USIJIDANGANYE, HAKUNA ANAYEKUZUNGUMZIA VIZURI
KUNA dhambi moja
kubwa sana ya asili ambayo sisi ngozi nyeusi tunayo, ubinafsi. Hii ni dhambi kubwa
ambayo imezalisha dhambi zingine nyingi ndogo ndogo, lakini ambazo zina madhara
makubwa katika maisha yetu ya kila siku.
Ubinafsi ninaousema
hapa hata wewe unayesoma makala haya unao. Ule wa kutamani vitu vyote vizuri
vinakuwa upande wako, yaani uwe na nyumba nzuri, gari zuri, mume handsome, mke
beautiful, mchumba mzuri, mshahara mnono, biashara kubwa, yaani kama hivyo!
Sina uhakika, na nasema tena sina uhakika, kama
kuna mtu angependa kumuomba Mwenyezi Mungu mambo hayo mazuri yamkute jirani
yake. Kama yupo, mtu huyo, hapa duniani, naamini njia ya peponi kwake ni nyeupe
kabisa.
Siyo vibaya kuwa na
mawazo ya kutaka kupata kila kitu kizuri, kinachotufanya sisi tuonekane wa
ajabu ni kwamba wakati tunajiombea mazuri, tunawaombea wenzetu mabaya!
Yaani wakati wewe
unajiombea gari kali la kisasa na la gharama la kutembelea, mimi huniombei
nipate japo baiskeli. Ungependa nitembee kwa miguu ili siku moja unipe lifti
nione jinsi gari lako lilivyo bomba.
Ndiyo maana katika
hali halisi, huwa tunazungumza maneno mengi sana juu ya watu waliofanikiwa.
Mwizi yule, mchawi yule, jambazi, anajiuza huyo, anauza unga na vitu vingine
vya namna hiyo.
Yaani huwa tupo tu
na negativity kwa wenzetu. Siyo kwamba hatuamini katika watu kufanikiwa, la
hasha. Watu tunawaona wanavyopambana na baadhi yao kushinda vita. Sisi tu tunaongozwa
na ile dhambi, yaani mafanikio ya mtu tunapenda kuyatia doa, ili mradi tu isiwe
kirahisi namna hiyo.
Ubinafsi huu tulio
nao, umetufanya hata tusiwape thamani watu wema ambao Mwenyezi Mungu
amewajaalia uwezo wa kutoa. Mtu akiwa na tabia ya kuwapa watu wanaohitaji kwa
urahisi, tunakimbilia kumpaka matope " Masharti ya mganga hayo"
Maana ni lazima pia
tukubali kuwa pamoja na dhambi hii ya ubinafsi, kuna baadhi yetu wamejaaliwa
karama ya kupata na kutoa. Yaani mtu anafanya vizuri kwenye kazi zake na wakati
huo huo, ni mwepesi kuguswa na shida za wengine. Anapojitokeza mtu wa namna
hii, na hasa akiwa ni mfanyabiashara, tutasema anafanya hivyo kwa sababu mganga
wake kampa hayo masharti!
Dhambi hii ya
ubinafsi imetufanya tuwe watu wa kusengenyana, wanafiki na tuliojaa hadaa
nyingi. Unaweza kuwa na majadiliano na wenzako, tuseme muwe zaidi ya watatu. My
friend, yaani ukitoka tu, huku nyuma badala wajadili yale uliyoyatoa,
wanakujadili wewe!
Wakati pekee ambao
angalau unajifariji kuwa watu hawakusemi vibaya, ni pale tu unapokuwa nao,
yaani ukiachana nao wewe unageuka kuwa ajenda.
Ndiyo maana
nikasema, usije ukajidanganya mwenyewe kwa kudhani kuwa kwa sababu una mashoga
zako, rafiki zako, au ndugu zako basi wewe upo salama. Hata kama unawasaidia,
kuna nyakati wanakusimanga na kukuombea mabaya.
Just imagine mtu
anakutatulia shida zako, anakupa connections, anakupa michongo na vitu kama
hivyo, lakini akiondoka, unaanza kuzungumza kuhusu udhaifu wake.
Kuna wale wa kula
vyombo. Unaweza kuwaita rafiki zako kwa ajili ya kupiga nao stori mbili tatu
huku mkipiga moja baridi moja moto. Watakuja na mtakaa pamoja mnabadilishana
mawazo. Ukiondoka kwenda chooni, wanabadilisha mazungumzo: "Sijui kazifuma
wapi mbwa huyu, leo mbona tutakoma!"
Usione wanakupamba
ukawaona ndiyo marafiki, wanakumaliza sana usipokuwa nao. Wengine wanakupamba
kwa sababu wameuona udhaifu wako upo hapo. Si unajua kuna wenzetu wengine wana
kilema cha kupenda kusifiwa? Sasa wakigundua una kipaji hicho na bahati nzuri
ukawa na mafanikio kimaisha, usijisahau.
"Ukitaka hela
yake yule bwege wee mpambe tu, hata milioni anakupa."
Ninachojaribu
kusema hapa ni kwamba, jitahidi kwa kadiri unavyoweza, kuishi maisha yako.
Usije ukajikondesha bure kwa kujiona huna kitu. Kitu kikubwa sana ambacho Mungu
amekujaalia ni afya, hivyo vingine vinapatikana ukiweka bidii.
Au usijione una
kasoro hii na kwamba watu wanakuzungumzia sana. Puuza hayo mawazo. Uwe na
kasoro, usiwe na kasoro, watu hawataacha kukusema.
Hebu fikiria,
pamoja na upendo wote ambao Yesu anasemwa alikuwa nao, lakini bado watu
walimtia ubaya, wakamuadhibu kikatili na kumuua. Sasa wewe ni nani hata uachwe?
Pambana na maisha yako, kila
mtu kimpango wake!

Post a Comment