PROFESA MBARAWA KUUNDA TIMU YA UCHUNGUZI UWANJA WA NDEGE ARUSHA
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amesema ataunda timu ya uchunguzi ili kujiridhisha kama gharama za ujenzi unaoendelea katika uwanja wa ndege wa Arusha zinawiana na thamani ya fedha.
Profesa Mbarawa amesema
hayo mara baada ya kukagua upanuzi na ukarabati wa miundombinu ya maegesho ya ndege,
magari na njia ya kuruka na kutua ndege (run way) katika uwanja huo.
“Nimekagua kazi ni nzuri
hongereni, ila nitaleta timu hapa iniambie hizi gharama za ujenzi mnazozitaja kama
zinaendana na thamani ya fedha”, amesema Prof. Mbarawa.
Amewataka wafanyakazi
wa uwanja wa ndege huo kufahamu umuhimu wao katika kutoa huduma bora kwa watalii
na abiria wengine ili kuvutia watu wengi kutumia uwanja huo na hivyo kuongeza mapato.
Amesisitiza kuwa uwanja
wa ndege wa Arusha ni wa tatu kwa mapato na wa pili kwa miruko ya ndege na abiria
katika biashara ya usafiri wa anga hapa nchini ukitanguliwa na uwanja wa ndege wa
Dar es Salaam (JNIA) na Mwanza hivyo Serikali inautazama kikamilifu.
Naye Kaimu Meneja wa
uwanja wa ndege huo Bw, Reston Mtafya amesisitiza kuwa watumishi wamejipanga vizuri
kimaadili, nidhamu na ubunifu ili kuleta tija katika kazi zao.
“Tumejipanga kuhakikisha
uwanja wetu unatumiwa na abiria wengi kwa kutoa huduma za viwango vya juu”,
amesisitiza Mtafya.
Katika hatua nyingine
Waziri huyo wa Ujenzi na Uchukuzi amekagua karakana ya Wakala wa Ufundi na Umeme
nchini TEMESA mkoa wa Arusha na kuwataka kufanya kazi zinazopimika na kumpa ripoti
za kazi hizo kila mwezi.
Amewataka kuhakikisha
malalamiko ya watumiaji huduma za TEMESA yanafika mwisho kwa kutoa huduma za kisasa,
kibingwa na za haraka katika fani ya utengenezaji wa magari, mitambo na umeme.
“Kila mwezi nataka ripoti
ioneshe imezalisha kiasi gani cha fedha, mmekusanya shilingi ngapi na mmetoa huduma
kwa kiwango gani ili tuwapime na watakaoshindwa watupishe”,
amesisitiza Prof. Mbarawa.
Amezungumzia umuhimu
wa TEMESA kufanya majukumu yake ya msingi katika kutoa huduma na kuwatumia wahitimu
wa VETA na Vyuo vya Ufundi kufanya mazoezi ili kuwajengea uwezo wakati wanatafuta
ajira.
Prof. Mbarawa yuko katika
ziara ya siku tatu mkoani Arusha kukagua miradi ya maendeleo ya taasisi zilizo chini
ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI
NA MAWASILIANO SERIKALINI WIZARA YA UJENZI NA UCHUKUZI

Post a Comment