WAZIRI NDUMBARO AJA NA OPARESHENI ONDOA WAFUGAJI KWENYE HIFADHI
NA STEPHANO MANGO, TUNDURU
WAZIRI wa maliasili na utalii Dkt Damas Ndumbaro, ametangaza
operesheni kabambe ya kuwaondoa wafugaji wote waliovamia na kufanya shughuli
zao katika hifadhi ya Taifa ya Nyerere na maeneo mbalimbali yaliyotengwa kwa
ajili ya utalii hapa nchini.
Dkt Ndumbaro ametangaza hatua hiyo jana wakati akiongea na
wananchi wa vijiji vya Kalulu na Jakika wilayani Tunduru, wakati wa ziara yake
ya kusikiliza kero ya wananchi kuhusiana na wanyamapori wanaovamia mashamba na
kufanya uharibifu wa mazao wilayani humo.
Alisema, tatizo la wanyama hususani Tembo wanaokula mazao ya
wakulima limechangiwa kwa kiasi kikubwa na wafugaji kuingiza mifugo yao kwenye
maeneo yasioruhusiwa kisheria jambo linalosababisha wanyama hao
kukimbia.
Kwa mujibu wa Dkt Ndumbaro, Serikali imeshatenga maeneo maalum
kwa ajili ya shughuli za ufugaji, lakini kutokana na kiburi cha
fedha wafugaji wanawatumia baadhi ya wenyeviti na watendaji wa
serikali za vijiji wasiokuwa waaminifu kukaidi na kupeleka
mifugo kwenye maeneo waliyotengewa.
Dkt Ndumbaro amewaonya wenyeviti na watendaji wa vijiji hao
kujiepusha na vitendo vya rushwa kwa kupokea fedha na
kuruhusu wafugaji kufanya shughuli zao kwenye maeneo ya utalii kwani tabia hiyo
ni kukiuka sheria za utumishi wa umma.
Waziri Ndumbaro, amewataka wananchi
kuepuka kuishi na kufanya shughuli zao kwenye hifadhi
kwani serikali haitahusika kulipa fidia wala kutoa kifuta machozi
kwa mtu atakayepoteza maisha, kujeruhiwa na kuharibiwa mazao.
Alisema, ili kukabiliana na wanyama wanaovamia mashamba na
kuharibu mazao,serikali kupitia wizara ya maliasili imeanza kutoa
mafunzo kwa vijana kwenye vijiji vinavyozungukwa na hifadhi na mapori ya akiba
ili kuwajengea uwezo wa kufukuza wanyama pindi wanapofika kwenye makazi ya
watu.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro
alisema,wilaya hiyo ni ya kilimo lakini changamoto kubwa ni kuvamiwa
na wafugaji na mifugo mingi kutoka katika maeneo mengine ya nchi jambo lililosababisha
kutokea kwa migogoro kati ya jamii ya wafugaji na wakulima.
Alisema, licha ya serikali ya wilaya kutenga zaidi ya vitalu
200 vya ufugaji, lakini jambo la kusikitisha baadhi ya viongozi wa
ngazi za vijiji wanaruhusu wafugaji kupeleka mifugo kwenye maeneo
yasioruhusiwa.
Mtatiro ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama
alisema, katika kukabiliana na changamoto hiyo serikali ya wilaya inafanya
operesheni za mara kwa mara kuwaondoa wavamizi wote wanaofanya shughuli za
kibinadamu kwenye hifadhi na maeneo yote yasiyoruhusiwa.
Baadhi ya wananchi wa vijiji hivyo,wameiomba serikali kupitia
upya
viwango vya fedha vinavyotolewa kwa waathirika wa matukio ya
kushambuliwa na wanyama wakali na wanapoharibu mazao
kwani havilingani na hasara inayotokea.
Mwenyekiti wa Baraza la wazee wilaya ya Tunduru Ajili Kalolo
alisema, wananchi wanalazimika kuondoa mazao yao mashambani kabla hayajakomaa
ili kuepuka kuliwa na wanyama.
Kalolo alisema, kama serikali itaendelea na msimamo wake wa
kuwaona wananchi ndiyo wenye makosa kwa kile kinachodaiwa kuvamia kwenye
hifadhi basi kuna hatari wilaya hiyo kukumbwa na janga la njaa.
Msanga Rashid mkazi wa kijiji cha Kalulu, ameiomba
wizara ya maliasili kuwasaidia kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu wa
mazao,badala ya kuwaona wananchi ndiyo wakosaji kwani kama serikali
itaendelea na msimamo huo kuna hatari baadhi ya vijiji kutokuwa na
watu kwa kuuawa na wanyama.

Post a Comment