IJUE HISTORIA YA MGOGORO WA ISRAEL NA PALESTINA

Mgogoro upo toka
enzi za manabii Ibrahim, Isaka, Ismail na Yakobo
Na Masudi Rugombana
Taifa hili
linapatikana Mashariki ya bahari ya Mediterrania, ni taifa dogo kwa eneo,
likiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 20,770. ( Imezidiwa ukubwa wa eneo na
Wilaya ya Sikonge nchini Tanzania kwa tofauti ya kilomita za Mraba 7103 ).
Israel inapakana na
nchi za Syria na Lebanon kwa upande wa Kaskazini, Jordan na eneo la Palestina
la Ukingo wa Magharibi (West bank) kwa upande wa Mashariki na kusini inapakana
na Misri na eneo la Palestina la Ukanda wa Gaza ( Gaza strip ).Taifa hili lina
idadi ya watu Milion 8,680,000 kwa takwimu za mwaka 2017.
Idadi ya Wayahudi
ni Milioni 6,484,000 sawa na 74.7% (Idadi hii inajumuisha Walowezi wa Kiyahudi
wanaoishi ukingo wa Magharibi (West bank) na eneo la Milima ya Golan). Waisrael
Waarabu ni Milioni 1,808,000 sawa
na 20.8% ya raia wote wa Israel. Idadi
ya Wakristo ambao sio Waarabu pamoja na watu wa jamii ya bahai ni 388,000 sawa
na 4.5% ya raia wote wa Israel. Lugha rasmi za Taifa la Israel ni Kiebrania
(Hebrew) na Kiarabu (Arabic).
Wapalestina ni
jamii ya Kiarabu inayopatikana kwa wingi katika ardhi yao inayokaliwa kimabavu
na Israel, kwenye ukingo wa Magharibi wa mto Jordan (West bank) na eneo la
Ukanda wa Gaza lililowekewa mzingiro na Taifa la Israel. (Besieged Gaza strip).
Idadi ya watu wanaoishi
katika ardhi ya Palestina ni milioni 4,543,126 kwa takwimu za mwaka 2017 ambapo
Wapalestina ni 3,950,926 na Walowezi wa kiyahudi wanaunda idadi ya watu 592,200.
Eneo la Ukingo wa Magharibi (West bank) lina ukubwa wa kilomita za Mraba 5,860
na Idadi ya Watu milioni 2,747,943 kwa takwimu za mwaka 2017. Eneo
lililozingirwa la Gaza (Besieged Gaza strip) lina ukubwa wa kilomita za Mraba
360 na idadi ya watu 1,795,183 kwa takwimu za mwaka 2017. (Ukubwa wa ukanda wa
Gaza umetofautiana kidogo na ukubwa wa Wilaya ya Ilala inayopatikana mkoa wa
Dar es salaam nchini Tanzania kwa kilomita tano za mraba). Lugha rasmi za
Wapalestina ni Kiarabu (Arabic) na Kiebrania(Hebrew).
UZAYUNI (ZIONISM)
NA KUTAWANYIKA KWA WAYAHUDI.
Uzayuni (Zionism)
ni Itikadi ya taifa la Israel. Mazayuni (Zionists) wanaamini kuwa Uyahudi
(Judaism) ni utaifa na pia ni dini. Na kwamba Wayahudi wanastahili kuwa na nchi
yao katika ardhi ya mababu zao kama ambavyo Wachina wanavyostahili kuishi China
au Wahindi wanavyostahili kuishi India. Itikadi hii ndiyo iliyosababisha
Wayahudi kuanza harakati za kurudi tena katika ardhi ya Palestina na kuunda
taifa la Israel mnamo mwaka 1948. Na hiki ndicho chanzo cha mgogoro wa sasa
kati ya Wapalestina na Waisrael.
Waisrael
wanapozungumzia Historia ya utaifa wao, huanzia kwenye ufalme wa Daudi (David)
ambaye ndiye muasisi wa Ufalme wa Israel uliojulikana kama United Monarch mnamo
mwaka 1004- 960BC. Baada ya kifo cha Daudi, mwanaye Suleiman (Solomon) alishika
hatamu ya uongozi kuanzia mwaka 961-922BC. Baada ya kifo cha mfalme Suleiman
mwaka 922BC Makabila kumi ya upande wa
Kaskazini yalikataa kuwa chini ya Utawala wa mfalme Rehoboam ambaye alikuwa ni
mtoto wa Mfalme Suleiman, hivyo makabila haya yalifanya uasi na kuanzisha ufalme
wao walioupa jina la Ufalme wa Israel-Samaria, mji mkuu wa Ufalme huu uliitwa
Samaria, baadae walihamishia makao makuu kwenda mji wa Wacaanan wa Sichem ambao
kwa sasa unajulikana kama Nablus. Ufalme huu ulisambaratika baada ya kuangukia
mikononi mwa dola ya Assyria ( Assyrian Empire) mnamo mwaka 720BC.
