WANAANGA WANNE WAREJEA DUNIANI BAADA YA SIKU 168 ANGA ZA JUU
Wanaanga wote wanne mara baada ya kufika
duniani kutoka kwenye kituo cha kimataifa cha anga za mbali.
Washington, Marekani.
Chombo cha kampuni
ya utafiti wa anga za juu ya SpaceX, kilichobeba wanaanga wanne kimerejea
duniani na kutua Florida Jumapili asubuhi, ikiwa ni mara ya kwanza kutua usiku
baharini.
Wanaanga hao
wameripotiwa kuwa wanaendelea vizuri kiafya baada ya kurejea duniani baada ya
kuwa katika Kituo cha Kimataifa cha Anga za Juu (ISS) kwa miezi sita, taasisi
ya NASA ilisema.
Chombo hicho
kilitua saa 8:56 usiku katika ghuba ya Mexico nje ya Panama City baada ya
kusafiri kwa saa sita-na-nusu kutoka ISS, picha za usiku zilizotolewa na NASA
zinaonyesha.
Timu zilizokuwa
katika meli ya Navigator zilikivuta chombo hicho na kukipakia melini kwa karibu
saa moka-na-nusu baadaye. Kwa NASA, hii ni mara ya kwanza kwa chombo cha anga
za juu kutua usiku tangu wanaanga waliokuwa katika chombo cha Apollo 8 walipotua
Bahari ya Pacific Desemba 27, 1968.
Kamanda Michael
Hopkins alikuwa wa kwanza kushuka baada ya mlango wa chombo hicho mithili ya
yai kufunguliwa, akijaribu kunyanyua miguu melini, na muda mfupi baadaye
kufuatiwa na mwanaanga mwenzake wa NASA, Victor Glover.
"Kwa niaba ya
wanaanga na familia zetu, tunataka tuseme tu asante ... Ni kitu cha kufurahisha
kwa kile tunachoweza kufanikisha wakati watu wakishirikiana. Wote mnaibadili
dunia. Hongera. Ni kitu kizuri kurejea," Hopkins alisema katika ujumbe wa
NASA uliotumwa Twitter.
Mwanaanga wa NASA,
Shannon Walker na Mjapani Soichi Noguchi ni watu wengine waliokuwa katika
chombo hicho.
Zilikuwa maili
milioni 71 ambazo wanaanga hao wanne walienda anga za juu Novemba mwaka jana
wakiwa katika mpango wa kwanza kamilifu wa kikazi katika kituo cha ISS
wakitumia chombo kilichotengenezwa na kampuni ya SpaceX inayomilikiwa na Elon
Musk.
SpaceX imekuwa
mshirika ambaye NASA inaonekana kupenda kufanya naye usafirishaji wa kibiashara
kwenda anga za juu.
Wanaanga hao
walisafiri maili milioni 71.2 (sawa na kilomita milioni 114.6) ndani ya siku
168 walizokuwa katika mzingo wa dunia (zikiwemo siku 167 walizokuwa katika
kituo hicho cha anga za juu), NASA ilisema.
Baada ya uchunguzi
wa kiafya, wanaanga hao wanne walitarajiwa kusafirishwa kwa helikopta kwenda
Pensacola kwa ajili ya kupanda ndege ya kuwapeleka Houston kuungana tena na
familia zao na marafiki, NASA ilisema.
Kabla ya safari yao, wanaanga wawili wa Kimarekani walifanya majaribio ya kwenda ISS mwezi Mei na kuishi huko kwa miezi miwili.
Hiyo ilikuwa ni
mara ya kwanza kuanzisha safari ya kwenda ISS kutokea ardhi ya Marekani tangu
mwaka 2011. Pia ilikuwa ni safari ya kwanza iliyojumuisha wanaanga kuendeshwa
na kampuni binafsi, tofauti na za NASA.

Post a Comment