ZIJUE ZINACHOJIVUNIA KLABU KONGWE ZA SOKA BONGO


SHEIKH ABEID AMANI KARUME: Mwanapinduzi aliyeibukia kwenye ubaharia |  FikraPevu


1. Young Africans Sports Club 'WANANCHI'

Ilianzishwa rasmi siku ya Ijumaa tarehe 11 February 1935. 

Awali ilijulikana kama Italiana , New Young  kabla ya hiyo Februari 11 1935 kujiita Dar es Salaam Young Africans au Yanga kwa matamshi ya Kiswahili. 

Walianza kutumia jezi za bluu ambapo pia wakijulikana kama The Navigators, ikiundwa na wajanja wazawa waliokuwa mabaharia enzi hizo, wenyeji wa mitaa ya Jangwani, jijini Dar es Salaam.

Jezi zao za sasa ambazo ni rasmi za Njano, Kijani na Nyeusi walianza kuzitumia mwaka 1948.

Ndani ya uwanja, Yanga wana rekodi kadhaa ambazo ni pamoja na kufika robo fainali Klabu bingwa Afrika zamani ikiitwa African Cup of Champions Clubs mwaka 1969 na 1970 . Pia mwaka 1998 waliishia hatua ya makundi.

Katika Michuano ya Kagame Cup, ambalo linashirikisha timu bingwa kutoka nchi za Afrika Mashariki na Kati, inayoratibiwa na Baraza la Michezo la eneo hilo, CECAFA, Yanga imelitwaa mara tano.

Katika Michuano ya Kombe la Washindi Barani Afrika enzi hizo, ambalo sasa linajulikana kama Michuano ya Shirikisho, Yanga imefika hatua ya makundi mara mbili, 2016 na 2018 na mwaka 1995, walifika hatua ya robo fainali.

Katika Michuano ya Ligi Kuu Tanzania, ndiyo timu iliyobeba mataji mengi zaidi, ikiwa ndiyo chanzo cha kuitwa mabingwa wa kihistoria, wakiwa wameweka kabatini kwao mataji 27, huku wapinzani wao wa jadi, Simba ikiwa na mataji 22 tu.

Katika michuano ya Kombe la Tusker, imetwaa mataji mawili, mwaka 2007 na 2009.

Makao makuu ya Jengo lao limejengwa na kampuni ya Mecco na kuzinduliwa rasmi April 1, 1974. Ndiyo klabu ya kwanza Tanzania kuwa na makao makuu yake yakiwa sambamba na uwanja wao ulioitwa Kaunda ambao kwa sasa hautumiki baada ya kukumbukwa na mafuriko ya mara kwa mara ya Mto Msimbazi.

 

2. Simba Sports Club 'WEKUNDU WA MSIMBAZI' 

Mwaka mmoja baada ya kuzaliwa Yanga SC nchini Tanzania (Tanganyika ), mwishoni mwa mwaka 1935 kuliibuka ugomvi mkubwa ndani ya klabu hiyo ya Jangwani, hususani katika mfumo wa uendeshaji na umiliki wake ambao ulisababisha baadhi ya watu kujiondoa na kwenda kuanzisha klabu yao. 

Ugomvi huo ulichochewa sana na Serikali ya kikoloni enzi hizo katika kuvunja umoja wa Watanganyika kupitia michezo. Wakiitekeleza vema ile dhana ya DIVIDE AND RULE yaani wagawe ili uwatawale vizuri. 

Hii ilipelekea kuibuka kwa Queens SC ambao ndiyo hasa chimbuko la Simba SC, hiyo ikiwa ni tarehe 17 March 1936, ambao ni muda wa kama mwaka mmoja na miezi miwili baada ya kuanzishwa kwa Yanga. 

Jina hilo halikuwavutia wengi kutokana na mikogo kwa wapinzani wao, Dar es Salaam Young Africans hivyo mwaka 1942 walibadilisha jina lao na kujiita The Eagles .

Walijiita The Eagles mwaka huo wakiwa daraja la pili sambamba na Yanga SC na klabu zingine. 

Eagles walikuwa vyema katika vifaa na jezi mbalimbali, wakitumia jezi nyeusi zenye michirizi miyekundu huku jezi nyeupe ikiwa ni jezi yao mbadala. 

Mwaka 1965 baada ya kuanzishwa rasmi ligi daraja la kwanza ambalo lilikuwa likishirikisha timu za bara na visiwani baada ya Muungano wa mwaka 1964, Eagles walibadili jina na kujiita Sunderland. 

Mwaka 1968 hayati Abeid Amani Karume, rais wa kwanza wa Zanzibar, alionesha mapenzi makubwa katika soka nchini, baada ya kutoa ufadhili kwa klabu za Bara na Visiwani.

