MJUE REGINA JANE ALIYEKUWA KAHABA LICHA YA KUWA NA HIV

Regina Jane, 25,
kutoka nchini Kenya, ni mwanamke ambaye amepitia milima na mabonde maishani mwake
kama anavyosimulia mwenyewe.
Mama huyo wa watoto
wawili, anasema kuwa alifahamu mambo yake yanapaswa kuwa siri kwa watoto wake
yaani ya maisha yake ya mapenzi kuanzia alipokuwa na umri wa miaka, 14, na
ikawa hivyo, hadi alipojitumbukiza katika kazi haramu ya ukahaba akiwa na miaka
16.
Bila shaka sio
simulizi yenye kuleta tabasamu lakini anachosisitiza ni kwamba dunia imekuwa
somo kwake, hasa kupitia aina ya maisha aliyochagua kuishi hapo awali.
Maisha ya utotoni

Regina Jane
alizaliwa na virusi vinavyosababisha maambukizi ya ukimwi - HIV
Regina alizaliwa
miaka 25 iliyopita, na anakiri kuwa alizaliwa na virusi vinavyosababisha
maambukizi ya ukimwi - HIV, ila alifahamaishwa hayo baada ya kifo cha mama yake
akiwa na umri wa miaka minane.
"Nilizaliwa
katika jamii iliyokuwa na mzazi mmoja pekee, ambaye ni mama yangu. Sijawahi
kumuona baba yangu hadi wa leo. Nikiwa mdogo nakumbuka mara nyingi nililelewa
na bibi na babu yangu kwani mama yangu mzazi alikuwa anafanya kazi mbali na nyumbani
kwetu", Regina anasema.
Aidha, anakumbuka
akimuona mama yake akiwa anaugua mara kwa mara ila kutokana na umri mdogo
aliokuwa nao, hakuelewa mengi kuhusu ugonjwa uliokuwa umemsibu mama yake.
Kwa hiyo mama yake
alipofariki alibaki mikononi mwa babu na bibi yake.
Punde baada ya mama
yake kufariki, Regina naye pia akaanza kuwa mgonjwa kila wakati kiasi cha yeye
kulazwa hospitalini kwa muda mrefu.
'Wanaume hawaamini
kwamba nina virusi vya HIV'
'Najuta kumuacha
dada yangu awe na mazoea na mume wangu’
Lakini wakati
wataalam walipokuwa wanamfanyia vipimo mbalimbali hospitalini, aligundulika
kuwa na virusi vya HIV akiwa na umri mdogo na ikawa vigumu kwake kuelezwa
kipindi kile kilichokuwa kina mtatiza au hata kuelewa kuwa na virusi hivyo
ilimaanisha nini ama kuwa na athari zipi katika maisha yake.
Baada ya hali yake
ya afya kugunduliwa, alianza kumeza dawa za kumsaidia kuimarisha kinga mwilini
- ARVs. Wakati alipokuwa anaanza kumeza dawa hizo, hakuelewa ni kwasababu ipi
anatakiwa kuzinywa kila siku, na alipomuuliza bibi au babu yake hakuna aliyempa
jibu kamili.
Hadi kufikia wakati
huo, anakiri kuwa tukio hilo lilimsumbua akili na kumuacha na maswali mengi.
Ilikuwa ada kwa babu kuhakikisha anameza tembe zake mbili tena kwa wakati, ila
hakuna aliyekuwa tayari kumuelezea dawa hizo ni za nini.
"Nikiwa na
miaka 12, kuelekea 13 hapo, nilikuwa nimeanza kukomaa na kuelewa mambo
mbalimbali. Na pia wakati huo nilikuwa ninajipeleka mwenyewe kliniki kuchukua
dawa zangu za mwezi mzima. Siku moja nikapata ujasiri na kumuuliza daktari ni
kwanini mimi humeza dawa kila siku? Alinijibu kwa kunielezea hali yangu ya HIV,
na kuniambia kuwa sina budi kumeza dawa hizo katika kipindi chote cha maisha
yangu", Regina anakumbuka.
Mama huyo anasema
kuwa nyumbani alitafuta sana majibu aliyopewa siku ile na daktari lakini kwa
kuwa mama yake alifariki kutokana na ugonjwa wa ukimwi, ilisalia kuwa siri
kubwa iliyolindwa kama dhahabu katika boma lile na ukweli wa kwamba mama yake
alikuwa amemwambukiza Regina virusi hivyo akiwa bado mtoto mchanga, hilo nalo
likawa mwiko kuzungumziwa ama na babu au bibi yake.
