SIMBACHAWENE, KILANGI WAMPELEKA GWAJIMA KWA DPP, DCI

WAZIRI wa MNambo ya Ndani, George
Simbachawene na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Profesa Adelardus Kilangi wamesema
azimio la Bunge la kutaka vyombo vingine vimchukulie hatua Mbunge wa Kawe (CCM)
Askofu Josephat Gwajima linatosha kumfanya Mkurugenzi Mkuu wa Upelelezi wa
Makosa ya Jinai kuanza uchunguzi wa shauri hilo.
Bunge liliazimia Gwajima na Mbunge wa Ukonga (CCM), Jerry
Silaa wasimamishwe kuhudhuria vikao vya mikutano miwili ya Bunge baada ya
kuwatia hatiani kwa kusema uongo, kushusha hadhi na heshima ya Bunge.
Wakati wa kuhitimisha adhabu kwa wabunge hao, Spika Job
Ndugai alisema Bunge limenawa mikono kwa upande wake, hivyo kinachotakiwa ni
Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene na Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Profesa Kilangi kutazama namna wanavyoweza kufanya.
Ndugai alisema kama hawatamhoji mbunge huyo, basi wasishangae
kuitwa mbele ya kamati ya maadili ambayo alisema itakuwa na kauli juu yao
wenyewe si kazi ya Bunge tena.
Akizungumza katika viwanja vya Bunge baada ya azimio hilo
kutolewa, Profesa Kilangi alisema jambo hilo litaangukia chini ya Mkurugenzi
Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kwa sababu ni suala la uchunguzi.
Alisema uchunguzi unalenga kufahamu kama jinai imetendeka kwa
shauri la Gwajima ama la.
“Akishafanya uchunguzi wake atalipeleka katika hatua
inayofuata ambayo ni kwa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP). Naye
atapima kuona kama kuna jinai hapa na upo ushahidi wa kutosha wa kuthibitisha
kuwa jinai,” alisema.
Alisema akishathibitisha kwamba kuna ushahidi wa kutosha kwa
mamlaka yake atafungua kesi mahakamani.
“Lakini ni vyema kutambua mamlaka ya DPP ni mamlaka
yasiyoingiliwa na taasisi yoyote, isiyoshinikizwa na taasisi yoyote, kwa hiyo
na yeye atajiridhisha. Atakavyokuwa ameona na akiona kuna jinai imetendeka na
ushahidi wa kutosha atalipeleka anavyoona inafaa,” alisema.
Alipoulizwa nani anakwenda kushtaki ili uchunguzi uanze,
Profesa Kilangi alisema lipo azimio la Bunge linatosha kumfanya DCI kuanza
uchunguzi.
Naye Waziri Simbachawene alisema maagizo ya Spika kuhusu kiongozi
huyo ameyapokea, lakini hawezi kusema jambo lolote hadi atakaposhauriana na
wataalamu wake.
Alisema hawakufanya haraka kumhoji Gwajima kutokana na suala
hilo kuwa na mchanganyiko wa masuala ya dini.
“Ni kweli nimemsikia, lakini haya mambo yameunganisha na
imani za kidini. Kabla sijasema jambo lolote lazima kwanza nijiridhishe kutoka
kwa wenzangu kama tunaona iko haja ya kufanya hivyo ili tusije tukaingilia
uhuru wa kuabudu,” alisema.
Hata hivyo, alisema akijiridhisha na kupata ushauri kuwa
inawezekana kuhojiwa, basi watamuita na kumhoji ili kupata ukweli wa kauli zake.
Silaa asindikizwa na askari
Hata hivyo, jana Gwajima hakuwepo bungeni wakati mjadala wa
suala lake ukiendelea, tofauti na Silaa aliyehudhuria na Spika Job Ndugai
alimuamuru atoke nje ya ukumbi wa Bunge huku akiwaagiza askari wamsindikize
mbali na viwanja vya Bunge.
Baada ya kauli hiyo, Silaa alisimama na kunyanyua mkoba wake
mweusi na kuweka kitabu kimoja ndani ya mkoba huo kabla ya kuchukua simu zake
na kutoka huku akiwa amesindikizwa na askari wawili.
Askari hao walimweka Silaa katikati na kuongozana naye hadi
nje ya viwanja vya Bunge kwa kupitia lango kuu la kuingilia bungeni.
Chanzo: Mwananchi

Post a Comment