POLISI NAIROBI WAFUNGA BARABARA KUELEKEA IKULU

Polisi Nchini Kenya, wamefunga barabara zote zinazoingia na kutoka katika Ikulu ili kizuia maandamano ambayo viongozi wake sasa wanataka yaelekee katika ofisi hiyo namba moja ya Rais William Ruto.

Maelfu ya wananchi wa Kenya jana waliingia mitaani katika miji kadhaa kuitikia wito wa kiongozi wa Azimio, Raila Odinga kutaka serikali kukwamua kupanda kwa gharama ya maisha na pia kupinga matokeo ya uchaguzi uliopita.

Watu kadhaa walikamatwa hiyo jana na hali ilikuwa mbaya katika Mji Mkuu Nairobi, hasa katika kitongoji cha Kibera ambako waandamanaji walichoma moto matairi huko polisi wakitupa mabomu ya kutoa machozi.

Katika kituo kikuu cha kuanzia maandamano hayo cha KICC, polisi wametanda ili kuzuia watu kukusanyika hasa baada ya wito kutolewa na viongozi kuwataka leo kuelekeza maandamano yao Ikulu.

Ukiondoa mapambano yanayoendelea joijini Nairobi kati ya Polisi na wananchi, hali ni shwari katika miji mingine, hasa Kisumu ambako kunatajwa kama ndiyo ngome kuu ya Raila kisiasa.

No comments