TUTAENDELEA KUIMARISHA MIUNDOMBINU YA UCHUKUZI - PROF. MBARAWA
WAZIRI
wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali itaendelea
kuimarisha miundombinu ya uchukuzi kwa nyanja zote ili kukuza biashara na
utalii hapa nchini.
Akipokea ndege mpya ya Edelweiss Airbus A 340 ikiwa na watalii 270 toka Zurich Uswisi iliyoanza kutoa huduma zake kati ya Zurich Uswisi na Kilimanjaro na Zanzibar hapa nchini, Prof. Mbarawa amesema hatua hiyo itaongeza fursa za ajira kwa kuwa itachochea shughuli za utalii na biashara nchini.
"Kuanza
kwa safari za ndege hii kunaonesha kuwa Tanzania iko salama kwa wageni na
wenyeji hivyo juhudi za mapambano dhidi ya Uviko 19, zitaendelea ili kuhuisha
tena huduma za utalii na biashara," amesema Prof. Mbarawa.
Aidha
ameushukuru uongozi wa Kampuni Edelweiss kwa kukubali kuanza safari kati ya
Uswisi na Tanzania na kuwataka Watanzania kuchangamkia fursa kwa kutoa huduma
bora za biashara na utalii.
Amesisitiza
kuwa kuanza kwa safari hizo kati ya Zurich Uswisi, Kilimanjaro na Zanzibar ni mkakati
wa Serikali kuimarisha huduma za utalii na biashara.
Naye Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Damas Ndumbaro amesema kupokea abiria 270 toka Uswisi kuja kutalii nchini ni ishara njema kwa sekta ya utalii na kuwataka Watanzania kuendeleza hulka za ukarimu kwa wageni ili kuvutia wageni wengi zaidi na hivyo kukuza utalii na biashara kwa ujumla.
Kwa upande wake, Balozi wa Uswisi nchini Tanzania, Didier Chassot amesema ubora wa utalii wa fukwe, mbuga na Mlima Kilimanjaro ndiyo umevutia watalii toka Uswisi kuja moja kwa moja kutalii nchini.
Amesema kuanzia sasa ndege za Edelweiss Airbus zitafanya safari mara mbili kwa wiki toka Zurich Uswisi hadi Kilimanjaro na Zanzibar.
Edelweiss
inakuwa ndege ya pili toka kampuni ya Lufthansa kutoka Ulaya kuja moja kwa moja
Tanzania kufuatia ndege yake nyingine ya Eurowings kuanza safari toka Frankfurt
Ujerumani kwenda Zanzibar mara mbili kwa wiki tangu Julai mwaka huu.
Imetolewa na Kitengo cha Habari
na Mawasiliano Serikalini Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Post a Comment