MTOTO WA SUNDAY MANARA ANAUMIZWA NA NINI?

 Haji Manara atoa ya Moyoni kuhusu Hassan Bumbuli - Wasomi Ajira : Wasomi  Ajira

VIJANA wa kizazi cha Bongo Fleva leo hii ukiwaambia kuwa kuna walemavu wawili waliwahi kuwa mastaa wa huu muziki huko nyuma watakataa katakata, lakini sisi ambao tuliushuhudia ukihama kutoka hatua moja kwenda nyingine, tunawajua Mabaga Fresh!

Sawa na mashabiki wa soka wa enzi hizi ambao wanadhani Haji Manara ni maarufu kuliko alivyokuwa baba yake, Sunday Manara 'Computer'.

Sisi wa enzi hizo tunapendelea zaidi kumuita Mtoto wa Sunday Manara, hasa anapofanya jambo zuri au baya, kwa sababu enzi tukiimba jina la baba yake, yeye alikuwa sawa tu na watoto wengine tusiowajua majina wa gwiji huyo wa soka ambaye alipewa jina la utani la kifaa ambacho ni Watanzania wachache mno walikuwa wakikifahamu miaka hiyo!

Haji Manara si mtu wa kwanza kutoka Simba kwenda Yanga katika ngazi ya uongozi. Alianza Super Coach, Syllersaid Mziray, miaka ile ya mwanzoni mwa tisini akafuata Senzo Masingisa miaka miwili iliyopita, kama kumbukumbu zangu zipo sawa!

Kama kuna siku Mziray (Mwenyezi Mungu mpatie mapumziko ya amani) aliwahi kuisema Klabu ya Simba kwa waliyomtenda, basi nadhani itakuwa ni ile siku anatoa sababu za kujiunga na Yanga.

Vivyo hivyo, tangu ajiondoe Simba, aliyekuwa CEO wao, Senzo amekuwa, mara nyingi, akikwepa kuizungumzia Simba kwa mabaya.

Lakini hali ni tofauti sana kwa huyu mtoto wa Sunday Manara. Tatizo liko wapi? Niliwahi kusema hapo kabla kuwa Haji hakupenda kuondolewa katika ile nafasi yake ya ubosi wa kitengo cha habari na siku zote alilalamikia njama zilizokuwa zikifanywa ile aondolewe.

Kwangu, kuna tatizo lingine ninaliona kwa Haji. Licha ya kuchukizwa na kitendo cha kuondolewa, lakini pia alihisi, yeye ni maarufu kuliko Klabu ya Simba, kiasi aliamini kuwa akiondoka, mambo yatavurugika Msimbazi.

Aliamini ataondoka na wafuasi na kusababisha 'rabsha' kutoka kwa mashabiki. Utulivu uliopo Simba katika ishu yake unamtesa. Ndiyo maana, badala ya kuifanya vyema kazi yake ya Uhamasishaji Yanga, kila mara anaizungumzia Simba.

Sasa amefikia hatua ya kusema ataipeleka Simba Mahakamani kudai fidia kwa kufanyishwa kazi bila mkataba. Of coz hiyo ni haki yake ya msingi, lakini ilikuwa ni lazima aseme hadharani?

Kwanza kwa kusema alifanyishwa kazi miaka sita bila mkataba, anajaribu kutuaminisha kuwa ni jinsi gani yeye alikuwa radhi kuifanya kazi ile bure, ili mradi tu yupo Simba. Alijua hatari ya kudai mkataba na yeye hakuwa tayari kukabili matokeo yake!

Kwa sisi tunaovijua kidogo klabu hizi mbili za Kariakoo, ni heri uwe mbeba jezi wa Simba na Yanga utapata maslahi makubwa kuliko kuwa Meneja wa timu yoyote ya Ligi Kuu, labda ukiondoa Azam.

Haji alipenda kuwepo na malumbano katika media baina yake na viongozi wa Simba. Lakini pengine kwa kufahamu udhaifu wake, wameamua kukaa kimya bila kujibu anachokisema, kitu ambacho kinamuumiza zaidi. Anatamani siku moja kiongozi amjibu, lakini kitendo cha kumkalia kimya ni kama kumdharau.

Ushauri wangu kwa Haji, angeachana na Simba, ni kubwa sana kwake. Kama ana madai, aende huko mahakamani kimyakimya, lakini kwa yeye kujaribu kujipima ubavu na klabu hii, anajidanganya.

Hakuna, narudia tena, hakuna mtu binafsi aliyejaribu kuweka msuli wake kwa klabu hizi mbili akafanikiwa. Mzee Hamis Kilomoni anaweza kuwa shahidi kwa Simba au ndugu yangu Magoma kule Yanga.

Patrick Rweyimamu aliyewahi kuondolewa umeneja Simba alikuwa na madai pia na klabu hiyo, lakini uliwahi kumsikia akizunguka katika vituo vya redio akiiponda?

Antonio Nugaz aliyeondolewa Yanga, unadhani amekifurahia kitendo hicho cha kuwekwa pembeni pale Jangwani? Mbona humsikii kwenye mitandao akilalamika. Au unafikiri hajui kuwa kuna watu flani ndiyo walisimamia ishu ya yeye kutoswa?

 

 

 

 

 

No comments