Hali hii ilipelekea
kuwepo kwa falme mbili za Kiebrania za upande wa Kaskazini na upande wa kusini
ambayo hii ya upande wa kusini ilibaki kuwa chini ya Mfalme Rehoboam
ilijulikana kama nchi ya Yuda (Judah), makao yake Makuu yalibaki katika mji wa
Jerusalem na baadae yalihamishiwa katika mji wa Hebron. Ufalme huu
ulisambaratika baada ya kushindwa vita na kuangukia mikononi mwa mfalme
Nebuchadnezzar wa Babeli mnamo mwaka 587BC.
Mwaka 63BC nchi ya
Yuda iliwekwa chini ya uangalizi wa dola ya Kirumi na mwaka wa 6CE
iliunganishwa na kuwa jimbo la Warumi. Mnamo kwaka 135CE Wayahudi waliasi na
kupelekea vita baina yao na Warumi ambapo walishindwa vibaya, walipoteza uhuru
wao na mji wa Jerusalem uligeuzwa kuwa mji wa kipagani.Wayahudi walipigwa
marufuku kuishi Jerusalem na Warumi waliibadili jina nchi ya Yuda na kuiita
Syria Palestina.
Kusambaratika kwa
falme hizi mbili za kiyahudi na kutawaliwa na madola makubwa kuanza Assyria
empire, Babylonian empire, Persian Empire (Iran), Greek empire, Roman Empire,
Rashidun Caliphate, Ummayad Caliphate, Ayyubid Dynasty, Mamluk Sultanate,
Ottoman Empire na British Empire (United Kingdom) kulipelekea Wayahudi
kutawanyika katika maeneo mbali mbali Duniani. Kutawanyika huku kuliwagawa
Wayahudi kwa majina kutegemea na maeneo waliyotawanyikia. Makundi haya ya
Wayahudi ni Ashkenazi (Ashkenazi Jews) kundi hili ni lile lililohamia katikati
na Mashariki ya bara la Ulaya. Sephard (Sephardic Jews ) ni kundi lililohamia
maeneo ya kusini ya bara la Ulaya na Kaskazini ya Afrika na Mizrahi (Mizrahi
Jews) ambao walibaki mashariki ya kati, Asia ya Kusini na Asia ya kati.
JE WAYAHUDI
WALIIKUTA ISRAEL IKIWA TUPU BILA WATU?
Ardhi ya Israel
(Palestina) ilikuwa na wenyeji ambao ni makabila ya mwanzo kuja kuweka makazi
yao katika nchi ya Palestina. Makabila haya yalihamia huko kutoka kusini na
Kaskazini mwa Bara Arabu takriban mwaka 3000 BC. Makabila hayo ni Wayebusi (Jebusites), Waamori (Amorites),
Wahiti (Hittites) Wakanaani (Canaanites) na Waperizi(Perizzites). Makabila haya
yalikaa katika maeneo tofauti ya nchi hiyo: Wakanaani waliweka makazi yao
katika eneo la Gaza na Wayebusi walibuni mji wa Yebus, ambao kwa sasa
unajulikana kama mji wa Jerusalem. Wayebusi walipokonywa mji huo na Wayahudi
baada ya kutoka Utumwani nchini Misri mwaka 1003BC chini ya utawala wa mfalme
Daudi ambaye aliufanya kuwa makao makuu ya ufalme wake.
Ibrahim ambaye uzao
wake ndio unaounda jamii ya wana wa Israel alihamia Palestina wakati huo
ikiitwa nchi ya Wacaanan mwaka 1900BC akitokea Kusini mwa Iraq katika eneo
lilijulikana kama Uru ya Wakaldayo (Ur of Chaldeans). Ibrahim aliishi kwa amani na jamii za eneo hilo
ambapo alizaa watoto wawili Ismail na Issaack. Ismail na Mama yake walihama
Canaan na kuweka makazi yao katika mji wa Makka wakati Issack alibaki Caanan na
baba yake Mzee Ibrahim na makazi yao yalikuwa katika mji wa Hebron( Halil).
Issack alimzaa Jacob (Yakubu) ambaye naye alifanikiwa kuzaa Watoto kumi na
mbili.Kutokana na nchi ya Canaan kukumbwa na baa kali la njaa, Jacob ambaye
baadae alibadili jina na kuitwa Israel
na watoto zake walihamia Misri.
