FIFA YAZINDUA UWANJA WA MICHEZO WA PELE KIGALI, KAGAME, INFANTINO WAONYESHANA UFUNDI UWANJANI
Rais wa Rwanda Paul Kagame na Rais wa Shirikisho la soka duniani (FIFA) Gianni Infantino wakiuzindua kwa pamoja Uwanja wa Michezo wa Kigali Pele jijini Kigali jana.
SHIRIKISHO la soka la Kimataifa (FIFA) jana lilishirikiana na Rwanda kuuzindua Uwanja wa Michezo wa Pele jijini Kigali ikiwa ni kuunga mkono ombi la Rais wa FIFA, Gianni Infantino la kuzitaka nchi zote duniani kuvipa viwanja jina la mkongwe huyo wa soka wa Brazil, Edson Arantes Do Nescimento aliyefariki mwaka jana.
Na Infantino akiwa na Rais Paul Kagame, mcheza tenisi ambaye ni shabiki mkubwa wa soka akishabikia Arsenal ya England, waliuzindua uwanja huo na kufuatiwa na mechi ya kirafiki iliyowashirikisha wawili hao wakiungwa mkono na mastaa wakubwa wa dunia.
Pele akiwa na vikombe vitatu vya dunia alivyovichukua wakati wa enzi zake akisakata kandanda na timu ya taifa ya Brazil
Timu ya Paul Kagame iliishinda ya Gianni Infantino kwa mabao 3-2 katika mchezo uliochezeshwa na mwamuzi wa kimataifa Salma Mukansanga, ambao utafuatiwa na kongamano la FIFA la 73 linalowajumuisha wajumbe 2000, ambalo pia litatumika kwa uchaguzi wa FIFA huku Inflantino akiwa mgombea pekee wa nafasi ya Urais.
Upande wa timu ya Kagame alikuwemo Jay Jay Okocha wa Nigeria, Patrice Motsepe ambaye ni bosi wa CAF na mmiliki wa klabu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Jimmy Mulisa, Kalekezi Olivier, Kayiranga Baptiste, Eric Nshimiyimana Bakanyijijeho wa Rwanda ambaye kwa sasa ni kocha, Grace Nyinawumuntu kocha wa timu ya wanawake ya Rwanda, rais wa Shirikisho la soka la Rwanda FERWAFA Olivier Nizeyimana.
Upande wa timu ya Infantino ilikuwa na wachezaji kama Youri Djorkaeff aliyewahi kuchezea timu za Paris Saint Germain na Monaco ambaye kwa sasa ni mshauri mkuu wa FIFA na Gilberto Silva aliyekuwa mchezaji maarufu wa Arsenal.
Januari mwaka huu, wakati wa mazishi ya Pele, Infantino, ambaye anamuelezea Pele kama“mwanamichezo wa mfano wa kuigwa”, aliahidi kuiomba kila nchi duniani kuupatia jina la Pelé uwanja, kwa heshima ya Mchezaji bora wa Brazil na dunia. Rwanda, ambayo inapokea kongamano la 73 la FIFA ni miongoni mwa nchi ambazo zimetekeleza ombi hilo.





Post a Comment