RC DKT SENGATI: ASILIMIA 75 YA WAKAZI MIJINI WANAISHI KATIKA MAKAZI HOLELA
Baadhi ya wadau wa Ardhi wa Mkoa wa Shinyanga wakiwa
katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati
pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Bi. Jasinta Mboneko mara baada ya
ufunguzi wa kikao kazi cha tathimini ya utekelezaji wa Mpango kazi wa mwaka
2020/2021 kilichokaa jana katika ukumbi wa Manispaa ya Shinyanga
Na Anthony Ishengoma, Shinyanga.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati
amesema zaidi ya asilimia 75 ya watanzania wanaoishi mjini wanaishi katika
makazi holela hali hiyo ikichangiwa na kasi ndogo ya serikali ya kupanga na
kupima viwanja katika miji mingi nchini.
Dkt Sengati aliongeza kuwa hali hiyo imepelekea kuwepo
kwa makazi yasiyo rasmi katika miji mingi ndiyo maana Serikali
kupitia Wizara ya Ardhi na TAMISEMI ilianzisha Programu ya Urasimishaji Nchini
ya Mwaka 2013-2023 inayoshirikisha sekta binafsi katika
urasimishaji kwa lengo la kuongeza kasi ya upangaji, upimaji na
umilikishaji wa ardhi.
Dkt. Sengati alisema hayo jana wakati wa ufunguzi wa
kikao kazi cha tathimini ya utekelezaji wa Mpango kazi wa mwaka 2020/2021
kilichokaa kupanga malengo ya mwaka, kujadili changamoto za utatuzi wa mogogoro
ya ardhi ya wananchi pamoja na kujipanga kukamilisha utekelezaji wa Programu ya
Kitaifa ya Urasimishaji Makazi ya 2013-2023.
Aidha Dkt. Sengati aliongeza kuwa lengo la kuongeza
kasi ya kupima, kupanga na kurasimisha ardhi kuimarisha usalama wa miliki za
ardhi na kuwajengea wananchi uwezo wa kutumia ardhi yao kama mtaji katika
maendeleo na uchumi wao na kumwezesha mwananchi kupata hatimiliki kisheria na
hivyo kuimarisha usalama wa miliki ya ardhi na kuitumia ardhi hiyo
kama mtaji kiuchumi na kimaendeleo.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Bi Jasinta Mboneko
aliwataka wataalamu hao wa ardhi kuhakikisha wanamaliza migogoro ya ardhi
Mkoani Shinyanga kwa kupima viwanja lakini pia katika upimaji wao wazingatie pia
maeneo kwa ajili ya shughuli za kijamii ikiwemo maeneo ya ujenzi wa Shule.
‘’Maeneo yapimwe lakini pia tutenge maeneo ya
uwekezaji lakini pia mnapopanga mtenge pia maeneo ya shughuli za kijamii kama
maeneo ya Shule ambayo pia ni changamoto, kwa hiyo tukumbuke maeneo hayo.”
Naye Bw. Ezekiel Kitilya Mkurugenzi wa Idara ya Ardhi Mkoa wa
Shinyanga alisema kuwa Kikao kazi hicho kinawakutanisha wadau wa Ardhi Mkoa wa
Shinyanga ikiwemo Benki ya NMB ambayo inaingia kwa utaratibu mpya
utakaohakikisha wananchi wanapata miliki salama ya ardhi na serikali inapata
mapato yake.
Bw. Kitilya aliongeza kuwa wadau wa ardhi mkoani Shinyanga
wanakutana pamoja ili kujenga uelewa lakini pia kufanya tathimini ya malengo waliojiwekea
kwa mwaka wa fedha ulioisha lakini na kujipanga upya kwa mwaka mpya wa fedha
ikiwemo kujipanga kutekeleza Programu ya Urasimishaji Nchini ya Mwaka
2013-2023.

Post a Comment