Wakiwa Misri
walizaliana kwa wingi na kuishi kama watumwa kwa muda wa miaka mia nne (400)
hadi Mwaka 1190BC waliporudi katika nchi ya Caanan wakiongozwa na Viongozi wao
walioitwa Mussa(Moses) na Joshua Nun (Yusha bin Nuun). Mussa (Mosses) alifariki wakati wakiwa
safarini hivyo Joshua ndiye aliyefanikiwa kuwafikisha katika nchi ya Caanan
ambapo walifanikiwa kuteka maeneo kadhaa baada ya kuingia kwenye mapigano na
wenyeji wao Wacaanan na makabila mengine. Hapo ndipo Joshua alifanikiwa
kuanzisha na kuongoza dola ya Wana wa Israel.
Dola hii haikuweza
kudumu muda mrefu kwani Ilisambaratika baada ya kufa Joshua (Yusha bin Nuun)
hivyo Wana wa Israel waliangukia kwenye mateso ya Wafilisti ambao ni jamii ya
Wacaanan waliokuwa wakielekea upande wa Kaskazini kutokea kwenye miji yao ya
pwani ya kusini ambayo ni Gaza, Ekron, Gath, Ashdod, na Ashkelon. Wana wa
Israel wakiongozwa na Sauli (ambaye kwa kiarabu anatajwa kwa jina la Twaaluti)
walifanikiwa kuwashinda Wafilisti na kuanzisha tena Dola ya Wana wa Israel
mnamo mwaka 1025BC.
Sauli alifariki mwaka 1004BC na hivyo Daudi
alishika uongozi na kuwa mfalme wa Dola ya Israel iliyojulikana kama United
Monarch. Ni katika utawala wa mfalme Daudi (King David) ndipo dola ya Israel
ilipoimarika na kujitanua katika maeneo mengi ikiwa ni pamoja na kuuteka mji wa
Jerusalem kutoka mikononi mwa Wayebusi (Jebusites) mnamo mwaka 1003BC. Mfalme
Daudi alifariki mwaka 960 na mtoto wake Suleiman ( King Solomon) alishika
hatamu ya Uongozi hadi Mwaka 922BC alipofariki. Kufariki kwa Mfalme Suleiman
kulipelekea kugawanyika kwa dola Israel (United Monarch) baada ya makabila kumi
ya upande wa Kaskazini kukataa kuutambua utawala wa mfalme Rehoboamu ambaye
alikuwa mtoto wa Mfalme Suleiman. Hali hii ilipelekea dola hii kuanguka na
kutawaliwa na madola mengine makubwa.
Baada ya kipindi
kirefu cha wastani wa miaka 1360 ya kutawaliwa na Madola mbali mbali makubwa
kama Assyrian empire, Babylonian empire, Persian Empire (Iran), Greek
empire na Roman Empire kilichopelekea
Wayahudi wengi kupelekwa utumwani na wengine kutawanyika sehemu mbalimbali huku
wakiziacha jamii nyingine zikiendelea kubaki katika eneo hilo la Palestine
(Israel) hatimaye Mji wa Jerusalem uliingia mikononi mwa dola ya Kiislam
(Rashidun Caliphate) mwaka 638CE baada ya kuwashinda Warumi wakati dola hiyo ya
Kiislamu ilipokuwa chini ya uongozi wa Caliph Omar Al Khatwab ambaye alifunga
safari kwenda Jerusalem kuchukua funguo za mji kutoka kwa kasisi Sophronius wa
dola ya Kirumi.
Makabidhiano hayo
ya mji wa Jerusalem yalifanyika katika kanisa linajulikana kama the Holy
Sepulchre (Church of the Holy Sepulchre ), katika makabidhiano hayo ya mji wa
Jerusalem, kasisi Sophronius na Caliph Omar Khatwab walisaini mkataba
uliojulikana kama OMAR TREAT, mkataba uliotoa hakikisho kwa Wakristo kuishi na
kufanya ibada zao bila kubughudhiwa. Mkataba huo ulisomeka hivi:
"Haya ndiyo ya
amani aliyowapa Umar kiongozi wa Waislamu watu wa Jerusalem. Amewapa amani kwa
nafsi zao na makanisa yao na misalaba yao, na kuwa hayatakaliwa makanisa yao
wala hayatavunjwa, wala hayatapunguzwa kitu katika majenzi yake wala katika
nafasi yake, wala hawatalazimishwa kuacha dini yao wala kudhuriwa yeyote katika
wao, na ni juu ya watu wa Jerusalem kutoa jizya (tribute) kama wanavyotoa watu
wa Madain"
Ni mwaka huo huo
ambapo miji mingi ya Palestina (Israel)iliingia katika Dola ya Kiislamu.
