ERB YATOA ADHABU KWA WAHANDISI 17
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Maadhimisho Siku
ya Wahandisi Tanzania kwa mwaka 2021, Prof. Bakari Mwinyiwiwa, akizungumza na waandishi
wa habari (hawapo pichani),kuhusu maadhimisho hayo yatakayofanyika
kwa siku mbili kuanzia tarehe 02 hadi 03 Septemba 2021 katika Ukumbi wa Dkt.
Jakaya Kikwete, mkoani Dodoma.
IMEELEZWA kuwa wahandisi 17 wamechukuliwa hatua mbalimbali
za kisheria kwa kukiuka maadili na taratibu za taaluma yao kwa kipindi cha
mwaka wa fedha 2020/2021.
Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Msajili wa Bodi ya Usajili
ya Wahandisi (ERB), Mhandisi Patrick Barozi, wakati akizungumza na waandishi wa
habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Wahandisi Tanzania kwa mwaka 2021 yatakayofanyika
kwa siku mbili kuanzia Septemba Mosi hadi tatu, 2021katika Ukumbi wa Dkt.
Jakaya Kikwete, mkoani humo.
“Wahandisi hawa 17 wamewajibishwa kwa mujibu wa makosa
na adhabu wanazostahili kupewa mfano ikiwemo kujihushisha na masuala ya rushwa,
upendeleo wa kazi, kushindwa kusimamia miradi na kusimamia baadhi ya miradi chini
ya viwango”, amefafanua Mhandisi Barozi.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Maadhimisho
Siku ya Wahandisi Tanzania Mwaka 2021, Mha. Ngwisa Mpembe, akisisitiza jambo kwa
waandishi wa habari (hawapo pichani), wakati akijibu maswali juu ya maadhimisho hayo yatakayofanyika kwa siku mbili
kuanzia tarehe 02 hadi 03 Septemba 2021 katika Ukumbi wa Dkt. Jakaya Kikwete mkoani
Dodoma.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi
ya Maadhimisho hayo, Prof. Bakari Mwinyiwiwa, amesema kuwa zaidi ya wahandisi
600 wanatarajiwa kula kiapo cha utii katika Maadhimisho ya Siku ya Wahandisi kwa
mwaka 2021 ili kuhakikisha wahandisi nchini wanawajibika vyema kwenye taaluma zao
na utendaji wao wa kila siku.
Prof. Mwinyiwiwa amesisitiza kuwa kiapo kitatumika dhidi
ya mhandisi atakapovunja miiko na maadili ya taaluma katika utendaji wake wa kazi
na hivyo vyombo mbalimbali vya kisheria vitatumia kiapo hicho kumchukulia hatua
za kisheria.
“Kiapo kinamkumbusha mhandisi kuzingatia thamani ya
fedha, usalama wa maisha ya binadamu na mazingira, kutoruhusu masuala ya jinai,
dini, jinsia, ukabila, rangi na masuala ya kisiasa katika utekelezaji wa kazi zao
za kiuhandisi”, amefafanua Prof. Mwinyiwiwa.
Mkutano huo utakaobeba kauli mbiu ya“Athari za Mapinduzi ya Nne ya Viwanda kwenye
Miundombinu na Viwanda kwa Uendelevu wa Uchumi wa Kati”utashirikisha wadau mbalimbali
kutoka ndani na nje ya nchi ikiwemo Uganda, Misri na wengine kushiriki
kwa njia ya mtandao ikiwemo nchi ya Afrika Kusini, Rwanda, Botswana, DRC na
Kenya.
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Post a Comment