DKT ABBAS ATAKA SPORTS BETTING ZICHANGIE TIMU ZA TAIFA

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi amezitaka Kampuni za Ubashiri wa Michezo (Sports Betting) kuwa sehemu ya kuinua na kukuza michezo nchini.
Dkt. Abbasi amesema
hayo Mei 05, 2021 Jijini Dar es Salaam katika kikao na Kampuni hizo ambapo
amesema kuwa Michezo ya Kubashiri ( Sports Betting) inayo nafasi kubwa katika
kuchangia maendeleo ya timu za Taifa hasa pale zinapokuwa katika mashindano.
“Lengo la Serikali
kwa sasa ni kuwekeza kimkakati kwenye michezo, tuwe na mpango wa moja kwa moja
wa kuzisaidia timu zetu za Taifa kifedha, mimi naamini tukishirikiana kwa
karibu tunaweza kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya michezo.” Alisema Dkt.
Abbasi.
Katibu Mkuu
Dkt.Abbasi amesisitiza kuwa changamoto zilizopo katika Kampuni hizo
zitatafutiwa ufumbuzi kupitia vikao na njia mbalimbali baina ya Serikali na
Kampuni hizo, ambapo amesisitiza ushirikiano kwa pande hizo mbili katika
kusaidia nchi.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Chama Cha Ubashiri wa Michezo Tanzania (TSBA) Jimmy Kenneth
ameiomba Serikali kutatua baadhi ya changamoto ikiwemo uwepo kwa kampuni za
ubashiri ambazo hazina usajili nchini ambazo zinaisababishia nchi kukosa mapato
ambapo Dkt.Abbasi ameahidi kufanyia kazi suala hilo.
Wadau hao kwa
pamoja wameonesha utayari wa kuzisaidia timu za Taifa huku wakiiomba Serikali
kuweka msisitizo wa mazingira rafiki ya ulipaji kodi.

Post a Comment