Ikumbukwe kuwa
Caliph Omar ndiye alijenga msikiti mdogo kwa ajili ya kufanya ibada katika eneo
ambalo Waislamu wanaamini ndipo ulipokuwa Msikiti wa Mbali (Al Aqsa) uliotajwa
kwenye Kitabu kitukufu cha Quran, Sura ya Kumi na Saba (Surat Bani Israil). Kwa
mujibu wa mafundisho ya dini ya kiislam, ni eneo hili ambalo Mtume Muhammad
aliwaongoza manabii katika ibada kabla hajapaa kwenda mbinguni katika kisa
maarufu kinachojulikana kama MIRAJI. Baadae msikiti huo uliongezwa ukubwa hadi
kufikia muonekano wake wa hivi sasa. Na kwa mujibu wa imani ya kiyahudi, katika
eneo hilo ndipo Mfalme Suleiman (King Solomon) alipojenga hekalu la kwanza. Pia
wanaamini kuwa ni katika eneo hilo ndipo patakapojengwa hekalu la tatu na la
mwisho. Eneo hilo ni sehemu takatifu kuliko zote katika imani ya kiyahudi.
MSIKITI WA AL AQSA:
Nchi ya Palestine
pamoja na nchi za Sham zote zilibakia katika utawala wa Kiislamu (Rashidun
Caliphate) kwa muda wa miaka 461. Ni katika kipindi hicho ndipo jamii za eneo
hilo la Palestina zilipojifunza lugha ya kiarabu, kubadili dini na kuingia katika Uislamu.
Dola ya Kiislamu ya
Rashidun ilipokonywa eneo la Palestina (Israel) mwaka 1099CE na Wakristo kutoka
Ulaya walipokuja kuzivamia ardhi hizo katika vita ya Msalaba iliyoshuhudia
mauaji ya Waislamu elfu sabini (70,000) katika eneo la Msikiti wa Aqsa ( Temple
Mount). Watu wa Msalaba (Crusaders) waliikalia ardhi ya Palestina wa muda wa
miaka 88 kabla ya kutimuliwa na Majeshi ya Waislamu wa Ayyubid Dynasty chini ya
Sultan wa Syria na Misri mwenye asili ya Kikurdi Swalaahud-Diyn Hasan
al-Ayyuubiy ambaye aliweza kuirudisha Palestina mikononi mwa Dola ya Kiislamu
mwaka 1187CE. Makao makuu ya dola hii ya kiislamu yalikuwa Cairo nchini Misri kati ya mwaka 1174CE hadi Mwaka
1250CE, baadae makao makuu ya dola hii yalihamishiwa Allepo nchini Syria mnamo
mwaka 1250-1260CE.
Mwaka 1250CE dola
ya Kiislamu ya Mamluk ilikamata hatamu ya kuiongoza Palestina na eneo lote la
Sham (The Levent) kutoka mikononi mwa utawala wa Swalaahudin Al Ayyuubin
(Ayyubid Dynasty). Dola hii ya Mamluk ndiyo iliyopigana na kushinda vita dhidi
ya wapiganaji shupavu wa jeshi la Mongol tarehe 6 Septemba 1260CE pale
walipoivamia na kutaka kuikalia ardhi ya Sham. Ushindi huu wa dola ya Mamluk
dhidi ya Wamongol ulikwenda sambamba na safisha safisha ya mabaki ya Wapiganai
wa Msalaba (Crusaders) waliokuwa wamebakia katika maeneo ya ardhi ya Sham (
Syria, Jordan na Lebanon).
Baada ya dola ya
Mamluki kuishiwa nguvu, hatimaye ardhi ya Palestina na eneo lote la ardhi ya
Sham liliangukia Mikononi mwa dola ya Kiislam ya Ottoman (Ottoman empire)
mwaka 1516CE. Dola ya Ottoman iliitawala
Palestina kwa muda wa miaka 400 hadi ilipoikabidhi mikononi mwa Utawala wa
Uingereza (United Kingdom empire) mwishoni mwa vita kuu ya kwanza ya Dunia
mwaka 1918CE. (Rejea: kitabu cha The Palestinian Issue kilichoandikwa na Dr. Mohsen
M. Saleh)
KUREJEA KWA
WAYAHUDI KATIKA NCHI YA PALESTINA NA KUUNDWA KWA TAIFA LA ISRAEL:-
Kutokana na
manyanyaso, kuteswa na kubaguliwa kwa Wayahudi waliokimbilia barani Ulaya, hali
hii ilipelekea Wayahudi kuanza kufuatilia kwa ukaribu zaidi asili yao. Ni
wakati huo katika karne ya 19 ndipo Wasomi wa kiyahudi walipoona umuhimu wa
kuwa na taifa lao katika ardhi ya asili ya mababu zao. Mwandishi wa Kiyahudi
mzaliwa wa Austria Theodor Herzl alikuwa mtu wa kwanza kupaza sauti kuhusiana
suala la utaifa wa kiyahudi (Jewish nationalism) katika harakati za kimataifa
mnamo mwaka 1896.
