WADANGANYA UMRI SASA KUUMBULIWA NA MASHINE

Tabia ya watu wa kada mbalimbali kudanganya umri wao, sasa watajikuta wakiumbuka baada ya mashine maalum kubaini uwezo wa kutambua umri kugundulika.

Mashine hiyo inayokwenda kwa jina la Magnetic Resonance Imaging au kwa kifupi MRI, inaweza kutambua umri wa binadamu kwa kupima baadhi ya viungo kama vile kiwiko, kifundo na vinginevyo.

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza BBC, mashine hiyo yenye muundo wa kitanda, pia ina uwezo wa kutambua maradhi ya binadamu kwa kupima bila upasuaji viungo kama moyo, figo, ini, kongosho, mapafu n.k.

Suala la udanganyaji wa umri limekuwa kubwa hasa kwa wanasoka wa Afrika wanaosaka malisho bora barani Ulaya au hata wale wanaosaka timu zenye malipo makubwa ndani ya Afrika.

Sababu kubwa inayowafanya wachezaji kupunguza umri wao ni klabu kutovutiwa na wale wenye umri mkubwa kwa kile wanachodai muda mchache wa kucheza na pia uwezo mdogo wa kumudu mikikimikiki ya uwanjani.

Nchini Tanzania, timu ya vijana chini ya umri wa miaka 23, iliwahi kuondolewa katika mashindano ya Afrika baada ya mchezaji wake Nurdin Bakari kubainika kudanganya.

Kuondolewa au kukutwa na kashfa ya kudanganya umri imeweza kukutwa pia kwa mataifa ya Chad, Congo DRC, Nigeria, Cameroon, Senegal kwa kuzitaja chache.

Miisimu miwili iliyopita, mashabiki wa soka nchini waliachwa midomo wazi baada ya Simba kumsajili mlinzi wa kati wa kimataifa kutoka Kenya, Joash Onyango Achieng, aliyedai kuwa na umri wa miaka 29, tofauti kabisa na muonekano wake.

No comments