Ikumbukwe kwa nyakati tofauti aliziwezesha African Sports ya Zanzibar, Mlandege, African Sports ya Tanga na Yanga SC kujiinua kiuchumia, kama alivyofanya  pia kwa Sunderland.

Miaka miwili baadaye, yaani mwaka 1970 alitoa wazo la klabu zenye majina ya kizungu kubadili majina yao, akipendekeza Sunderland kuitwa Simba wa Afrika ). Ni Agosti 8, 1972 ndipo Sunderland ikafa rasmi na kuanza kutumika kwa jina la SIMBA SPORTS CLUB.

Katika historia ya Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo zamani ilijulikana kama ligi daraja la kwanza, Simba ndiyo ilikua klabu ya kwanza kutwaa taji hilo, ikifanya hivyo mwaka 1965. Lakini wameweza kuchukua kombe hilo mara 22 tu, nyuma ya Yanga SC walioweza kufanya hivyo mara 27.

Ndiyo vinara wa michuano ya Kagame Cup, inayoshirikisha timu kutoka nchi za Afrika Mashariki na Kati, ikiwa imetwaa taji hilo mara sita, nyingi kuliko timu nyingine yoyote.

Ndiyo klabu pekee kutoka Tanzania kuwahi kucheza fainali za michuano ya Afrika, ikifanya hivyo mwaka 1993, ilipokosa kombe mbele ya Stella Abdjan ya Ivory Coast, ambalo sasa linaitwa Kombe la Shirikisho.

Katika michuano ya kombe la Tusker, timu hiyo wamelichukua mara nne, miaka ya 2001, 2002 , 2003 na 2005.

Wana rekodi ya kufika hatua ya robo fainali klabu bingwa Afrika mara tatu, mwaka 1994, 2018-19 na mwaka huu. Ina nafasi ya kuwa klabu ya kwanza Tanzania kuandika rekodi ya kufika nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika endapo itaitoa Kaizer Chiefs inayokutana nayo katika hatua ya robo fainali.

3. African Sports Club 'WANA KIMANUMANU' 

Hawa ni watoto wa jijini Tanga walioanzisha timu yao Julai 12, 1936 miezi michache baada ya kuanzishwa Simba SC jijini Dar es Salaam.

Africans Sports ni matokeo ya mapinduzi ya kukua kwa mwamko wa soka Tanganyika yaliyoanzia jijini Dar es Salaam baada ya kuzaliwa Yanga na Queens (Simba SC).

Wazee wa Tanga waliamua nao kuanzisha timu yao ili kupata nafasi ya kushiriki michuano ya ligi ya Pwani iliyotawaliwa sana na timu za Dar es Salaam.

Hawa walikuwa na undugu na Yanga ya jijini Dar es Salaam pia African Sports ya Zanzibar. Walitumia jezi zilizofanana.

Ndani ya uwanja, hawa ni mabingwa wa Ligi Kuu ya Muungano mwaka 1988, wakiwa wameanza kucheza ligi ya daraja la kwanza mwaka 1965 na kushuka mwaka  1991 kabla ya kurejea tena mwaka 2015 baada ya kupita miaka 23 lakini kwa sasa imeshuka tena daraja.

Historia yao inaanzia mwaka 1932 barabara ya 12 jijini Tanga . Hapo ndipo walipoanza kuisuka timu yao kabla ya mwaka 1936 kupata leseni ya kuwa klabu rasmi ya mpira na michezo mingine.

4. Coastal Union 'WAGOSI WA KAYA' 

Wagosi wa Kaya, walianzishwa rasmi mwaka 1948 wakitokea ubavuni mwa African Sports kama ilivyo kwa Simba SC na Yanga SC . 

Hawa ni mabingwa wa Nyerere Cup mwaka 1980 na 1988.

Mabingwa wa Ligi kuu Tanzania Bara mwaka 1988 wakashindwa kutetea kombe hilo mwaka 1989 ambapo lilikwenda kwa Malindi ya Zanzibar. (Wakati huo kukiwa na Ligi Kuu ya Muungano)

Ni wapinzani wa Jadi wa African Sports huku wakiwa na undugu wa miongo kadhaa na Simba SC hali inayowafanya kuwa pia na upinzani na Yanga SC ambao wana undugu na African Sports.

Mwaka 1981 walijitoa Ushiriki wao klabu bingwa Afrika lakini waliweza kushiriki mwaka 1989 na kuondolewa hatua za awali. Walijitoa mwaka 1981 kutokana na Ukata.

Credit kwa Samuel Samuel wa Futbal Planet FB

 

No comments