Regina anasema ni
hali aliyoikubali japo shingo upande, wakati huo alitamani sana kama maneno
aliyoarifiwa hospitalini yangetoka kwa wapendwa wake, ila haikuwa hivyo.
Alipofikisha miaka 14 alikuwa ameanza kubaleghe, na hapo ndipo alipoanza urafiki japo kwake yeye ulikuwa urafiki wa kawaida tu na mwanamume mtu mzima. Urafiki huo uliendelea kwa muda na kubadilisha kabisa mkondo wa maisha yake.

"Nikiwa darasa
la saba nilikuwa nimeanza kuhudhuria warsha zilizokuwa zinahusu wanarika na
watoto waliokuwa wamezaliwa na virusi vya HIV. Nilikuwa ninasafiri umbali mrefu
kiasi kuhudhuria shughuli hizo na hapo ndipi nilipokutana na mwanamume mmoja
ndani ya gari la usafiri wa umma, aliyeanza kuonyesha hisia za mtu mkarimu.
Sikuwa na wasiwasi naye kabisa licha ya kwamba ilikuwa ni mara yangu ya kwanza
kukutana naye. Alisisitiza kwamba angenitembelea kwetu kesho yake," Regina
anasema.
Regina Jane
alibakwa na mtu ambaye alikuwa amemuamini
Ziara ya mwanaume
huyo kumuona Regina, iliishia kwa kitendo cha kunajisiwa kichakani na hiyo
ikawa mara yake ya mwisho kumtia machoni.
Kilichofuata,
Regina alibainika kuwa mjamzito. Wakati huo, alikuwa bado ni mwanafunzi wa
shule ya msingi. Kibaya zaidi, ukawa ndio mwisho wa safari yake ya kutafuta
elimu na kulazimika kukumbatia majukumu yakuwa mlezi.
Na hadi anaanza
utekelezaji wa jukumu la kuwa mama baada ya kupata mtoto wa kiume, Regina
alikuwa anakabiliwa na unyanyapaa, chanzo cha hilo ikiwa ni kukosa kumnyonyesha
mtoto wake. Baadhi ya kina mama wenzake walianza kumsema na kumsimanga.
Muda si muda,
taarifa hizo zikawa gumzo mtaani, jambo lililomuathiri mno kisaikolojia kiasi
cha hata kufanya uamuzi wa kukosa kumeza tembe zake kwa kipindi cha miezi
minane.
Ndani ya miezi
hiyo, akawa yuko mbioni kujaribu kutumia kila njia kubadilisha uhalisia wa hali
yake ya kuwa mwathirika wa virusi vya HIV mbele ya watu.
'Nilidhani kuwa
nikiombewa nitapona'
Kwa sababu ya
changamoto alizokuwa anakumbana nazo kipindi kile, Regina aliamua kuwa muumini
wa dhehebu moja, na kuamini kwamba maombi maalum aliyopata katika eneo hilo la
ibada, yangebadilisha hali yake ya afya.
"Nilikuwa
ninaabudu katika eneo moja la ibada, hii ni baada ya kuelezewa kuwa nikiombewa
nitapona. Mimi niliamini hilo kwa asilimia 100, na nilipojipeleka kliniki
kupimwa tena, bado nikapatikana na HIV. Yule mhudumu wa afya alinipa nasaha ya
kwamba licha ya kuwa naendelea kupokea maombi, nisiache kumeza dawa
zangu", anasema Regina.
Hayo yote Regina
anasema yalikuwa mahangaiko ya kujitafutia tiba akiwa na matumaini kwamba
hatimaye atapona kabisa virusi vya HIV.
Regina anakiri kuwa
kuna kipindi maishani mwake alihisi machungu mengi na pia kujiuliza maswali
chungu nzima kuhusu wajibu wa mama yake marehemu katika maisha aliyokuwa
anaishi.
Fikra zilizotokana
na ukweli kwamba aliyemuambukiza alikuwa mama yake mzazi aliyeamua kumnyonyesha
licha ya kufahamu kwamba ana virusi hivyo ilhali alikuwa na kiu sana ya
kumsamehe kwa dhati ya moyo wake hata kama hakuwepo tena duniani.
Majuto ya kuingia
kwenye ukahaba
Baada ya Regina
kujifungua alifahamu fika kuwa hangeendelea kuishi na babu yake na kuamua
kuanza kufanya biashara mbalimbali kama njia ya kijitafutia riziki aweze
kujikimu kimaisha.
Akiwa bado
anajitafuta, baadhi ya rafiki zake wa kike aliokuwa anatembea nao walimshawishi
kuingia katika biashara ya ukahaba.
