ASANTE LENGAI OLE SABAYA

 Sabaya jela miaka 30

LENGAI Ole Sabaya, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, amehukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la unyang'anyi wa kutumia silaha. Pamoja naye, wapo wengine wawili.

Katika hali ya kawaida ya kibinadamu, hili la kufungwa siyo jambo ambalo ungependa mwenzako limtokee, hasa kwa uwingi wa miaka aliyohukumiwa, ingawa pia haipendezi mtu anapovunja sheria ambayo kimsingi alipaswa kuisimamia.

Sitapenda kuingia kwa undani juu ya kile alichokifanya, kwa sababu tayari mahakama imejiridhisha, pasipo shaka kuwa alifanya jinai. Hata hivyo, anayo haki ya kukata rufani na nani anajua, anaweza kushinda na kurejea uraiani.

Lakini vyovyote itakavyokuwa, Sabaya ametupatia somo moja kubwa sana ambalo wala hauna haja ya kuwa na Shahada ya Uzamivu ili kulielewa vyema. Linaeleweka kirahisi kabisa, ili mradi tu, ukubali kwamba ni somo.

Katika umri wake wa miaka 34, dogo alifikia levo za juu kabisa kiasi kwamba alikuwa mmoja kati ya 'Untouchables' wachache tuliobarikiwa kuwa nao hapa nchini.

Akiwa DC tu, (yes, Mkuu wa Wilaya ni mtu mdogo tu kimuundo serikalini, licha ya ukweli kuwa ni mwakilishi wa Rais katika eneo lake. Juu yake kuna watu wengi kabla hajamfikia aliyemteua), Sabaya alikuwa na nguvu za ajabu!

Kama uliifuatilia vizuri kesi yake, kuna mambo alikuwa anafanya kwa sababu tu alikuwa shahiba wa Rais. Binafsi, niliwahi kumsikia akihojiwa siku chache kabla hajakamatwa, akijisifu kuwa alikuwa na uwezo wa kumpigia Rais Magufuli simu hata saa nane za usiku.

Can You Imagine! Kwa namna nilivyokuwa nikimfuatilia marehemu Magufuli, ninaamini kabisa wapo mawaziri ambao hawakuthubutu kumpigia mida hiyo.

Achana na alichokuwa akiongea naye, nazungumzia tu hiyo fursa! Katika kipindi kile, wenye fursa hizo walikuwa wachache na bahati nzuri, wengi wao wanafahamika.

Sabaya alijisahau, akaamini mambo yatakuwa vile milele, hakuweza hata kujikumbusha kuwa baadhi ya matendo yake yalikuwa ni jinai na wanasheria wanasema jinai haifi!

Kwa nini ninasema Asante Sabaya? Ninasema hivi kwa sababu watu wa aina yake wapo wengi, siyo tu wale walioko serikalini, lakini hata kwenye taasisi za umma na binafsi.

Vyeo hivi ni kama makoti ya kuazima, muda wowote mwenye lake atakuja kulichukua, tena bila kulazimika kukutaarifu ili angalau ulifue.

Wapo watu wenye hizo nafasi za kufanya maamuzi au kutoa maelekezo, wanasahau kwamba ipo siku watakuja wengine kukaa hapo walipo.

Wamejaa dharau, viburi na jeuri ya madaraka. Wanajiona wao kama watu spesheli hivi, kwamba hakuna zaidi yao. Wapo baadhi yao, wanaogopwa na kunyenyekewa kuliko hata waliowateua kukamata nafasi hizo.

Yes, ukiwa na nafasi, hasa ya uongozi, lazima uwe imara, usiyeyumba na mwenye uthubutu, ili mradi tu, shughuli tarajiwa ziende kama inavyotakiwa.

Lakini, tujifunze kuwa na kiasi. Siyo kila jambo linahitaji nguvu kulifanya liende, au dharau kwa unaowaongoza, kejeli na majigambo. Maisha huwa ni magumu sana cheo hicho kikiondoka.

Wapo baadhi yetu wanatumia nafasi walizokabidhiwa kuwaumiza wenzao, kwa sababu tu ya ama tamaa, wivu, ushamba au hata kujionesha kuwa wao ndiyo wao.

Ukiwa muungwana kwa unaowaongoza, uongozi wako utapata baraka za Mungu, naye atakubariki udumu hapo ulipo, lakini ukienda kinyume anguko lako litapikiwa pilau mlango wa pili.

Kama mtu ambaye aliweza kuingia popote katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro na kufanya lolote alilotaka hivi sasa ni mfungwa, wewe ni nani usiwaze kuwa kesho yaweza kuwa zamu yako.

Kuna baadhi ya watendaji katika nyadhifa zao serikalini, wanajiona miungu watu, kisa tu kule juu kuna mtu wa kumlinda. Wapo wengine ni mabosi huku kwenye sekta binafsi, wanawaumiza wenzao kwa sababu tu ni maswahiba wa wenye mali.

Cheo, hata kiwe kikubwa vipi, kina mwisho na ukikitumia kwa ubaya, kitakulipa ubaya pia!

 

 

 

No comments