VIONGOZI NAMTUMBO WANASUBIRI MABANGO YA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN?

NA STEPHANO MANGO, SONGEA
WANANCHI kote nchini
bado wana kumbukumbu na hotuba za Rais Samia Suluu Hassan, alizotoa katika
matukio mbalimbali ambapo ameonyesha mwelekeo wa serikali yake kwa kutoa
maelekezo yenye nia ya kutibu majeraha na kugusa maeneo yaliyo kuwa yakilalamikiwa
na kukwamisha kasi ya maendeleo.
Akihutubia baada ya
kuwaapisha Mawaziri, Manaibu Waziri, Makatibu Wakuu na Manaibu Makatibu,
alisisitiza ufanyaji kazi wenye kuondoa kero kwa wananchi na uletaji
tija kwa taifa na kuepusha mabango kutoka kwa wananchi.
Rais aliwaonya
watendaji wa chini akisema kuwa viongozi wakikutana na mabango ya
malalamiko katika ziara zao basi atawaondoa Mkurungenzi wa
Halmashairi husika pamoja na Mkuu wa wilaya hiyo.
Alisema imekuwa ni
kawaida viongozi wakifanya ziara mkoani na wilayani wanapokewa na mabango ya
wananchi wakilalamikia kero mbalimbali na masuala yanayolalamikiwa sio ya
kitaifa.
“Naomba tunapokuja
huko, Mimi, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu, tukikuta bango basi ziwe ni issues (masuala)
ya kitaifa lakini si mambo ya kushughulikiwa kule chini.
"Nataka niseme
bango moja aidha Mkurugenzi au Mkuu wa wilaya amekwenda, na hii haina maana mkazuie
watu kuandika kero zao, naomba kero za wananchi zikashughulikiwe. Tumekuja
tumekuta bango moja, Mkuu wa wilaya na Mkurungenzi umekwenda.
"Ninaomba
mkafanye kazi na kuwatumikia watanzania bila ubaguzi kama mlivyoapa hapa, mkawe
msaada na si bugudha au adha kwa watanzania, mkawe neema na sio kero na nuksi
kwa watanzania, mkasimamie haki na sio udhalimu na dhulima na unyanyasaji kwa
watanzania," alisema Rais Samia.
Pamoja na onyo hilo, bado
kuna viongozi, pengine kwa kufanya kazi kwa mazoea au makusudi, wanapuuzia kutatua kero za wananchi jambo
ambalo linaweza kusababisha uwepo wa mabango wakati wa ziara ya viongozi
wakuu wa nchi.
Hivi karibuni
imeripotiwa habari za kuwepo kwa mgogoro wa ardhi kati ya mkuu wa wilaya
mstaafu wa Namtumbo, Luckness Amlima na wananchi katika kitongoji cha Nyerere
katika kijiji cha Mchomoro.
Wananchi kutoka koo 16
wa kijiji hicho kilichopo katika Kijiji cha Mchomoro kilichopo katika
Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma, walimuomba aliyekuwa Mkuu wa
Mkoa wa Ruvuma, Christine Mdeme kuingilia kati utatuzi wa mgogoro wa
ardhi yao zaidi ya heka 700 kati yao Luckness Amlima ili waweze kuendelea na
shughuli zao za kimaendeleo.
Wananchi hao
wanalalamika kuwa wakiwa na familia 68 wamekuwa hawasikilizwi na viongozi wao,
wakihisi wanamlinda kiongozi mwenzao, kwani kwa zaidi ya miaka minne sasa wamekuwa
wakipuuzia mgogoro huo kwa sababu zao binafsi hali ambayo inaashiria kuwa ni
kumpendelea mkuu huyo wa wilaya mstaafu.
Rashid Malamaye anayesimama
kwa niaba ya koo hizo, anasema mkuu huyo wa wilaya amevamia katika maeneo yao
ya asili ambayo wao walikuwa wanayatumia kwa shughuli za kilimo na ufugaji kwa
miaka mingi.
