DCI WAMBURA: UCHUNGUZI UMEBAINI HAMZA ALIKUWA GAIDI WA KUJITOA MUHANGA

HUKU mamilioni ya
Watanzania wakisubiri kwa hamu kujua hatima ya uchunguzi wa Polisi juu ya
mauaji ya watu watano yaliyowahusisha polisi na raia mmoja, hatimaye Mkurugenzi
wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Camillius Wambura amedai uchunguzi umebaini
Hamza Mohammed alikuwa gaidi wa kujitoa mhanga.
Hamza aliuawa na polisi Agosti 25, mwaka huu baada ya kuwaua kwa risasi askari
wanne, watatu kati yao wa polisi na mmoja wa kampuni binafsi ya ulinzi jirani
na ulipo ubalozi wa Ufaransa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza leo Alhamisi Septemba 2, 2021 jijini Mwanza na waandishi wa habari
Wambura amesema uchunguzi huo ulijikita katika mambo makuu matatu ambayo ni
kutaka kutambua Hamza Mohammed ni nani, nini kilimsukuma Hamza kwenda kufanya
tukio lile na kutaka kutambua mshiriki mwingine katika tukio hilo.
Wambura amesema katika uchunguzi huo polisi imebaini kwamba Hamza alikuwa
akiishi kisiri huku akiwa amegubikwa na viashiria vyote vya ugaidi.
"Amekuwa akijifunza mambo mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii ambayo
kwa kipindi kirefu amekuwa akijifunza mambo ya kigaidi kwa kuangalia mitandao
ambayo inaonyesha matendo ya Al-Shabab na makundi kama ISIS yanayoendelea na
wagaidi wengi hujifunza kupitia mitandao hiyo," amesema Wambura.
Amesema kwamba kitendo alichokifanya Hamza kilikuwa ni cha ugaidi wa kujitoa
mhanga.
"Tabia na matendo ya Hamza aliyapata kupitia mawasiliano aliyokuwa nayo na
watu wanaoishi katika nchi zenye matendo ya kihalifu ikiwemo ugaidi hasa wa
kupitia mtandao yanayojulikana kama "Radicalisation through social
media)," amesema Wambura.
Kuhusu taarifa zinazodai kwamba Hamza aliwashambulia askari hao kwa sababu
walimdhulumu madini yake, Wambura amekanusha na kusema katika uchunguzi huo
wamebaini kwamba Hamza hakuwa na madini wala fedha katika mazingira yale.
"Hamza hakuwa na madini wala pesa na hakuwa katika nafasi yoyote ya
kumiliki madini wala pesa mbali ya kwamba watu wengi wameongea kwamba alikuwa
anamiliki migodi ya madini kule Chunya na maeneo ya Makongolosi uchunguzi wetu
umebaini hali hiyo ya maisha ilikwisha simama muda mrefu," ameongeza
Wambura.
Wambura ameongeza kuwa taarifa ya uchunguzi huo pia imebaini kwamba Hamza
alikuwa kwenye kundi la magaidi wanaoamua kuifia dini.

Post a Comment