DAKTARI MIREMBE ATAKA WAJAWAZITO KUACHA MITUNGI
MKURUGENZI Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Magonjwa ya Akili Mirembe Dkt. Paul Lawale amewaasa akina Mama kuacha matumizi ya vilevi wanapokuwa wajawazito ili kuwanusuru watoto walio tumboni kuzaliwa wakiwa na matatizo ya afya ya akili.
Dkt. Lawale amesema hayo Jijini Dodoma wakati
akisoma tamko la siku ya maadhimisho ya afya ya akili duniani yanayoadhimishwa
Oktoba 10 kila mwaka kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima.
Amesema mama mjamzito anapokunywa pombe anamuweka
hatarini mtoto atakayezaliwa kwani inaweza kumsababishia athari katika ukuaji
wa ubongo kwa mtoto aliye tumboni na hivyo kumsababishia tatizo la afya ya
akili pindi atakapozaliwa.
“Tunapoangalia ongezeko la watu wenye matatizo
ya afya ya akili, lazima tuangalie tangu mtoto anapokuwa tumboni, wapo akina
mama wengi wanatumia vilevi wanapokuwa wajawazito hii ina athari kwa mtoto
aliye tumboni, " alisema Dkt. Lawale.
Ameongeza kuwa Mama mjamzito anapotumia vilevi
inasababisha ukuaji wa ubongo wa Mtoto kuathirika na kusababisha Mtoto kuzaliwa
na matatizo ya afya ya akili na kuendelea kuongeza idadi ya wagonjwa wenye
matatizo ya afya ya akili nchini.

Post a Comment