WANANCHI WAMTUHUMU MWENYEKITI WA KIJIJI WIZI FEDHA ZA MICHANGO YA MAENDELEO
 
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati
akiongea na wananchi wa Kijiji cha Mwiseme Kata ya Solwa Wilaya ya Shinyanga
alipofika Kijijini hapo kwa lengo la kuwasikiliza lakini pia kutoa suluhisho la
changamoto walizonazo katika Kijiji hicho.
Na Anthony Ishengoma, Shinyanga
Wananchi wa Kijiji cha Mwiseme Kata ya Solwa
Wilaya ya Shinyanga kwa nyakati tofauti wameutuhumu  uongozi wa
Kijiji akiwemo Afisa  Mtendaji wa  Kijiji kwa ubadhilifu wa
fedha za wananchi Kijijini hapo ambazo wamekuwa wakizichanga kwa ajili ya
ujenzi wa Shule pamoja na Zahanati na miradi mingine ya Maendeleo.
Tuhuma hizo za wananchi kwa Mwenyekiti wao wa
Kijiji Bw. Deus Manumba zilitolewa na wanakijiji hao mbele ya Mkuu wa Mkoa wa
Shinyanga Dkt. Philemon Sengati aliyefika Kijijini hapo kujionea maendeleo yao
lakini pia kusikiliza kero zao baada ya kubaini kuwepo kwa tuhuma hizo.
Bw. Jigela Salanya Mkazi wa Kijiji cha Mwiseme
alilalamika mbele ya Mkuu wa Mkoa kuwa Mwenyekiti wa Kijiji alichangisha fedha
kiasi cha Tsh. 12 elfu kutoka kwa wananchi kijijini hapo kwa ahadi kuwa
atasaidia kuwapati vitambulisho vya Taifa zikiwa ni pamoja na kugharamia
usafiri kufuatilia vitambulisho vyao lakini mpaka sasa zoezi hilo
halijafanyikiwa hivyo kumtaka Mkuu wa Mkoa kumuondoa kiongozi huyo.
Katika hatua nyingine Bw. Zambi Ruchambagula
Jegu aliwekwa ndani na viongozi wa Kijiji hicho kwa sababu ya kuhoji kuhusu
kusomewa mapato na matumizi ya Kijiji hicho na badala yake Mwenyekiti na watu
wake walimfuata mke wake na kuiba  kiasi cha Shilingi laki nne na
alitumia fursa hiyo kuomba Mkuu wa Mkoa kusaidia ili aweze kurejeshewa fedha
yake.
Kama hiyo haitoshi Bw. Lunde Manyabili
alisema  Mwenyekiti huyo wa Kijiji Bw. Deus Manumba pia
alishachangisha wananchi Kijijini hapo fedha kiasi cha Tsh. 13000/= ili aweze
kujenga Choo cha Shule lakini wakazi hao wanashangaa kuona choo hicho
kimejengwa kwa miti na hivyo kuhatarisha maisha ya wanafunzi shuleni hapo.
Malalamiko hayo ya wanakijiji hayo yakamsukuma
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati kuwasimamisha kazi Mtendaji wa
Kata na Mwenyekiti wa Kijiji ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili.
‘’Hizi tuhuma ni kubwa muno na mimi kama
msimamizi wa amani mkoa wa Shinyanga siwezi kuendelea kuvumila haya kwa hiyo
ninatamka rasmi kwamba tunamsimamisha kazi Mwenyekiti, Mtendaji wapishe
uchunguzi ambao utabainisha ukweli kati yenu ninyi wananchi na wao."
Dkt. Sengati aliongeza kuwa uchunguzi huo
utaangalia suala zima la ubadhilifu wa fedha lakini pia wa kimaadili ili
ikibainika wanamapungufu kimaadili basi wachukuliwe hatua za kinidhamu lakini
kama watabainika wanakabiliwa na upotevu wa fedha basi hatua za kisheria
zitachukuliwa dhidi yao.
Kufuatia hali hiyo Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga
Bi. Jasinta Mboneko amewataka watendaji katika ngazi ya Tarafa, Kata na Vijiji
kuhakikisha wanasimamia miradi ya maendeleo na kuhakikishia mapato na matumizi
yanawekwa wazi kwa ajili ya wananchi kupata uelewa wa matumizi ya fedha
yao.    

Post a Comment