajili
wachezaji, yeye ndiye anajadiliana na kocha. Mbaya zaidi, yeye ndiye mwakilishi
wa mdhamini ndani ya klabu.
Ingawa kimuundo
unaona kama Yanga nayo ina benchi la ufundi linalohitajika kwa timu ya kisasa,
lakini siyo vibaya kuhisi, kwa namna
timu inavyoendeshwa, kwamba huenda Injinia huwa anapenyeza 'mawazo' yake
juu ya nani aanze kucheza na nani asicheze kwenye mechi husika.
Kama matajiri wa
nchi yetu wataamua kuwekeza kwenye mpira wa miguu, kisha wakaajiri watu wenye
taaluma kwenye maeneo husika, ni wazi kuwa tunaweza kuwa na timu zinazotisha
kama Simba hata zaidi ya nne au tano kwa wakati mmoja.
Fikiria kama Azam
itakuwa namna hiyo, Yanga, uwekezaji wa maana pia ukafanywa Kagera na Mtibwa,
vipi tukose timu zinazoweza kupambana kwenye anga la kimataifa kama ilivyo sasa
kwa Afrika Kusini ambayo inaingiza timu mbili hatua ya robo fainali ya Ligi ya
Mabingwa Afrika?
Watu wenye hela
wapo, pengine TFF iunde timu ya wataalamu wa kwenda kutoa ushawishi kwa
matajiri ili waone namna gani wanaweza kupata faida kwa kuwekeza kwenye soka.
Hawa wataalamu
wawatembelee na kuzungumza na watu kama akina Rostam Aziz ili airejeshe timu ya
nyumbani kwao kule Mirambo, Bin Slum wa Coastal Union, Asas afanye hivyo kwa
Lipuli na wengine na wengineo.

Post a Comment