WAKALA UNUNUZI WA MAHINDI RUVUMA WADAIWA KUWATENGA WAKULIMA, WANUNUA MAZAO YA WAKUBWA

 Single News | Songea Municipal Council

NA STEPHANO MANGO, SONGEA

WAKULIMA wa zao la mahindi Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma wameilalamikia Serikali kupitia wakala wa hifadhi ya Taifa (NFRA) Kanda ya Songea kwa kushindwa kununua mahindi yao badala yake wananunua mahindi ya wafanyabiashara wakubwa na viongozi wa kada mbalimbali nyakati za usiku.

Wakizungumza mbele ya waandishi wa habari jana nje ya eneo la NFRA Kanda ya Songea kwa nyakati tofauti mjini hapa, wakulima hao ambao wameomba majina yao yahifadhiwe walisema kuwa mahindi yao hayanunuliwi kwa kigezo kuwa ni machafu na hayana ubora wakati jambo hilo sio la ukweli.

Walisema kuwa nyakati za usiku kumekuwa na magari ambayo yanaingia moja kwa moja ndani na kwenda kupimwa kwa lengo la kuuzwa mahindi  bila kuzingatia utaratibu wa kufuata foleni kama ulivyopangwa  hali ambayo imekuwa ikiwashangaza na kuhoji kuwa mahindi hayo ni ya watu gani na yanatoka wapi.

Walisema kuwa awali waliambiwa kuwa  watanunua mahindi toka kwa wakulima gunia 80, baadae wakasema watanunua gunia 50 kwa kila mkulima lakini leo wanasema kuwa watanunua mahindi gunia 10 kwa kila mkulima, kitu kinachowashangaza kwani wako kwenye foleni kwa muda wa wiki mbili na kila mmoja akiwa na magunia zaidi ya mia moja.

“Tunashindwa kuelewa hatima yenu ni ipi katika ununuzi wa mahindi yetu, kila kukicha tunaandikisha majina ya wakulima 20 lakini katika kwenda kupima wakulima 7 tu kati ya 20 ndio wanafanikiwa kupimiwa mahindi yao na 13 waliobaki mahindi yao yanatolewa nje kwa madai kuwa ni machafu, huku tukiwa tunadaiwa fedha za usafiri wa mahindi kutoka vijijini kuyaleta hapa," alisema mmoja wa wakulima hao.

Walimeiomba Serikali kuona umuhimu wa kuangalia kwa upana wake suala la ununuzi wa zao hilo kutoka kwa wakulima kwa sababu ndio zao pekee kwao na wakati wa msimu ujao wa kilimo unakaribia.

Kwa upande wake Meneja wa NFRA Kanda ya Kusini Mohamed Nondo alisema kuwa fedha wanazopokea toka Serikalini ni ndogo, hivyo kadri wanavyopokea ndivyo wanavyonunua, na kwamba kwa sasa wanatarajia kununua tani 4000.

Nondo alisema kuwa madai mengine yanayotolewa na wakulima hao hayana ukweli wowote na kama kuna mkulima ana ushahidi wa jambo hilo basi aupeleke kwenye vyombo vinavohusika ili hatua ziweze kuchukuliwa.

 

No comments