Herz ambaye
alishuhudia unyanyasaji mkubwa wa Wayahudi alishawishika kuamini kuwa Wayahudi
hawangeweza kuishi kwa usalama wakiwa nje ya taifa lao. Aliandika Insha
(essays) na kuandaa mikutano iliyochochea uhamiaji mkubwa wa Wayahudi kutoka
Ulaya kwenda katika ardhi ya Palestine (Israel). Kabla ya harakati za Herz, ni
Wayahudi elfu ishirini tu (20,000) waliokuwa wakiishi katika ardhi ya
Palestina. Lakini hadi Adolf Hitler anafanikiwa kukamata madaraka idadi ya
Wayahudi iliongezeka mara nane.
Pia harakati za
Wayahudi kurudi katika ardhi ya Palestina zilichochewa zaidi na azimio la
Balfour (Balfour Declaration) la mwaka 1917, mwishoni mwa vita kuu ya pili ya
Dunia ambapo utawala wa Uingereza kupitia Waziri wake wa mambo ya nje Arthur
James Balfour ulitangaza kuanzisha Taifa la Wayahudi kwenye ardhi ya Palestina
kupitia barua yake aliyoiandika kwenda kwa Lord Rothschild aliyekuwa kiongozi
wa Jumuiya ya Kiyahudi ya Uingereza (British Jewish Community).
Waarabu waliona
kumiminika kwa Wayahudi kama ni harakati za ukoloni kutoka Ulaya. Pande hizo
mbili za Wayahudi na Waarabu ziliingia katika mapigano makali yaliyoshindwa
kudhibitiwa na Utawala wa Uingereza katika Palestina. Mwaka 1947 Umoja wa
Mataifa ulipiga kura kuigawa ardhi ya Palestina kuwa nchi mbili. Wayahudi ambao
idadi yao ilikuwa 650,000 walikubaliana
na uamuzi huo na kutangaza rasmi kuunda Taifa la Israel mnamo 14 May 1948 chini
ya David Ben Gurion ambaye alikuwa Mkurugenzi mkuu wa Shirika la kizayuni
Duniani (World Zionist Organization).
Wapalestina
(Waarabu) ambao idadi yao ilikaribia 1,200,000 waliuchukulia uamuzi huo kama
muendelezo wa mkakati wa muda mrefu wa
Wayahudi kuwaondoa katika ardhi zao, waliukataa mpango huo. Huo ndio ukawa
mwanzo wa Mgogoro wa ardhi unaoendelea sasa baina ya Wapalestina na Waisrael.
Wanamgambo wa Wapalestina wakisadiwa na
mataifa ya kiarabu ya Misri, Jordan, Iraq na Syria walitangaza vita
dhidi ya Israel mnamo tarehe 15 May, 1948.Vita vilimalizika tarehe 10 March
1949 kwa Israel kushinda na kunyakua ardhi zaidi kutoka mikononi mwa
Wapalestina ambao wengi wao waliuawa na zaidi ya laki saba (700,000)
kulazimishwa kuondoka katika ardhi zao hali iliyopelekea waishi katika makambi
ya wakimbizi tatizo ambalo hadi sasa bado halijapata ufumbuzi.
ARDHI YA PALESTINA
INAVYOKALIWA TANGU 1946
Hadi kufikia mwaka
2017 kuna idadi ya wakimbizi milioni saba wa Kipalestina sehemu mbali mbali duniani
ambao Israel imewanyima haki ya kurudi katika maeneo yao. Katika vita hiyo
Israel iliongeza ukubwa wa ardhi kutoka asilimia 55 hadi 77. Wapalestina
walibaki na asilimia 23 tu ya ardhi inayojumuisha eneo la Ukingo wa Magharibi
(West bank) na Ukanda wa Gaza (Gaza Strip). Tukio hili linakumbukwa na
Wapalestina kama Nakba ( Janga) au catastrophe kwa kiingereza na huko Israel
siku ya Nakba husherehekewa kama kumbukumbu ya kuanzishwa kwa Taifa la Israel.
Maeneo ya Ukingo wa
Magharibi na Ukanda wa Gaza yalitekwa na
Israel mwaka 1967 katika vita ya siku sita (Six day war) kati ya Israel
na Mataifa ya Kiarabu ya Misri, Lebanon, Jordan na Syria. Israel iliruhusu
Walowezi wa Kiyahudi kujenga makazi katika maeneo hayo ambapo makazi hayo
yanachuliwa kuwa sio halali na sehemu kubwa ya Jumuiya ya Kimataifa.
