ASILIMIA 45 YA WATANZANIA WANATIBIWA KWA MITI SHAMBA
KAIMU Naibu Makamu Mkuu
wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), upande wa Taaluma, Profesa Samwel
Kabote amesema asilimia 45 ya watanzania wanatibiwa kwa tiba asili na tiba
mbadala.
Alitoa kauli hiyo wakati akifunga maadhimisho na maonesho ya wiki ya tiba asili
ya Mwafrika Kanda ya Mashariki yaliyofanyika kwenye viwanja vya Soko Kuu la
Chifu Kingalu Manispaa ya Morogoro yaliyowakutanisha wadau wote kwenye mnyororo
wa thamani ya mimea dawa kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania.
"Takwimu zinaonyesha kuwa tiba asili inachangia kwa kiasi cha asilimia 45
katika kutoa huduma za afya kwa Watanzania na asilimia 55 ndiyo madawa mengine
ya madukani, kwa hiyo asilimia hizo sio ndogo kama ambavyo watu wengi wanadhani
maana naamini wengi zaidi wanaikimbilia tiba asili katika kutatua changamoto
zao mbalimbali za kiafya na hivyo kupata afya ya kuwawezesha kufanya kazi za
kiuchumi," alisistiza Profesa Kabote.
Aidha amewataka waganga wa tiba asili na mbadala kuendelea na juhudi za
kuboresha dawa hizo kwa kushirikiana na watafiti wa SUA na Chuo cha Afya
Muhimbili na taasisi zingine za kupima ubora na usajili ili zizidi kuaminika na
jamii nzima bila kujali elimu ya mtu, kipato wala rangi yake na hivyo kuongeza
soko na huduma zaidi kwa jamii na kujiongezea kipato.
Profesa Kabote ametoa wito kwa waganga wa tiba asili kushirikiana na watafiti
kote nchini katika kubaini miti dawa ambayo wanaona ina faida kubwa katika tiba
ili ifanyiwe utafiti zaidi na kuongeza thamani ya mimea hiyo ili kupta dawa za
kitanzania nzuri na zenye ubora wa hali ya juu kwa matumizi ya hapa nchini na
nje ya nchi.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufunga maadhimisho hayo
Mkurugenzi wa Shahada za Juu Utafiti, Ushauri na Uhawilishaji wa Teknolojia
Profesa Hesron Karimuribo alisema Wizara ya Afya inatambua mchango mkubwa wa
SUA katika jitihada za kusaidia tiba asili nchini na ndio maana wakapewa nafasi
ya kuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo kwa kanda ya mashariki.
"Kama mkurugenzi mwenye dhamana ya utafiti SUA tumekuwa tukihakikisha
tunafanya tafiti mbalimbali kupitia wataalamu na watafiti wa chuo chetu katika
sekta ya tiba asili kwa kushirikiana na wadau hawa ili kuboresha na kuongeza
thamani dawa zao na namna wanavyotoa huduma lakini pia kuhamasisha upandaji wa
mimea dawa ili isiweze kutoweka kwa kuwa inatumiwa sana na kuvunwa kwa wingi,"
alisema.
Ameongeza kuwa SUA imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kufanya
tafiti za kupata dawa za kukabiliana na ugonjwa wa UVIKO -19 ambapo umepata
dawa mbalimbali ikiwemo dawa maarufu ya SYNADOL ambayo inatumiwa na watanzania
wengi kwa sasa ndani nan je ya Mkoa wa Morogoro kutokana na ufanisi wake katika
kusaidia wagonjwa hao.
Akieleza ushirikiano wa SUA na wadau wa tiba asili Mtafiti Mkuu wa Mradi wa
GRILL Dkt. Faith Mabiki alisema kuwa uanzishwaji wa jukwaa la ubunifu la wadau
wa bidhaa za tiba asili nchini GRILL ni moja kati ya mikakati mikubwa iliyozaa
mafanikio makubwa katika kuwakutanisha wadau wote kwenye mnyororo wa thamani
lakini pia kuwapa sauti ya pamoja na kubadilishana mawazo na uzoefu nchini.
"Sisi kama watafiti wa SUA ambao tumekuwa tukifanya kazi karibu sana na wadau
hawa wa tiba asili, tunajivunia mabadiliko makubwa tunayoyaona sasa tunapofika
kwa kila mganga wa tiba asili kwa kuona namna wanavyofungasha bidhaa zao na
kutengenza dawa katika ubora wa hali ya juu tofauti na zamani ambapo walikuwa
wakiwapatia wateja au wagonjwa wao magome ya miti, majani na kuweka kwenye
mifuko isiyofaa kuweka dawa," alisema Dkt. Mabiki.
Kwa upande wake Mratibu wa tiba asili na tiba mbadala mkoa wa Morogoro Dkt.
Wille –Anne Ngalula alisema kuwa jukwaa la ubunifu la tiba asili Tanzania
lililoanzishwa na SUA linaendeleza malengo na jitihada za Serikali katika suala
zima la utoaji wa dawa na kuboresha afya nchini kupitia tiba asili.
’’Kwa sasa Mkoa wa Morogoro una waganga wa tiba asili waliosajiliwa na Baraza
la Tiba Asili Tanzania wamefikia 1872 na tayari maduka 71 ya tiba asili
yamesajili katika mkoa wa Morogoro, hii inaonyesha mwamko mkubwa uliopo kwa
wganga hawa katika kufuata sheria na kanuni za serikali katika utoaji wao wa
huduma lakini pia muitikio wa wananchi katika kutafuta huduma zao ndio maana
wanaongezeka siku hadi siku na hii inatokana na kazi kubwa iliyofanywa na SUA
pamoja na timu yetu ya mkoa," alieleza Dkt. Ngalula.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyamna vya Waganga wa Tiba Asili Tanzania Mkoa wa
Morogoro (SHIVYATIATA) Ramadhani Sanze ameishukuru SUA kwa kuendelea kuwa mlezi
wa waganga wa tiba asili nchini na kwa jitihada wanazozifanya katika kuboresha
utoaji wao wa huduma kwa wagonjwa kwani imeongeza thamani ya dawa zao lakini
pia kuwajengea kuaminika na kujiamini katika utoaji wa huduma na hivyo
kuwaongezea elimu na kipato.
Maadhimisho ya tiba ya wiki ya tiba asili ya Mwafrika Kanda ya Mashariki
yamefanyika kwa kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo kutoa huduma za ugani kwa
waganga wa tiba asili kwenye maeneo yao ya kutolea huduma, kongamano la
kisayansi la tiba asili kwa njia ya mtandao pamoja na maonesho makubwa ya kanda
ya mashariki yaliyokutanisha waganga wa tiba asili na wadau wengine kwenye
mnyororo wa thamani wa tiba asili kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania.

Post a Comment