MV MWANZA KUKAMILIKA MWAKANI


  

Muonekano wa Meli ya Mv -Mwanza Hapa Kazi tu unavyoendelea kujengwa  na  hadi sasa ujenzi  wake umefikia asilimia 74 na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwaka 2022.


 

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi DktLeonard Chamuriho amesema ujenzi wa Meli ya Mv Mwanza Hapa kazi tu ambao hadi sasa umefikia asilimia 74 utakamilika baadaye mwakani.

Waziri Chamuriho ameyasema hayo leo jijini Mwanza alipokuwa akikagua ujenzi wa meli hiyo ya kisasa inayojengwa na Kampuni ya Gas Ente kutoka Korea ya kusini ikishirikiana na Kaang Nam Corperation pamoja na Suma JKT.

Aidha Waziri Chamuriho amesema ujenzi wa meli hiyo ni moja ya miradi mikubwa minne inayotekelezwa na  kampuni ya huduma za Meli Nchini (MSCL) na kusimamiwa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi. 

“Miradi mengine inayotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa ni pamoja na ukarabati  wa Meli ya New Victoria, Ujenzi wa MV Butiama pamoja na Chelezo ambayo ujenzi wake umekamilika”, amesema Chamuriho.

Katika hatua nyingine Waziri Chamuriho amesema Wizara pia imejipanga kuendeleza miradi mingine katika Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa ikiwemo mradi wa Ukarabati wa meli kongwe ya MV Liyemba.

Kwa upande wake Msimamizi wa mradi wa ujenzi wa Mv Mwanza Mhandisi Vitus Mapunda amesema Ujenzi huo umeajiri Zaidi ya watumishi 180 katika kada mbalimbali na utakapokamilika utaleta fursa nyingi za ajira nchini.

Naye Kaimu Mtendaji Mkuu wa Huduma  za Meli (MSCL) Philemon  Bagambilana amesema kampuni imejipanga kuboresha na kutoa huduma bora katika usafiri wa majini kwenye Ziwa Victoria, Ziwa Nyasa, Ziwa Tanganyika na kupanua huduma kwenye Bahari ya Hindi.

 

 

IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI WIZARA YA UJENZI NA UCHUKUZI.

 

 

No comments