Wapalestina
waliendeleza harakati za kujikomboa kwa kuanzisha vyama vya ukombozi vya PLO
(Palestine Liberation Organisation) kilichoanzishwa 28 May 1964 chini ya Yasser
Arafat, sasa hivi PLO inaongozwa na Mahmoud Abbas (Abuu Mazen). Chama kingine
ni HAMAS kilichoanzishwa mwaka 1987 chini ya Ahmed Yasin na Abdel Aziz al
Rantiss, kwa sasa Chama hicho kinaongozwa na Ismail Haniya, waziri mkuu wa
zamani wa Palestina . Chama cha Hamas kimejizatiti zaidi katika eneo la ukanda
wa Gaza wakati chama cha PLO kikiwa na Ushawishi mkubwa katika eneo la ukingo
wa Magharibi wa mto Jordan (West bank).
Kutokana na
kuimarika kwa harakati za Mashambulizi ya Hamas kupitia tawi lao la kijeshi la
Izzudin al Qassam brigades linaloongozwa na makamanda shupavu Mohammed Deif
na Marwan Issa dhidi ya Walowezi wa
Kiyahudi huko Gaza, Israel ililazimika kujiondoa Gaza na kubomoa makazi yote ya
Walowezi wa Kiyahudi. Hatua hiyo iliipa Hamas hatamu ya uongozi katika Ukanda
wa Gaza.
Hata hivyo tangu
Mwaka 2005 Israel kwa kushirikiana na Misri zimeendelea kuiwekea vikwazo Gaza
kwa kuiwekea Mzingiro wenye lengo la kuzuia uingizaji wa silaha na harakati za
wapiganaji wanaoingia na kutoka kwenye eneo hilo. Mzingiro huo umeleta madhara
makubwa kwa wananchi wa Gaza kwa kulifanya eneo hilo kukosa mahitaji mengi
muhimu ya kibinadamu kama mafuta, nishati ya umeme, na uagizaji wa bidhaa za viwandani kutoka nje.
Kujitoa kwa Israel
kutoka ukanda wa Gaza (Unilateral Withdrawal) ilikuwa mwanzo wa taifa hilo la
Kiyahudi kuanza harakati kubwa za ujenzi wa makazi ya Walowezi wa kiyahudi
katika eneo la ukingo wa magharibi (West bank) ukiwemo mji wa Jerusalem
Mashariki ambao Wapalestina wanatarajia kuwa ndio utakaokuwa Mji mkuu wa Taifa
lao. Hadi mwaka huu 2017 idadi ya Walowezi wa Kiyahudi katika eneo hilo
inafikia laki tano (500,000) ambapo Israel imeshasisitiza kuwa Jerusalem kamwe
haitagawanyika na ndio mji wao mkuu wa milele.
Ukiondoa Marekani
ambayo Mwezi Desemba 2017 kupitia Rais Donald Trump imetangaza rasmi kuitambua
Jerusalem kama mji mkuu wa Israel na kuagiza Ofisi za ubalozi wa Marekani
zihamishiwe Mjini Jerusalem kutoka jijini Tel Aviv, bado jumuiya ya Kimataifa
imeendelea kutotambua msimamo huo wa Israel ambapo nchi nyingi zimefungua
balozi zao Mjini Tel Aviv.
Eneo la West bank
lina kumbukumbu Muhimu sana kwa dini za Kiyahudi, Kiislamu na Kikristo kutokana
na kuwa na urithi wa maeneo matakatifu kwa dini hizo kama vile Misikiti ya Al
Aqsa (The dome of the rock) na Haram al sharif (Temple mount) inayopatikana
mjini Jerusalem, pia kuna Church of the Holy Sepulchre. Maeneo mengine ni
Msikiti wa Ibrahim (Cave of the Patriarchs) mjini Hebron na Church of Nativity
mjini Bethlehem ambako ndipo inasemekana alizaliwa Yesu Kristo.
JE WAISRAEL
WATAENDELEA KUIKALIA ARDHI YA PALESTINA MILELE?
Ni swali linalosumbua
sana wanasiasa wa Israel kutokana na wingi wa makazi ya walowezi wa kiyahudi
kwenye ardhi ya Palestina huko ukingo wa Magharibi. Vyama vya siasa vya mrengo wa Kushoto, kati na kulia vimekuwa
na mitazamo na sera tofauti kuhusiana na hatima ya makazi ya Walowezi wa
Kiyahudi katika ardhi ya Palestina.
Misimamo ya vyama
vya mrengo wa kulia:
Chama cha Likud
chenye Wabunge 30 kati ya Wabunge 120
katika bunge la Israel (Kneset) kinachoongozwa na Waziri mkuu Binyamin
Netanyahu, Bayit Yehudi (Jewish Home) chenye wabunge 8 kinachoongozwa na Waziri
wa Uchumi Naftali Bennett, United Torah Judaism chenye Wabunge Sita kinachoongozwa na waziri wa afya Yaakoov
Litzman na SHAS chenye wabunge saba kinachoongozwa na Waziri wa Mambo ya ndani
Aryeh Deri vinapinga kuanzishwa kwa taifa la Palestina. Vyama hivi
vinavyoongoza serikali ya sasa ya Israel vinaunga mkono ujenzi wa makazi ya
Walowezi wa kiyahudi kwenye ardhi ya Palestina.
