NI WAKATI WA KUIPELEKA LIGI KUU TANZANIA BARANI AFRIKA

Wiki iliyopita, Ligi Kuu ya Tanzania ilitajwa kuwa ni ya tano kwa Ubora barani Afrika, ikitanguliza na Misri, Algeria, Afrika Kusini na Morocco.

Ni jambo ambalo miaka mitano nyuma ingekuwa ni maajabu makubwa kumweleza mtu kuwa tunaweza kuwa na ligi bora kuzishinda nchi kama Nigeria, Senegal, Togo, Ghana, Tunisia, Cameroon au hata Sudan, Zambia, DRC!

Hapana shaka kuwa ubora huo wa ligi yetu, umechangiwa zaidi na ushindani miongoni mwa timu zinazoshiriki, ambazo zimezifanya timu zinazoshiriki michuano ya kimataifa nchini kufanya vizuri.

Simba, ambayo ndiyo klabu iliyofanya vizuri zaidi, ikifika hatua ya makundi mara kadhaa na hata robo fainali ya michuano ya CAF, imekuwa kielelezo kizuri cha soka letu.

Hata hivyo, pamoja na ligi hiyo kupewa thamani hiyo, bado hauoni dhamira ya dhati ya timu zetu kuthibitisha hilo kwa kutawala soka la Afrika.

Misri ambao wana ligi bora zaidi Afrika, wanatawala kweli soka la bara hili. Timu zake kama National Al Ahly, Zamalek, Piramids, Ismailia na nyinginezo, kufika hatua za makundi au robo fainali ni jambo la kawaida tu na ni madra kwa klabu zake kupitisha misimu miwili bila kuleta kombe nyumbani.

Ni wakati sasa, hasa kwa kuanzia msimu huu, utani wa Yanga na Simba, ungehamia huko. Zishindane kufanya vizuri ili badae klabu kama Azam, nayo ijiunge katika kuonyesha ubora wa NBC Premier League.

Itakua haina maana kama ligi yetu inabakia kuwa nzuri bila uzuri huo kuakisi ushiriki wa michuano ya kimataifa.


No comments