RC DAR APIGA MARUFUKU MICHANGO MASHULENI

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amepiga marufu
michango inayotozwa kwa wazazi wa wanafunzi wa shule za Serikali mpaka hapo
atakapotoa kibali chake.
Ametoa agizo hilo leo Jumatano Septemba 1,
2021, kwenye mwendelezo wa kusikiliza kero za wakazi wa mkoa huo ambapo leo ni
zamu ya Wilaya ya Ilala na mkutano huo unafanyika viwanja vya Ghana Buguruni.
Hatua hiyo ilifikiwa baada ya mmoja wa
wananchi, aliyejitambulisha kwa jina la Abinani Lukwale, kueleza kuwa michango
imezidi kuwa mingi shuleni na mengine wasipotoa watoto wao hurudishwa nyumbani
au kunyimwa kufanya mitihani ambapo kila siku hutakiwa kutoa Sh300 na Jumamosi
Sh1,000.
Akilitolea maagizo Makalla amesema kuanzia sasa
anapiga marufuku michango hiyo mpaka pale itakapopata ridhaa yake.
"Kama shule ina wanafunzi 2,000 ina maana
shule inakusanya Sh600,000 na hapo bado Sh1,000 ambazo wanazikusanya kila
Jumamosi kwa watoto hao.
"Ukweli ni kwamba michango hiyo
huwaongezea mzigo wazazi wakati serikali ishaamua kutoa elimu bila malipo,hii
sitaikubali ndani ya uongozi wangu," amesema.
Kutokana na hilo amesema kuanzia sasa michango
yoyote lazima iidhinishwe na yeye mwenyewe na hii ni baada ya kikao cha wazazi
na uongozi wa shule kama ambavyo muongozo wa elimu unavyoelekeza.
Katika hatua nyingine amekataza biashara
zinazofanywa pembezoni mwa shule ili kuwawekea mazingira mazuri watoto kusoma.
Badala yake ametaka kuwekwa utaratibu wa watu
watakaotambulika na uongozi wa shule kufanya biashara zao ndani ya shule.
Ameagiza watendaji kulisimaamia hilo kwa kutoa
elimu na kuweka vibao vya makatazo.

Post a Comment