WAJUE 'MAJASUSI' WALIOONGOZA USALAMA WA TAIFA
IDARA ya usalama wa Taifa (TISS)
imeundwa kwa sheria ya bunge namba 15 ya mwaka 1996 (Tanzania Intelligence and
Security Service act No. 15 of 1996) iliyosainiwa na Rais Benjamin Mkapa tarehe
20 mwezi Januari mwaka 1997. Sheria hiyo ndio inayoipa mamlaka Idara hiyo
kufanya kazi zake ndani na nje ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania.
Pamoja na idara hii kusajiliwa kisheria mwaka 1996, lakini ilkuwepo tangu
wakati wa utawala wa kikoloni chini ya ofisi ya Gavana wa Tanganyika. Baada ya
Uhuru mwaka 1961 ilihamishiwa ofisi ya Rais.
Tangu idara hii kuanzishwa hadi sasa imeongozwa na Wakurugenzi 9 akiwemo Diwani
Athumani Msuya aliyepo kwa sasa
Wa kwanza ni mzee Emilio Mzena, huyu aliongoza mwaka 1961 hadi mwaka 1975.
Ndiye Mkurugenzi wa TISS aliyeongoza idara hii kwa miaka mingi zaidi kuliko
wengine (miaka 14). Aliaminiwa na Mwalimu Nyerere baada ya idara yake kuzima majaribio
kadhaa ya kumpindua.
Wa pili ni Dr. Lawrence Gama (PhD). Huyu alipokea kijiti kutoka kwa Mzena.
Aliongoza kwa miaka mitatu tangu mwaka 1975 hadi mwaka 1978, kabla ya Mwalimu
Nyerere kumuondoa katika nafasi hiyo na kumteua kuwa mkuu wa mkoa wa Dodoma.
Wa tatu ni Dr. Hassy Kitine (PhD) ambaye aliongoza idara hii kwa miaka miwili
toka mwaka 1978 hadi 1980. Kitine alichaguliwa kuongoza idara hiyo nyeti akiwa
kijana wa miaka 36 tu. Anakumbukwa kwa jinsi alivyoiwezesha TISS kushirikiana
na Idara ya Usalama na Utambuzi Jeshini (MI) Chini ya Meja Jenerali Tumainieli
Kiwelu, kuiteka nyara ndege ya makomandoo kutoka Libya iliyokuja kumsaidia Idd
Amin katika vita ya Kagera.
Mwaka 1980 Mwalimu Nyerere alimteua kijana mwingine mwenye miaka 35 Dr.
Agustine Mahiga (PhD) - (Marehemu) ambaye alikuja kuwa Waziri wa Mambo ya Nje
na baadaye Waziri wa Sheria chini ya Hayati Rais Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli - kuwa Kaimu Mkurugenzi mkuu wa TISS. Alikaimu nafasi hiyo hadi mwaka
1983, Nyerere alipomuondoa na kumteua Kaimu Balozi wa Tanzania (Minister
Plenipotentiary) nchini Canada.
Baada ya Mahiga kwenda Canada, Mwalimu Nyerere alimteua Luteni Jenerali Imrani
Kombe kuwa Mkurugenzi mkuu wa 5 wa TISS mwaka 1983. Nyerere alipong'atuka
alimuacha Kombe kwenye idara hiyo na alidumu hadi mwaka 1995.
June 30 mwaka 1996 Jenerali Kombe aliuawa na Jeshi la polisi kwa madai kuwa
walifananisha gari lake (Nissan Patrol) na gari iliyokua imeibiwa na mtuhumiwa
Ernest Mushi maarufu kama "White".
Alimininiwa risasi 4 kifuani licha ya kushuka kwenye gari na kunyoosha mikono
juu kama ishara ya kusurrender. Askari waliohusika na mauaji hayo walihukumiwa
kunyongwa lakini Rais Kikwete aliwapunguzia adhabu mwaka 2011. Bado kifo cha
Jenerali Kombe kina maswali mengi kuliko majibu.
Baada ya Kombe kuuawa alifuata Kanali Apson Mwang'onda. Huyu aliteuliwa na Rais
Benjamin Mkapa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa 6 wa TISS ambaye aliongoza Idara hiyo
hadi mwaka 2005 alipostaafu. Cornel Mwang'onda anasifiwa kwa kuifanyia
marekebisho makubwa idara ya TISS ya kimfumo na kiutendaji. Ndiye aliyewezesha
muswada uliounda sheria ya TISS mwaka 1996.
Mwaka 1980 Mwalimu Nyerere alifanyiwa jaribio kubwa la kutaka kupinduliwa na
baadhi askari wa JWTZ (akina Tamin, McGhee na Kepteni Maganga) . Hili lilikua
jaribio la 3 kubwa la kumpindua Nyerere, lakini ni jaribio la 7 katika orodha
ukijumlisha na mengine madogo. Cornel Apson Mwang'onda akiwa Mkurugenzi wa
ndani wa TISS (DOI) alifanikiwa kuzima jaribio hilo. Historia hii ilimuongezea
sifa ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi mkuu wa TISS mwaka 1995.
Mwaka 2005 Rais Jakaya Kikwete alimteua Othman Rashid kuongoza Idara hiyo hadi
mwaka 2016 alipostaafu. Othmna Rashid alikuwa Mkurugenzi wa 7 wa idara hiyo.
August 24 mwaka 2016 Rais John Magufuli alimteua Mchungaji Dr. Modestus Kipilimba
(PhD) wa Kanisa la City Harvest Church la jijini Dar es Salaam kuwa Mkurugenzi
Mkuu wa 8 wa TISS. Kabla ya uteuzi huo Kipilimba alikua Kaimu Mkurugenzi Mkuu
wa Mamlaka ya Vitambulisho vya taifa (NIDA).
Mchungaji Dr. Kipilimba amedumu katika nafasi hiyo hadi September 12 mwaka 2019
alipotenguliwa uteuzi wake na nafasi yake kuchukuliwa na Kamishna wa Polisi CP
Diwani Athumani Msuya.
Credit: Jamii Forum

Post a Comment