SIMBA WALIKOSA BAHATI, WALITAWALA KILA KITU

Kuna baadhi ya mashabiki wa soka wanaamini kuwa safari ya klabu ya Simba kuelekea robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika, itakuwa ngumu hasa baada ya kukibali kipigo cha bao 1-0 jana mbele ya Horoya Fc ya Guinea.

Simba ilipoteza mchezo ambao iliutawala kwa kiwango kikubwa, hasa katika kipindi cha pili, wakitafuta kurejea mchezoni baada ya kutanguliwa katika kipindi cha kwanza.

Ni mashabiki wachache kati ya wengi walioangalia mchezo huo waliamini kama klabu hiyo iliyojipambanua kufanya vizuri kimataifa, itaondoka mikono mitupu, kwani ilistahili hata pointi moja.

Kilichoiangusha Simba ni kukosa utulivi, kila mchezaji akitaka kufunga, hivyo kuwafanya wacheze kwa presha kubwa.

Mshambuliaji kiongozi na nahodha John Bocco, alikuwa na uwezo mkubwa wa kufunga si chini ya mabao matatu, lakini nafasi zote alizopata alipoteza.


Kiungo fundi, Clatous Chama naye kwa namna ambayo mashabiki hawajamzoea, alipata nafasi nzuri ndani ya eneo la penati, lakini akapaisha.

Wapo baadhi ya mashabiki wanamlaumu mwamuzi, kuwa aliibeba Horoya, lakini kwa namna mchezo ulivyokuwa, Simba hawana sababu ya kumlaumu mwamuzi, isipokuwa wao wenyewe.

Na kwa namna walivyocheza, inatoa matumaini kuwa bado wana nafasi ya kupata nafasi katika kundi lao ambalo pia lina timu za Raja Casablanca ya Morocco na Vipers ya Uganda.

Baada ya jana Simba kupata matokeo hayo, leo ni zamu ya watani wao, Yanga wanaoingia uwanjani ugenini huko Tunisia.


No comments