SERIKALI YAMWEKEA PINGAMIZI MBOWE KESI YAKE YA KIKATIBA

Serikali imemwekea pingamizi Mwenyekiti wa Chadema, Freeman
Mbowe, katika kesi yake kikatiba, ikitaja sababu nne na kudai kuwa kesi hiyo ni
batili kwa kuwa ina upungufu wa kisheria.
Hivyo Serikali inaiomba mahakama hiyo iifute kesi hiyo bila
kuisikiliza hoja za msingi.
Mbowe alifungua kesi hiyo ya kikatiba Julai 30 mwaka huu,
Mahakama Kuu dhidi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Mkuu wa Jeshi la Polisi
(IGP) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Katika kesi hiyo namba 21 ya mwaka 2021, Mbowe anapinga
utaratubu uliotumika kumkamata, kumweka kizuizini na hatimaye kumfungulia kesi
ya uhujumu uchumi akikabiliwa na mashtaka ya ugaidi.
Kesi hiyo inayosikilizwa na jopo la majaji watatu
linaloongozwa na Jaji John Mgetta, akishirikiana na Jaji Leila Mgonya na Jaji
Stephen Magoiga, ilitajwa kwa mara ya kwanza Agosti 9, mwaka huu ambapo waidai
waliomba siku 14 kuwasilisha majibu yao dhidi ya madai ya Mbowe.
Leo Agosti 30, kiongozi wa jopo la wadaiwa, wakili wa
Serikali Mkuu Hangi Chang’a amekanusha madai ya Mbowe.
Wakili Kibatala kwa upande wake aliieleza mahakama kuwa baada
ya kurejea mambo mbalimbali kuhusiana na kesi hiyo wameona kwamba hakuna haja
ya kuwasilisha kiapo cha ziada.
Kutokana na pingamizi hilo la awali, kama ilivyo kawaida,
mahakama imelazimika kusimamisha kwanza mwenendo wa kesi ya msingi na badala
yake itasikiliza na kuamua kwanza pingamizi la Serikali.
Ikiwa mahakama itakubaliana na hoja za pingamizi la Serikali,
basi itaitupilia mbali kesi hiyo na hicho ndicho kitakuwa kifo chake.
Lakini kama mahakama itupilia mbali hoja za pingamizi la
Serikali basi kesi hiyo itakwenda katika hatua ya pili ambayo ni usikilizwaji
wa hoja za Mbowe katika kesi ya msingi pamoja na hoja za Serikali kuhusiana na
madaia ya Mbowe na kisha itatoa uamuzi.
Katika usikilizwaji wa pingamizi hilo la awali, Wakili
Chang’a aliomba ufanyike kwa njia ya maandishi maombi ambayo mahakama
imekubaliana nayo baada ya mawakili wa Mbowe kueleza kuwa hawana pingamizi
dhidi ya maombi ya Serikali ya kusikiliza pingamizi hilo kwa njia ya maandishi.
Jaji Mgetta ambaye atasikiliza na kuama pingamizi hilo
aliwataka Serikali kuwasilisha hoja zake za maandishi Septemba 6 na Mbowe
kuwasilisha majibu yake ya hoja za pingamizi la Serikali Septemba 9 mwaka huu.
Pia Jaji Mgetta aliiamuru Serikali kama itakuwa na hoja za
nyongeza kuhusu majibu ya Mbowe, kuziwasilisha mahakamani Septemba 13 na
akapanga kutoa uamuzi wa pingamizi hilo Septemba 23, mwaka huu, saa Nane Mchana.

Post a Comment