MKUU WA MKOA RUVUMA AAGIZA VYANZO VYA MAJI KULINDWA
Na Stephano Mango, Songea
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma
Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amekagua vyanzo vya maji kwenye
miradi ya maji Ndongosi na Liula wilayani Songea na kuagiza vyanzo
hivyo kulindwa ili viwe endelevu.
Brigedia Jenerali Ibuge
amesikitishwa na uharibifu wa vyanzo hivyo unaoendelea kufanywa na wananchi kwa
kulima mazao na shughuli nyingine za kibinadamu hali inayosababisha vyanzo
hivyo kuwa katika hatari ya kutoweka.
“Naagiza kila kijiji
kuitisha mkutano mkuu wa kijiji, kati ya ajenda zake kuu, iwe ni namna gani ya
kukabiliana na tabia hii ya kuharibu vyanzo vya maji,nimeona miti
inavyoangushwa kama haina mwenyewe’’,alisema RC Ibuge.
Hata hivyo alisema
serikali inapenda watu wajipatie kipato kutokana na kilimo,ametahadharisha kuwa
shughuli za kinadamu ndizo zinazoathiri vyanzo vya maji.
Ametoa rai kwa watalaam
wote wa maji wakiwemo RUWASA na Bonde la Maji la Ziwa Nyasa,waende vijijini ili
kutoa elimu ya mazingira kwa wananchi na kuweka ramani kwenye eneo zima
ambalo lenye vyanzo vya maji ambapo ameagiza utekelezaji wa maagizo
hayo ufanyike kabla ya Desemba Mosi mwaka huu.
“Tusiseme tuna changamoto
ya tabianchi ni sisi wenyewe ndiyo tunaoharibu kwa kukamata miti,kulima hadi
kwenye kingo za mito ,tunachoma moto misitu na kuvunja sheria mbalimbali za
mazingira’’,alisema RC Ibuge.
Awali akitoa taarifa ya
utekelezaji wa miradi ya maji ya kijiji cha Ndongosi
na Liula kwa Mkuu wa Mkoa,Meneja RUWASA Wilaya ya Songea Mhandisi
Mathias Charles alisema mradi wa maji Ndongosi ulisanifiwa kwa zaidi ya
shilingi milioni 332.
Hata hivyo alisema kati
ya fedha hizo zaidi ya shilingi milioni 23 ni fedha za maandalizi ya
mradi,zaidi ya shilingi milioni 51 ni za usimamizi na zaidi ya shilingi milioni
256 ni fedha za ujenzi wa mradi wa maji.
Ameutaja mradi wa maji
Ndongosi ulisanifiwa kuhudumia wakazi wapatao 3,175 wenye mahitaji ya maji lita
119,062.5 kwa siku na kwamba chanzo cha maji kutoka mto
Mlaimonga kina uwezo wa kuzalisha maji lita 902,016 kwa siku na
kwamba mradi umefikia asilimia 98.
Kuhusu mradi wa maji wa
kijiji cha Liula,Mhandisi huyo wa maji amesema mradi huo awali, ulisanifiwa kwa
gharama ya zaidi ya shilingi bilioni moja ambapo RUWASA kwa kutumia
watalaam wake wa ndani wamefanikiwa kumaliza shughuli zote kwa shilingi milioni
56 ambapo mradi umekamilika na unahudumia watu wapatao 4,320.
Hata hivyo amezitaja
changamoto kuu zinazoikabili miradi hiyo ni uharibifu wa vyanzo vya
maji unaofanywa na wananchi kwa kuchoma moto hovyo,kulima kwenye vyanzo na
kukata miti.

Post a Comment