WATU 220 WAFARIKI, 41 WAPOTEA KIMBUNGA FREDDY MALAWI, RAIS AOMBA MSAADA


Rais Chakwera akiwafariji baadhi ya wahanga wa kimbunga hicho mjini Blantyre

Jumla ya watu 220 wamethibitishwa kupoteza maisha kote nchini Malawi, huku 41 wakiwa hawajulikani walipo kutokana na kadhia ya kimbunga Freddy kilichoandamana na mvua kubwa iliyosababisha mafuriko na maporomoko ya makazi.

Rais wa Malawi Lazarus Chakwera ametangaza siku 14 za maombolezo ya kitaifa huku akiomba msaada wa kimataifa kusaidia katika shughuli za uokozi na kulijenga upya taifa hilo baada ya mvua kubwa iliyonyesha kwa siku sita kusababisha maafa makubwa nchini humo.

"Malawi iko katika hali ya janga, kile kimbunga Freddy imefanya ni kuturudisha nyuma ilhali tulikuwa tunajijenga upya kutokana na majanga ya kipindi cha nyuma. Naiomba jumuiya ya kimataifa kutuangalia kwa jicho la huruma kwa sababu tunahitaji msaada, tunahitaji msaada wa kuwashughulikia manusura ambao wamepoteza kila kitu.Wanahitaji vitu vya msingi,makazi,mavazi,chakula."

Zaidi ya watu 4000 wameyahama makazi yao na kwa sasa wanahifadhiwa katika majengo ya muda kote nchini.

Rais pia alisema mkutano wa dharura wa baraza la mawaziri uliidhinisha kutolewa kwa dola milioni 1.5 kusaidia maelfu ya Wamalawi walioathiriwa na dhoruba huku akisisitiza kuwa kiwango hicho cha fedha hakitoshi kwani uharibifu uliotokea ni mkubwa.


No comments