''Nilisafiri kutoka
kwetu Lamu hadi Mombasa. Nikiwa kule nilikutana na mwanadada mmoja
aliyenikaribisha kwenye kazi ya ukahaba. Sababu kubwa iliyopelekea mimi
kukubali kazi hii, ni kutokana na kuwa nilijiona kama mwanamke aliyefeli
maishani. Nilikuwa na umri mdogo wa miaka 16 na kuamini kwamba ingekuwa vyema
ikiwa nitachagua njia ya mkato kujikimu kwa kuuza mwili wangu", Regina
anasema.
Na bila kufikiria
mara mbili, Regina akajitosa kwenye biashara haramu ya ukahaba. Kila usiku hata
wakati mwingine mchana, alijipeleka katika mitaa mbalimbali kusaka wateja.
"Sio kwamba
biashara ya ukahaba ni kazi yenye tija. Niligundua kuwa wanawake wengi wakiwa
makahaba huwa wanadharauliwa mno kwani kuna wakati mwingine ningekutana na
wateja ambao wanalipa kunitumia tu, na baada ya hapo wanakuona kama chombo chao",
Regina anakumbuka.
Kazi ya ukahaba na
HIV
Je biashara ya
ukahaba ilikuwaje ilihali alikuwa anajuwa kwamba ana virusi vya HIV?
Regina anasema
kwamba alikuwa akiwaeleza ukweli baadhi ya wateja wake ila wengi ni wale ambao
hawakumsikiliza ama walikuwa wakaidi wa kuwajibikia hali yao ya kiafya.
Mama huyo anasema
katika biashara ya ukahaba, idadi kubwa ya wateja aliotoka nao, hawakuwa
wanatumia mipira ya kondomu hata baada ya kuwatahadharisha mara kwa mara.
"Nilikuwa
ninaamini ya kuwa ni wajibu wa kila mtu mzima kujijali, na wakati wanaamua
kushiriki ngono na makahaba wajikinge".
Regina anasema
safari yake hii ilikuwa na panda shuka za aina yake na hata kama ilimpa riziki
kwa zaidi ya miaka minne, hasara ni nyingi sana kuliko hata mapato aliokuwa
anapata.
Bado anakumbuka
majina aliyopewa wakati anaendeleza kazi hiyo, hatua iliyozidisha unyanyapaa
hata zaidi kwa watu wanaoishi na HIV.
Kwa mfano, Regina
anasimulia kilichotokea siku moja akidai kuwa hawezi kuisahau maishani mwake.
"Nilikuwa
nimempata mteja mmoja ambaye nilikwenda naye kwenye vyumba tulivyokuwa
tunavikodisha. Baada ya muda wake kumalizika, alinilipa na nikaanza
kujitayarisha kuondoka sehemu ile, ila aliniamrisha nirejee tena. Nikamueleza
kwamba atatakiwa kunilipa tena. Lakini cha kushangaza ni kuwa papo hapo alianza
kunizaba makofi huku akinichania nguo zangu. Hakuna hata mtu mmoja aliyeingilia
kati kunisaidia. Ilibidi nichukue nguo mmoja iliyokuwa imeanikwa kwenye kamba
ili nijisitiri", Regina anasema.
Kuanzia kipindi
hicho, Regina alianza kufikiria na kujutia hatari iliyokuwa inamkodolea macho,
vilevile hatari ambayo alikuwa anajiwekea kutokana na kuwa kahaba anayeishi na
virusi vya HIV.
Ila kila alipowaza
kuiwacha ile kazi ya ukahaba, alijikuta akijiuliza maswali mengi kuhusu namna
atakavyoweza kusukuma gurudumu la maisha pamoja na familia yake.
Pia anasema kuwa
ukahaba unahitaji ujasiri ambao sio wa kawaida kwa hiyo wakati mwingi aliishia
kunywa pombe pamoja na kuvuta bangi nyingi kuliko kawaida.
Kumaanisha kuwa
kila wakati alipokuwa kazini ni lazima angekuwa mlevi. Hilo ni moja wapo ya
yale yaliyomkosesha usingizi na baada ya kujitathmini tena, ikawa moja ya kilichochea
kuachana na ukahaba.
Na ili kufanikiwa
kuanza safari mpya ya maisha na kuupiga teke ukahaba, Regina aliamua kufanya
maamuzi ambayo hayakuwa rahisi kwake, kuondoka mji wa Mombasa na kuhamia mji
mkuu nchini Kenya, Nairobi.
Na hapo ndipo
alipoamua kuwa mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu na pia kutoa mafunzo
maalum kwa umma na hasa kwa watu wanaoishi na virusi vya HIV.
Chanzo BBC

Post a Comment