Msimamo wa vyama
hivi ni kuwa na Taifa moja la Israel lenye wakazi wa jamii za Kiyahudi na
Kiarabu ambao watakuwa na uhuru wa kuishi sehemu yeyote ndani ya Israel.
Kwenye kampeni za
uchaguzi za mwaka 2015 Waziri Mkuu Binyamin Netanyahu akihutubia katika makazi
ya walowezi wa kiyahudi ya Har Homa (Har Homa Settlements) aliahidi kujenga
maelfu ya makazi ya walowezi wa kiyahudi kwenye ardhi ya Palestina na
kusisitiza kuwa hatoruhusu kuundwa kwa Taifa la Palestina katika utawala wake.
Naftari Bennett
mtoto wa wahamiaji wa kiyahudi kutoka Marekani na mwanamama Ayelet Shaked
(Waziri wa Sheria wa Israel) kutoka chama cha Bayit Yehudi ni wanasiasa wenye
misimamo uliyofurutu mipaka wanaotaka Wapalestina wote wachukue uraia wa Israel
na wale wasiotaka basi waishi Israel kwa vibali maalum kama raia wa kigeni au
wakimbizi. Pia wanapinga haki ya kurejea nyumbani kwa wakimbizi wa Kipalestina
waliokimbia wakati wa vita vya mwaka 1948 na 1967.
Chama kingine cha
Mrengo wa kulia cha Yisrael Beiteinu (Israel nyumbani kwetu) chenye wabunge 5,
kinachoongozwa na Waziri wa ulinzi Avigdor Lieberman kinaunga mkono kuundwa kwa
Taifa la Palestina. Chama hicho kupitia mpango wake unaojulikana kama Lieberman
Plan (Populated Area Exchange Plan) kinataka Miji yote ya mipakani ya Israel
yenye wakazi wengi Waarabu kama vile Umm el Fahm, Tayyibe, Ar'ar, Baqa
al-Gharbiyye,Kafri Qara,Qalansawe, Kafr Qasim, Tira, Kafr Bara na Jaljulia
ihamishiwe Palestina kwa kubadilishana na Makazi makubwa ya walowezi wa
kiyahudi yaliyojengwa kwenye ardhi ya Palestina inayopakana na Israel kama vile
Beital Illit, Ma'ale Adumin na Modi'in Illit. Kwa mujibu wa mpango huo Israel
itajiondoa katika makazi mengine machache yaliyojengwa maeneo ya ndani zaidi
kwenye ardhi ya Palestina.
Msimamo wa Vyama
vya mrengo wa kati:
Vyama vyote vya mrengo wa kati vinavyounda
kundi la Zionist Union vya Hatnua chenye Wabunge watano kinachoongozwa na
mwanamama Tzipi Livn, Labor cha Avi Gabbay chenye wabunge 19, Green Movement
cha Yael Cohen ambacho kina mbunge mmoja na Yesh Atid chenye wabunge 11
kinachoongozwa na Mwandishi wa habari Yair Lapid, pia chama cha Kulanu cha
Moshe Kahlon chenye wabunge 10 vinaunga mkono Israel kujiondoa katika maeneo ya
Palestina kupitia mpango wa kuanzishwa kwa mataifa mawili (Two state Solution).
Isipokuwa msimamo wao kuhusu hatima ya mji wa Jerusalem hautofautiani na ule wa
vyama vya mrengo wa kulia ambao unasisitiza kuwa Jerusalem isiyogawanyika ndio
mji mkuu wa milele wa Israel. Pia vyama hivyo vinaunga mkono ujenzi wa ukuta
(Separation wall ) utakaotenganisha eneo la Palestina la West bank na
Israel.Mpango wa kujenga Ukuta ulianzishwa na Waziri mkuu wa zamani hayati
Ariel Sharon lakini haukuweza kukamilishwa hadi sasa.
Msimamo wa vyama
vya mrengo wa kushoto:
Vyama vya mrengo wa kushoto vinavyounda United Arab Joint List vya Hadash
(The Democratic Front for Peace and Equality) chenye wabunge watano
kinachoongozwa na Ayman Odeh, Balad (National democratic assembly) chenye
wabunge watatu kinachoongozwa na Jamal Zahalka, Ta'al (Arab Movement for
Renewal) chenye wabunge wawili kinachoongozwa na Ahmad Tibi, na United Arab
List chenye Wabunge watatu kinachoongozwa na Masud Ghnaim vinapinga ujenzi wa
Makazi la walowezi kwenye ardhi ya Palestina, pia vinataka kuundwa kwa taifa la
Palestina ambalo mji wake mkuu utakuwa Jerusalem Mashariki. Pia msimamo wa
chama cha Wayahudi cha Meretz chenye wabunge watano kinachoongozwa na Zehava Gal-On
hautofautoani sana na Msimamo wa vyama vinavyounda United Arab List.
