NAIBU WAZIRI WA AFYA AIPONGEZA ASASI YA ROA SONGEA KWA KUIUNGA MKONO SERIKALI
Na Stephano Mango, Songea
NAIBU Waziri wa Afya na
Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mwanaidi Ali Khamis ameipongeza Asasi
ya Ruvuma Orphans Association (ROA) kwa kazi kubwa ya kutoa elimu juu ya
masuala ya ustawi na maendeleo ya makundi yaliyo katika hatari ya kuathirika au
kuathiriwa na umaskini na magonjwa.
Akizungumza hivi karibuni alipotembea Asasi ya Roa hiyo mjini hapa,
Naibu Waziri Mwanaid Ali Khamis alisema kuwa Serikali ina mipango mingi
ambayo inapaswa kuungwa mkono na wadau wake wa maendeleo zikiwemo Asasi za
kiraia.
Alisema kuwa amefarijika sana kuona kuwa asasi ya Roa imekuwa
ikishiriki kikamilifu kutoa elimu ya kujikinga na magonjwa na upatikanaji wa
mimba za utotoni kwa vijana balehe wenye umri wa miaka 10-19 ambao ni asilimia
22.9 ya idadi ya watanzania wote.
Alisema kuwa hili ni kundi kubwa sana ambalo Serikali imewekeza
nguvu kubwa za kuhakikisha wanalindwa dhidi ya changamoto zinazowakabili
zikiwemo mimba za utotoni , magonjwa ya ngono, utumiaji wa madawa ya kulevya.
“Nimefarijika sana kusikia kuwa Shirika hili limekuwa likitoa
elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto kwani jitihada hizo
zinaunga mkono mpango mkakati wa Taifa wa kutokomeza aina zote za ukatili kwa
makundi hayo “ Alisema Naibu Waziri Mwanaid Ali Khamis.
Awali Mwenyekiti wa Asasi ya Ruvuma Orphans Association (ROA) Mathew Ngalimanayo akitoa neno la utangulizi mbele ya kiongozi huyo alisema kuwa dhamira ya ROA ni kubuni, kupanga na kutekeleza mipango inayolenga kuwafikia, kuwasaidia, kuwaokoa na kuwaendeleza watu walio katika hatari ya kuathirika/kuathiriwa na umaskini na magonjwa kwa kushirikiana na wananchi, Serikali na wadau wengine.
Ngalimanayo
alisema kuwa Katika utekelezaji wa mradi wa matunzo na kinga dhidi ya
VVU/UKIMWI wamewafikia wasichana/wanawake wanaofanya biashara ya ngono 3,201 (Songea
MC – 1670, Songea DC – 0, Mbinga TC – 0, Mbinga DC – 568 na Nyasa DC – 963) kati
ya lengo la kuwafikia walengwa 4,022 ambayo ni sawa na
asilimia 80% ya lengo la mradi.
Pia wamewafikia
wasichana wa rika balehe na wanawake wadogo 8,082 (Songea MC -
1319, Songea DC - 2698, Mbinga TC - 2078, Mbinga DC – 941 na Nyasa DC – 996) kati
ya lengo la mradi la kuwafikia walengwa 9,846 ambayo ni sawa
na asilimia 80%.
Alisema
kuwa wamefanikiwa kuwafikia watu 31,191 kati ya hao
watu 11,458 walipimwa VVU kupitia njia ya huduma ya Mkoba
watu 7,056 walipimwa kupitia njia ya ufuatiliaji wa mnyororo
wa wateja (HIV Index Testing) na watu 12,677 walipimwa kupitia
njia ya Jipime (HIV Self Testing).
Alieleza
zaidi kuwa wamefanikiwa kuwafikia watu 1,168 kati ya lengo la
kuibua visa 771 waliopata changamoto za Ukatili wa Kijinsia na
kuwapatia rufaa kwenda maeneo ya kupata huduma husika. Hii ilikuwa ni sawa
na asilimia 152, pia wamefanikiwa kuwafikia watu 2,531 na
huduma ya Dawa Kinga (PrEP) kati ya lengo la watu 10,417.
Hii ilikuwa ni sawa na asilimia 24.
Aidha
wamefanikiwa kuwaunganisha watu 1,609 wanaoishi na VVU/UKIMWI
kwenye Kliniki ya tiba na matunzo na huduma zingine.

Post a Comment