TUNALEA RUSHWA KATIKA SOKA LETU

Ingawa soka la Tanzania katika ngazi ya klabu linaonekana kukua, bado wengi wa mashabiki hawaridhiki na namna mamlaka za mchezo huo zinavyoendesha mambo yake.

Shirikisho la soka nchini TFF, kwa maana ya viongozi wake, hawajiamini. Ni wepesi kutumia rungu kumuua inzi, wakati kuondoa uozo ndani ya nyumba ulitosha kuwaondoa wadudu wote wabaya wasirudi tena.

Unapomshambulia inzi kwa rungu ili hali uozo ukiwemo, haisaidii kuwaondoa wadudu kwani uchafu unawavutia kugombea kuingia bila kujali hatari iliyopo mbele yao.

Kitu cha kwanza kinachoonyesha uwepo wa mambo kutokuwa sawa katika taasisi ni udhibiti wa taarifa zake na kutokuwa tayari kukosolewa au kuhojiwa.

TFF mara kadhaa imeonyesha udhaifu katika eneo hili. Watu wote wanaolihoji hawabaki salama. Mifano ya watu waliokumbana na kadhia kutoka kwa shirikisho letu hili ni wengi, wachache miongoni mwao ni Haji Manara, Shafii Dauda na mmiliki wa klabu ya Gwambina, Alexanda Mnyeti.

TFF haijawahi kuwa siriaz na suala la kukomesha au japo kupunguza vitendo vinavyoashiria rushwa michezoni. Golikipa wa zamani wa Yanga. Kabwili aliwahi kuituhumu klabu moja kubwa kutaka kumpa rushwa, lakini licha ya ukubwa wa jambo hili, shirikisho letu liliacha mambo yaishe kama yalivyokuja.

Licha ya hayo, mchezaji mmoja wa timu moja mkoani Mbeya, aliwahi kulalamika hadharani, jinsi viongozi wa timu nyingine kubwa walivyokuwa wakihaha kuwahonga ili wafungwe.

Tungetegemea wachezaji hawa wangekuwa msaada mkubwa kwa TFF kuweza kuwafahamu waliohusika na hatua kuchukuliwa.

TFF inawaogopa Simba na Yanga. Kocha wa zamani wa Simba, marehemu Aggrey Siang'a, raia wa Kenya, aliwahi kusema hadharani kuwa viongozi wa timu hiyo walikuwa wakitumia fedha kupanga matokeo.

Rushwa haiwezi kundoka kama jambo hili halichukuliwi kwa uzito unaostahili. Aliyewahi kuwa mmiliki wa timu moja ya Ufaransa ya Olimpic Marsseille, Bernad Tapie aliwahi kufungwa jela kwa kujihusisha na upangaji matokea. Ikumbukwe Tapie alikuwa tajiri enzi hizo.

Kule Italy, jambo kama hilo liliwahi kumkuta mmiliki wa AC Milan ambaye alipata kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Silvio Berusconi.

Zipo kelele za kila siku za mashabiki wa timu hizi kubwa mbili, kila mmoja akimlalamikia mwenzake kuwa anashinda mechi zake kwa kununua. Ni kweli kuwa ni vigumu kuthibitisha rushwa, lakini mazingira yangetosha kuonyesha mwelekeo.

Hivi kwa nini timu zetu nyingi zinashinda mechi za nyumbani kuliko ugenini ukiziondoa hizi za Kariakoo?

Hivi kwa muda wote tangu Wallace Karia ameingia pale ofisini hajakutana na vitendo vya rushwa mpirani? Kwa nini Mnyeti aliyetoa tuhuma za kuombwa rushwa na watu wa TFF asipewe ushirikiano ili awataje wahusika na badala yake wanageuka mbogo na kumtaka athibitishe?

Maana nyepesi ni kuwa wanamtisha ili kuwanyamazisha wengine wasiongee ukweli. Rushwa haiwezi kuachana na soka letu kama tutaendelea na utaratibu huu.


No comments