Kutokana na tofauti
hizo za kimitazamo baina ya vyama vya siasa vyenye nguvu kuhusu namna ya
kutanzua mgogoro wa Palestina na suala la Makazi ya walowezi wa kiyahudi,
uhakika wa walowezi hao kuendelea kuikalia ardhi ya Palestina ni mdogo kwani wakati
wowote wanaweza kuondolewa kutegemea na sera za chama kilichopo madarakani na
makubaliano yatakayofikiwa baina ya Wapalestina na Waisrael.
NINI SULUHISHO LA
KUDUMU LA HUU MGOGORO
Kutokana na sababu
za kihistoria, jamii zote mbili za Wayahudi (Waisrael) na Waarabu (Wapalestina)
zina haki ya kuishi katika eneo hilo na kumiliki ardhi. Kila upande unapaswa
kutambua na kuheshimu haki za upande mwingine. Mgogoro huu unaweza kutatuliwa
kwa njia mbili tu ambazoni ni ama kuwa na Taifa moja lenye watu wa jamii mbili
zenye kuishi pamoja (One state solution) au kuwa na mataifa mawili ya jamii
mbili zinazopakana (Two state Solution) kama ilivyoamuliwa mwaka 1948 na Umoja
wa Mataifa.
Wazo la kuwa na
Taifa moja (One state solution):
Halikubaliki
miongoni mwa Wapalestina ambao wana hofu kuwa hatua hiyo itawafanya wapoteze
utambulisho wao na kufanywa watu wa daraja la pili nchini Israel. Kwa upande wa
Israel wazo hili linakubalika zaidi na wanasiasa wa mrengo wa kulia nchini
Israel ambao wanataka kuiona Israel ikiwa ni taifa moja. Wasichokitaka
wanasiasa hao wa mrengo wa kulia ni haki ya Wakimbizi wa Kipalestina zaidi ya
7000,000 walioko nje ya Israel kuruhusiwa kurejea nchini humo.Hofu yao ni
kwamba Waarabu watakuwa wengi (Majority) kuliko Wayahudi hivyo kupoteza hadhi
ya Israel kuwa taifa la Kiyahudi ( Jewish state ).
Wazo la Kuwa na
Mataifa Mawili (Two state solution).
Linakubalika kwa
wananchi na wanasiasa wengi wa pande zote mbili. Kikwazo kikubwa katika
utekelezaji wa mpango huu ni hatma ya mji wa Jerusalem na Makazi (Settlements)
ya Walowezi wa kiyahudi yaliyojengwa katika ardhi ambayo Palestina wanatarajia
ndio iwe nchi yao. Ikiwa Palestina wataendelea na dai lao ya kutaka Jerusalem
Mashariki kuwa mji mkuu, Israel inaweza kumaliza mgogoro kwa kuamua kuitwaa
Jerusalem, kuondoa Makazi ya walowezi, kujenga mpaka wa ukuta utakaotenganisha Israel
na eneo la Palestina la ukingo wa magharibi na kisha kuondoa wanajeshi wake
kutoka ukingo wa Magharibi bila kushauriana na upande wowote (Unilateral
Withdrawal). Kwa hatua hii Palestina itakuwa imepoteza dai lake la mji wa
Jerusalem huku ikirejesha maeneo mengine yote yaliyokuwa yanakaliwa.
SULUHISHO
LINALOKUBALIKA KIMATAIFA
• Ni Israel kukaa meza moja na nchi za
Palestina na Jordan ili kujadili na kufikia makubaliano juu ya hatma ya
Wayahudi kufanya Ibada na kuzuru maeneo matakatifu yaliyopo Jerusalem
Mashariki.
• Kuondoa Makazi (Settlements) yote ya
walowezi wa kiyahudi kwenye eneo la Ukingo wa Magharibi.
• Kujiondoa kijeshi katika ardhi yote ya
Palestina kwa kurudisha majeshi yake hadi kwenye mpaka wa Mwaka 1967 kabla ya
vita ya siku sita. (1948 Armistice border)
• Kuondoa mzingiro uliowekwa dhidi ya
Wapalestina huko Ukanda wa Gaza.
Kwa kufanya hivyo
Palestina itakuwa huru. Mgogoro wa haki ya Wakimbizi wa Kipalestina kurudi
nchini mwao utakuwa umemalizika na nchi hizo mbili zitaweza kuishi pamoja
ambapo Jerusalem Magharibi itakuwa mji mkuu wa Israel na Jerusalem Mashariki
itabaki kuwa mji mkuu wa Palestina.

Post a Comment