MKUU WA MKOA RUVUMA AKAGUA UKARABATI UWANJA WA NDEGE
Na Stephano Mango, Songea
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akiwa
ameongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama, amekagua mradi wa ukarabati wa
kiwanja cha ndege cha Songea ambacho serikali imetoa shilingi bilioni 37.09
kutekeleza mradi huo.
Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo, Mkuu wa
Mkoa ameishukuru serikali ya Awamu ya sita kwa kuhakikisha kuwa Tanzania na
Mkoa wa Ruvuma unaendelea kufunguka katika Nyanja mbalimbali za usafiri ukiwemo
usafiri wa anga.
“Leo nimefika hapa katika uwanja wa ndege wa Songea kukagua kazi
ambazo zimekuwa zinaendelea za kukarabati uwanja huu, ikiwemo kuurefusha uwanja
na miumbombinu ambayo sasa imewezesha kuongeza ratiba ya
safari za ndege kutoka mara mbili kwa wiki hadi mara tatu kuanzia mwezi ujao,"
alisema RC Ibuge.
Brigedia Jenerali Ibuge ametoa rai kwa wananchi mkoani Ruvuma , mikoa
jirani na Nyanda za Juu Kusini kuutumia uwanja wa ndege wa Songea ambao sasa
upo tayari kutumika kusafiri kwa haraka ndani ya Tanzania na
kuelekea maeneo mengine duniani.
Amesema kuanzia Novemba Mosi mwaka huu Shirika la Ndege Tanzania
ATCL litaanza kutoa huduma za usafiri wa anga toka Dar es salaam hadi Songea
mara tatu kwa wiki kwa siku za Jumatatu, Jumatano na Ijumaa na kwamba Mashirika
mengine ya ndege tayari yamepanga kuanza kuutumia uwanja wa ndege wa Songea
likiwemo Shirika la Auric Air.
Mkuu wa Mkoa anayakaribisha mashirika mengine ambayo yanaliona
soko la usafiri wa anga la Kusini kupitia Songea wafike kwa sababu uwanja wa
ndege upo salama na kwamba kiu ya wananchi wa Ruvuma ni kuhakikisha kuwa
biashara zinafanyika kwa haraka zaidi ndani na nje ya nchi kupitia usafiri wa
anga.
Hata hivyo Brigedia Jenerali Ibuge amesema kufunguliwa kwa
uwanja wa ndege wa Songea, kuna fungua fursa za uwekezaji
na utalii, kwa sababu Mkoa una vivutio vya kila aina
likiwemo ziwa Nyasa, Hifadhi ya Taifa ya Nyerere, Mto Ruvuma, milima ya
Livingstone na maeneo mengi yenye utalii wa kihistoria na kiutamaduni.
Kwa upande wake Meneja wa Ndege wa Songea Jordan Mchame amesema
mara baada ya serikali kukarabati kiwanja cha ndege, idadi ya abiria inazidi
kuongezeka ambapo ndege ya Bombadier yenye uwezo wa kubeba abiari 76 hivi sasa
inabeba abiria kati ya 65 hadi 74.
“Hali hiyo inaonesha kwamba kuna abiria wengi wanaosafiri kwa
ndege kwa kutumia uwanja wa ndege wa Songea, usafiri wa anga ni wa
haraka na salama kuliko aina nyingine zote za usafiri, kadri idadi ya abiria
inavyoongezeka tunatarajia hata gharama za nauli zitapungua," alisisitiza
Mchami.
Hata hivyo amesema kabla ya ATCL kuanza kutoa huduma, nauli ya
ndege binafsi kutoka Songea hadi Dar es salaam kwenda pekee ilikuwa kati ya
shilingi 500,000 hadi 600,000 ambapo hivi sasa kupitia ATCL nauli
kwenda ni shilingi 250,000 ,ambapo kwenda na kurudi ni shilingi 375,000
Naye Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Lazack
Alinanuswe akizungumzia mradi wa ujenzi wa uwanja huo, unaogharimu bilioni
37.09, amezitaja baadhi ya kazi ambazo zimekamilika kuwa ni barabara
ya kurukia na kutua ndege na kwamba kilichobakia ni mnara na
taa za kuongozea ndege ambavyo vinaendelea kukamilishwa.
Kiwanja cha ndege wa Songea ni miongoni mwa
viwanja bora vya ndege Tanzania ambacho kilijengwa kati ya mwaka
1974 hadi 1980 na kiliwekewa lami hivyo kuwa na uwezo wa kutua ndege majira
yote masika na kiangazi.

Post a Comment