HII INATISHA, KUNA MADANGURO 320 KINONDONI PEKEE
Hii kwa kweli inatisha. Wakati biashara kongwe duniani ya ngono ikiendelea kusumbua akili ya viongozi kwa kukiuka maadili ya Mtanzania, imebainika kuwa katika Wilaya ya Kinondoni pekee, jijini Dar es Salaam kuna madanguro yanayofahamika yapatayo 320.
Kwa mujibu wa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Songolo Mnyonge, kitongoji cha Mwananyamala kina madanguro 150, Tandale kinayo 135 na Msasani yapo madanguro 35.
Ili kudhibiti biashara hiyo, kiongozi huyo alisema wameanzisha vita endelevu ambapo kwa kuanzia, watakusanya taarifa za maeneo ya biashara hizo ili kuwa na data za uhakika.
Aidha, Mnyonge alisema baadae watawaita na kuzungumza na wenye nyumba zinazotumika kwa biashara hiyo ili kuelewa changamoto zao ikiwemo kujiridhisha kama kubadili matumizi ya nyumba hizo kumefuata matakwa ya kisheria kwani vinginevyo watawafikisha mahakamani.
Aliwataka wananchi kuwaunga mkono katika vita hivyo kwani kwa wale wanaopanga vyumba wanawaharibu watoto kwa vitendo vyao, akisema ni afadhali ya wadada poa wanaojipanga barabarani kuliko wale waliopanga vyumba.

Post a Comment