PROFESA MBARAWA AMTAKA MKANDARASI TANGA –PANGANI KUONGEZA SPIDI
WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amemtaka Mkandarasi China Henan International Cooperation Group Co. Ltd (CHICO), anayejenga barabara ya Tanga-Pangani KM 50, kwa kiwango cha lami kuongeza kasi ya ujenzi huo ili kuwawezesha wananchi kunufaika na barabara hiyo.
Akizungumza wakati wa
kukagua maendeleo ya ujenzi huo ambao umefikia asilimia 18, kwa sasa Prof.
Mbarawa amesema changamoto zilizochelewesha mradi huo zimepatiwa ufumbuzi hivyo
hakuna tena kisingizio cha kuchelewesha mradi huo.
“Mkandarasi,
Msimamizi na TANROADS nawapa miezi minne nikija tena nataka kuona mabadiliko makubwa
yanayoendana na ubora wa kazi”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Amesema kila hatua ya
ujenzi ifuate maelekezo ya usanifu ili kuiwezesha barabara hiyo muhimu kwa utalii
wa fukwe za bahari na hifadhi ya Saadani kuvutia utalii na kukuza uchumi wa mikoa
ya Tanga na Pwani.
Amemhakikishia Mkuu
wa Mkoa wa Tanga kuwa watu wote wanaostahili fidia kwa mujibu wa sheria watalipwa,
hivyo wajibu wao uwe kufanya kazi kwa bidii na kulinda rasilimali za miundombinu
na wakandarasi.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga
Bw, Adam Malima amemshukuru Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi na kumhakikishia usalama
katika miradi yote ya ujenzi mkoani humo na kusisitiza barabara ya Tanga–Pangani
KM 50, itakapokamilika itafufua uchumi wa
Wilaya ya Pangani na Mkoa wa Tanga kwa ujumla.
Naye Meneja wa TANROADS
Mkoa wa Tanga Eng. Alfred Ndumbaro amesema barabara hiyo itakapokamilika itakuwa na makalvati makubwa 19 na madogo116 ili kuruhusu
maji yanayoelekea baharini kuingia kwa urahisi.
Barabara ya Tanga-Pangani
KM 50, ni sehemu ya barabara ya Tanga- Pangani- Saadani -Bagamoyo yenye urefu wa
KM 256 ambayo ni sehemu ya barabara kuu ya Horohoro-Tanga- Pangani- Saadani -Bagamoyo
hadi Dar esSalaam kwa upande wa Tanzania na Malindi-Mombasa hadi Lungalunga nchini Kenya ambayo ina lengo la kurahisisha usafirishaji
wa mizigo, biashara za mipakani na kukuza utalii itakapokamilika.
Katika hatua nyingineWaziri
Prof. Mbarawa amekagua ujenzi wa barabara ya Muheza-Amani KM 40 ambayo imeanza kujengwa
kwa lami KM 7 na kuahidi kuwa serikali itazijenga KM zote 40 kwa kiwango cha
lami ili kuhuisha biashara na kilimo cha matunda, viungo na utalii Wilayani Muheza.
Prof. Mbarawa yuko katika
ziara ya siku tatu Mkoani Tanga kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya barabara,
reli, uwanja wa ndege, bandari, vivuko na majengo ya Serikali.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO
SERIKALINI WIZARA YA UJENZI NA UCHUKUZI

Post a Comment