Anasema katika
mashamba hayo kulikuwa na nyumba za nyasi, mazao ya muda mrefu aina ya minazi,
machungwa, migomba na mihogo yamechomwa moto na kufyekwa, huku pia walinzi
wakiwa wamewekwa kulinda maeneo yao kuwazuia wasiingie.
Taarifa zinasema
kiongozi huyo wa zamani aliomba na kupewa kiasi cha heka 40, lakini kwa
mshangao wa wananchi, amedhulumu ekari 700, tena bila vikao vya vijiji kama
sheria inavyosema.
Wananchi
wanasikitishwa na jambo hili kwani viongozi wa kijiji badala ya kulinda raia na
mali zao wao wamekuwa chanzo cha kutengeneza migogoro kinyume na kiapo chao cha
uadilifu ambacho waliapa.
Alifafanua kuwa hali
iliyopo kwa sasa sio nzuri kwani wenye mashamba wakienda kufanya shughuli zao
wanakamatwa na kufunguliwa kesi mbalimbali katika kituo cha polisi Wilaya ya
Namtumbo hali ambayo inazidisha uhasama kati ya wananchi na mkuu huyo.
Mwenyekiti wa kijiji
hicho Said Mohamed Mkalela anakiri kuwepo kwa mgogoro huo na kusema kuwa hatua
zinaendelea kuchukuliwa ingawa wananchi hao wamekuwa wakikosa imani nao
kutokana na kuchelewa kumalizika kwa mgogoro huo.
Mkalela alisema kuwa
wao waliingia madarakani mwaka 2019 lakini nyaraka zinaonyesha mwekezaji huyo
alipata eneo la heka 40 kihalali toka mwaka 2016 katika maeneo ya Namambigi na sio
Mihane, lakini hatua za kutatua mgogoro huo zinaendelea ingawa wananchi
wanateseka.
Cha kushangaza,
mtuhumiwa anakataa kuwepo kwa mgogoro huo, akidai waulizwa viongozi wa vijiji.
Katibu Tawala wa
Wilaya, Aden Nchimbi anakiri kuusikia mgogoro huo na kuagiza wahusika kwa
kushirikiana na afisa ardhi wa Halmashauri kukutana na kuumaliza ili
kuwaondolea kero wananchi.
Jambo lililo wazi hapa
ni kuwa viongozi wa vijiji hawawezi kuutatua mgogoro huo kwa vile wana masilahi
kwenye suala hilo.
Taarifa zilipofika
hapo zinaonyesha kuwa mkuu huyo aliomba mashamba heka 50 na kupewa
heka 40 kisheria kwenye mashamba ya Namambigi lakini katika mazingira ya kutatanisha
hivi sasa ana miliki heka zaidi ya 600 na kusababisha uvamizi wa mashamba ya
wananchi.
Uvamizi huo umepelekea
kufika mpaka kwenye mashamba ya wanakijiji katika eneo la Mihane ambapo mazao
yao aina ya michungwa, minazi, na migomba ilifyekwa huku wananchi wakikamatwa
na kubambikwa kesi na mkuu huyo wa wilaya mstaafu.
Viongozi wa kijiji
ambao wana jukumu la kulinda raia na mali zao hawajachukua hatua stahiki za
kukomesha mgogoro huu kwani wanaonyesha kumbeba kiongozi huyo wa zamani.
Kwa namna mazingira ya
suala hili yalivyo, wanakijiji wakiwa wametoa taarifa za mgogoro huo kwa
viongozi wao wa CCM, Mkurugenzi wa Halmashauri, na Mkuu wa Wilaya, ni wazi kuwa
hitimisho la suala hilo ni mabango kwenye ujio wa viongozi wa kitaifa kwani
muunganiko wa viongozi wa ngazi zote wakikandamiza, ni vigumu haki kutendeka.

Post a Comment