MAHAKAMA YAAMURU MGOMBEA BINAFSI TANZANIA
Baada ya Mahakama ya Rufani mwaka 2009 kutengua uamuzi wa
Mahakama Kuu uliotamka kuwa wagombea binafsi wana haki ya kushiriki uchaguzi
nchini, mtetezi mkuu wa haki hiyo, mwanasiasa machachari, Christopher Mtikila
hakukata tamaa.
Mwaka 2011, Mtikila alishirikiana na Kituo cha Sheria na Haki
za Binadamu (LHRC), kutetea wagombea binafsi katika Mahakama ya Afrika ya Haki
za Binadamu na Watu (AfCHPR).
Katika Mahakama hiyo yenye makao yake makuu Arusha, waombaji
hao walitaka itoe tamko kuwa Serikali ilikiuka Ibara ya 2 na ya 13 (1) ya
Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu (African Charter on Human and
People’s Rights) kwa kufanya marekebisho ya Katiba yaliyozuia wagombea binafsi.
Pia, waliitaka itoe amri ya kuitaka Serikali ichukue hatua za
kikatiba na kisheria kuhakikisha haki za binadamu zilizo chini ya Ibara ya 2 na
ya 13 (1) ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu na zile za 3 na 25
za Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kisiasa na Kiraia (ICCPR) zinatekelezwa
Pia, waliiomba Mahakama hiyo iiamrishe Serikali kutoa taarifa
mahakamani hapo ndani ya miezi 12 tangu siku ya hukumu kuhusu utekelezaji wa
hukumu hiyo
Kwa mujibu wa Mtikila, Katiba ya Tanzania ilikiuka haki yake
ya kuungana na wenzake kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi kwa kuzuia
wagombea binafsi kugombea urais, ubunge na nafasi za Serikali za mitaa.
Alidai kuwa kitendo cha Serikali kuanzisha mchakato wa
mabadiliko ya Katiba na hatimaye kuzuia watu binafsi kugombea urais, ubunge na
Serikali za mtaa wakati kukiwa na kesi mahakamani inayosubiri kuamuliwa kuhusu
suala hilo, kulikiuka misingi ya utawala bora.
Mtikila alidai kuwa kitendo cha Serikali kilikiuka haki zake
chini ya Ibara ya 2, 10 na 13(1) ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na
Watu, Ibara za 22, 25 na 26 za mkataba wa ICCPR na Ibara za 1, 7, 20 na 21(1)
za Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu.
Mchungaji Mtikila aliitaka Mahakama hiyo ya Afrika itoe tamko
kuwa sheria inayozuia wagombea binafsi kugombea katika uchaguzi wa kisiasa
ilikuwa inapingana na mkataba wa ICCPR.
Kabla ya kuanza kwa usikilizwaji wa kesi hiyo, Serikali
iliweka mapingamizi ya awali kuhusu uhalali wa kupokewa kwa kesi ya Mtikila na
mamlaka ya Mahakama hiyo ya Afrika kusikiliza shauri hilo.
Katika pingamizi la kwanza, Serikali ilidai kuwa Ibara ya 62
(2) Itifaki ya AfCHPR inaweka sharti kuwa ili Mahakama hiyo iweze kusikiliza
maombi yaliyo mbele yake, mleta maombi alipaswa kutumia njia zote ndani ya nchi
yake kabla ya kwenda huko.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) alidai kuwa Mtikila na LHRC
hawakufanya hivyo kwa sababu uamuzi wa mwisho wa Mahakama ya Rufani ulitamka
kuwa suala hilo ni la kisiasa, hivyo lilitakiwa limalizwe na Bunge. Alidai kuwa
njia ya Bunge kumaliza suala hilo bado ilikuwa haijatumika.
Katika pingamizi lingine, AG alidai kulikuwa na
ucheleweshwaji usio na sababu kufungua maombi katika Mahakama ya Afrika.
Pia, alidai waleta maombi walichukua muda mrefu kufungua
maombi yao.
Wakati Mahakama ya Rufani ikitoa uamuzi wake Juni 17, 2010,
waleta maombi walisubiri hadi Juni 2011 kufungua maombi yao.
Pingamizi lingile lililoletwa na Serikali ni kwamba Mahakama
hiyo haikuwa na mamlaka ya kusikiliza shauri hilo, ikidai wakati unaodaiwa
ukiukwaji huo wa haki za binadamu ukitokea, itifaki hiyo ya kuanzishwa kwa
Mahakama ya AfCPHR ilikuwa haijaanza kufanya kazi.
Mwisho wa siku, Mahakama hiyo iliyatupilia mbali mapingamizi
yote ya Serikali kwa kutokuwa na msingi na kuendelea kusikiliza kesi hiyo.
Katika hukumu yake ya Julai, 2013, Mahakama ya AfCPHR
ilikubaliana na hoja za Mtikila na LHRC kuwa Tanzania ilikiuka haki za raia
kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi yao moja kwa moja au kupitia
wawakilishi kwa kulazimisha raia kuwa wanachama wa vyama vya siasi ili wapate
kibali cha kugombea urais, ubunge na Serikali za mitaa.
Mahakama hiyo ya AfCPHR ikaiamuru Tanzania kuchukua hatua za
kikatiba na kisheria ‘kutibu’ ukiukwaji huo wa Katiba.
Mahakama hiyo ya Afrika ilikubali hoja kuwa mkataba wa ICCPR
ulilinda haki na uhuru wa kila raia kushiriki bila kuingiliwa katika shughuli
za utawala wa nchi, moja kwa moja au kupitia wawakilishi.
Kwa maoni yake, haki hiyo haikumaanishwa ifurahiwe tu na wale
walio ndani ya makundi kama vyama vya siasa.
Mahakama ya AfCPHR iliona kitendo cha kuwataka watu kuwa
sehemu ya vyama vya siasa au kuteuliwa na vyama vya siasa wanapotaka
kuchaguliwa kilikiuka haki zao kujumuika na wengine.
Zaidi ya hapo, mahakama hiyo ya AfCPHR ilisema kwa kufanya
mabadiliko ya Katiba yaliyolenga kuzuia wagombea binafsi kugombea nafasi
mbalimbali za uongozi, Tanzania ilikiuka wajibu wake chini ya Ibara ya 2 ya
Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu na pia Ibara ya 3 (2) ya mkataba
huo.
Ibara hizo zinatambua kuwa kila mtu ana haki ya uhuru na
kulindwa bila kubaguliwa kwa namna yoyote, ikiwamo upande wa siasa anaouamini.
Kuhusu hoja ya Mtikila kuwa Tanzania ilikiuka misingi ya
utawala bora kwa kupitisha mabadiliko ya katiba yaliyofuta wagombea binafsi ili
kukwepa madhara ya uamuzi wa Mahakama Kuu iliyotamka kuwa mabadiliko hayo
yalikuwa kinyume cha katiba, Mahakama ya Afrika ilisema kuwa dhana ya utawala
bora si dhana ya jumla na isingeweza kujibu hoja ya waleta maombi kwa sababu
hawakueleza ukiukwaji wake kuhusiana na haki fulani.
Mahakama hiyo ya AfCPHR ikaielekeza Tanzania kuchukua hatua
za kikatiba, kisheria na hatua nyingine zote muhimu ndani ya muda stahiki
‘kutibu’ ukiukwaji wa haki za binadamu kama ilivyoziainisha na iijulishe
Mahakama hiyo hatua zilizochukuliwa.
Source: Mwananchi

Post a Comment