MZEE PAUL KIMITI AUNGA MKONO MASHAMBA MAKUBWA YA SAMIA
Mwenyekiti wa Taasisi ya Kumbukizi ya Mwalimu
Nyerere, amesifu mpango wa Serikali wa kuanzisha mashamba makubwa maarufu kama
Buld Better Tomorrow.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, mzee Kimiti
alisema mpango kama huo uliwahi kubuniwa na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward
Sokoine na Mwalimu Nyerere walianzisha mfuko kuanzia mwaka 1983 hadi 1988, ingawa
wazo hilo halikufikiwa kwa vile alifariki mapema.
Mzee Kimiti aliwataka vijana kuwa wawajibikaji katika kila sekta lakini pia kujenga utamaduni wa kupenda kilimo.
Alisema katika mpango huo, Sokoine alijitolea
kutoa nusu ya mshahara wake ili kuwezesha jambo hilo, kwani kwa mazoea, watu
wanaolima hapa nchini ni wazee badala ya vijana ambao ndiyo wenye nguvu.
Jana, Rais Samia Suluhu Hassan alizindua mpango
kamambe wa mashamba makubwa huko Chinangali Dodoma, ambako vijana wapatao 800
watapewa mafunzo kwa miezi minne kabla ya kukabidhiwa mashamba hayo ili walime.
Aidha, sambamba na uzinduzi huo, pia Rais Samia
alikabidhi magari na mitambo kwa Tume Maalum itakayosimamia mashamba hayo na
kumtaka Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kuhakikisha fedha zinazotolewa kwenye
mpango huo hazitumiwi kwa matumizi mengine.
Mzee Kimiti licha ya kuwahi kuwa Waziri na Mkuu wa
Mikoa kadhaa wakati wa uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere pia alikuwa ni mtaalam wa
kilimo aliyesomea nchi mbalimbali duniani.


Post a Comment