WAPENI VIPAUMBELE WANANCHI KATIKA MIRADI YA UJENZI – WAITARA
NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Mwita
Waitara amewataka viongozi wa mikoa ya Mtwara na Lindi wanaosimamia kazi za
ujenzi wa barabara na viwanja vya ndege kutoa vipaumbele vya ajira kwa
wananchi.
Amesema hatua hiyo licha ya kuwawezesha kiuchumi
wananchi pia itawafungamanisha wananchi hao na miradi hiyo na hivyo kuwafanya
wawe walinzi wazuri wa miradi kwa muda wote na kuiwezesha kudumu kwa muda
mrefu.
“Meneja hakikisha unashirikiana na viongozi wenzako
ili kuwatambua wananchi wazalendo na wenye uwezo wa kufanya kazi kwa bidii na
uaminifu ili wapate ajira…,” amesema Waitara.
Naibu waziri huyo amesema Serikali imepanga
kufungua miundombinu ya mikoa ya Lindi na Mtwara kwa kuboresha Bandari, Uwanja
wa Ndege wa Mtwara na Barabara ya Mtwara – Nanyamba – Tandahimba – Newala –
Masasi yenye urefu wa kilomita 210 ili kuhuisha huduma za kilimo na hatimaye
kukuza uchumi wa maeneo hayo.
“Fanyeni kazi kwa bidii, ongezeni kasi ya kilimo
cha mazao ya chakula na biashara kwa sababu miundombinu hii ikikamilika
itavutia wawekezaji wengi kuja kuwekeza na kuchochea ukuaji wa uchumi kwa
wananchi kwa ujumla,” amesisitiza Naibu Waziri huyo.
Kwa upande wake Mbunge wa Mtwara Mjini, Mhe. Hassan
Mtenga ameitaka Serikali ikamilishe miradi ya ujenzi wa miundombinu katika
Ukanda wa Kusini kwa wakati ili kuepuka gharama zisizo za lazima na kuepuka migogoro
kati ya Serikali na wananchi hali inayochelewesha baadhi ya miradi.
Naye Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mtwara, Eng. Dotto
John amemhakikishia Naibu Waziri Waitara kwamba miradi yote ya barabara
itakamilika kwa wakati na barabara zitapitika wakati wote, huku Meneja wa
TANROADS Mkoa wa Lindi, Eng. Efatha Mlavi akisisitiza kwamba Barabara ya
Ruangwa – Nanganga Km 53 inayojengwa kwa kiwango cha lami itakamilika Novemba
mwakani.
Naibu Waziri Waitara alikuwa katika ziara ya siku
mbili katika mikoa ya Lindi na Mtwara ambapo pamoja na mambo mengine amekagua
maendeleo ya miundombinu ya Bandari, Uwanja wa Ndege na barabara.
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Post a Comment