ZIARA YA SASHA KENYA YAIBUA MJADALA

ZIARA ya siku mbili ya Rais Samia Suluhu Hassan 'SASHA' nchini Kenya, imeibua mjadala mkubwa nchini, kufuatia makubaliano yaliyofikiwa kati yake na mwenyeji wake, Uhuru Kenyatta wa kuondoa vikwazo vya kibiashara baina ya nchi hizi jirani.
Katika ziara hiyo,
wawili hao walitia saini makubaliano ya ujenzi wa bomba la gesi kutoka Dar es
Salaam hadi Mombasa, mradi ambao endapo utafanikiwa, utaisaidia zaidi Kenya
inayohitaji nishati kwa ajili ya matumizi ya viwanda vyake.
Pia, viongozi hao
walikubaliana kuondoa vikwazo kwa wafanyabiashara wa nchi hizo mbili, ambapo
kwa kuanzia, Rais Uhuru alitaka wafanyabiashara wa Tanzania kuwekeza bila
kuhitaji kwanza vibali vya kufanya kazi (working permit).
Pia, mgogoro
kuhusiana na mahindi ya Tanzania ambayo yalikuwa yamezuiwa mpakani, yametakiwa
yawe yameruhusiwa kuingia Kenya ndani ya wiki mbili kuanzia juzi.
Kwa nyakati
tofauti, watanzania wamekuwa na mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii juu
ya makubaliano hayo, wengi wakionekana kuridhishwa nayo, huku wachache
wakijiuliza kama itimisho la ziara hiyo lina tija kwa taifa.
Wanaounga mkono
makubaliano hayo, walisema Tanzania itafaidika kwa kupata uwekezaji zaidi
kutoka Kenya, hivyo kusaidia katika kukabiliana na tatizo la ajira, aidha pia
kupata fursa ya kujifunza na kunufaika na uzoefu wa Kenya katika biashara ya
bidhaa za viwandani.
Eneo jingine ambalo
Tanzania itanufaika nalo ni soko la uhakika kwa bidhaa za kilimo, kama vile
nafaka, matunda na maua.
Wale wanaotilia
shaka ushirikiano huo mpya, wanadai kwa kuipelekea Kenya gesi, itamaanisha kuua
viwanda vyetu, kwani majirani hao wenye uzoefu katika viwanda, watatengeneza
bidhaa zao kwa gharama ndogo na hivyo kuvishusha bei hapa nchini, kitu ambacho
kitapelekea kukosa soko kwa bidhaa zetu.

Post a Comment