DKT. SENGATI AAHIDI KUPAMBANA NA CHANGAMOTO YA UMASIKINI SHINYANGA

Na Anthony Ishengoma- Shinyanga.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati
amesema mkoa huo una utajiri wa rasilimali lakini hali ya maisha ya wananchi wake
haiendani na hali halisi, akiitaja kuwa ndiyo changamoto kubwa.
Dkt. Sengati amesema hayo leo wakati wa kumkaribisha Katibu
Tawala Mpya wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Batlida Buriani ambaye kwa mara ya kwanza
amefika katika ofisi yake mpya tayari kwa makabidhiano na kuendelea majukumu
yake mapya.
Dkt. Sengati aliongeza kuwa Shinyanga kuna umasikini
ambao umejificha katika utajiri mkubwa lakini hususani kwa wakazi wa pembezoni
akiahidi kuifanyia kazi changamoto hiyo ili wakazi wake waweze kuinua hali yao
itakayoendana na rasirimali zilizopo.
‘’Unakuta mtu ana ng'ombe zaidi ya elfu moja lakini
mtu huyo anaishi katika mazingira yaliyo duni sana au haoni faida ya kupeleka
mtoto katika elimu ya juu hii changamoto ambayo lazima tuifanyie kazi,”
alisisitiza bosi huyo wa mkoa.
Naye Katibu Tawala Dkt. Batlida Buriani amesema kuwa lazima kuwe
na ubunifu katika kutafuta vyanzo vipya vya mapato na kuzitaka Halmashauri za
Mkoa wa Shinyanga kukusanya mapato bila ya kuleta kero kwa wananchi.
Aidha Dkt. Buriani amesema pia ipo haja ya kuingalia
upya mianya yote ambayo imekuwa ikichangia upoteaji wa mapato kwa lengo la
kuinua na kukuza uchumi wa mkoa wa Shinyanga.
Pamoja na mambo mengine Dkt. Buriani amesema
ataliangazia pia suala la maendeleo na ustawi wa jamii kwa kuhakikisha ipo
miradi ambayo inaweze kuingiza kipato kwa wazee na wanawake ili nao waweze
kuchangia katika kujiletea maendeleo lakini pia kuchangia katika maendeleo ya
Taifa.
‘’Najua Shinyanga kuna wazee wengi sana na hali zao
sio nzuri na katika jambo ambalo ninataka tufanikiwe ni kuhakikisha wanashiriki
katika miradi ambayo itawanufaisha najua kuwa Shinyanga kuna mifugo mingi hivyo
tunaweza tukatumia fursa ya mifugo iliyopo kuzalisha siagi kwa wingi
sana," alisema.
Naye aliyekuwa Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Bw. Albert
Msovera alisema bado kuna changamoto ya watumishi lakini zipo juhudi ambazo
zimekuwa zikiendelea kuhakikisha changamoto hiyo inatatuliwa na hivyo kumtaka
mrithi wake kuangalia namna bora ya kuendelea kulifanyia kazi jambo hilo ili
kukabiliana na upungufu wa rasilimali watu.

Post a Comment