SERIKALI KUPUNGUZA TOZO ZA LESENI MITANDAONI
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Innocent Bashungwa, amesema Serikali inakwenda kuondoa asilimia
hamsini ya ada za tozo mbalimbali za leseni kwenye marekebisho ya Kanuni za
maudhui ya mtandaoni na maudhui ya utangazaji katika redio na televisheni
yaliyofanywa hivi karibuni ili kuzalisha ajira na vipato.
Bashungwa alisema hayo jana Septemba
1, 2021 Dodoma katika kikao cha kupokea taarifa ya maboresho ya Rasimu ya
Marekebisho ya Kanuni za Maudhui Mtandaoni za mwaka 2020 na Kanuni za Maudhui
ya Utangazaji katika Redio na Televisheni za mwaka 2018 yaliyotolewa na wadau
mbalimbali hivi karibuni.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pauline Gekul na
Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson
Msigwa.
“Serikali inayoongozwa na Rais
Samia Suluhu Hassan imeamua kwa dhati kufanya marekebisho ya kanuni hizi kwa
kuwashirikisha wadau wake ambapo sasa katika kipindi kifupi kijacho
tutashuhudia maboresho yanaleta matumaini na mapinduzi makubwa kwenye sekta na
wadau wategemee ongezeko la ajira na kuboreka kwa vipato vyao kwa kiwango
kikubwa,” alisema Bashungwa.
Bashungwa alisema ada kwa Leseni
za ‘simulcasting’ imeondolewa kabisa ambapo ameeleza kwamba hatua hiyo
imefikiwa baada ya kuzingatia maoni ya wadau ya kuiomba Serikali tahfifu ya ada
husika ili waweze kumudu kulipa bila faini au kulimbikiza madeni ambapo amesema
watoa huduma wanatazamiwa kuongezeka kutokana na viwango vya ada kuwa rafiki.

Post a Comment