UKARIBU NA CHOKI ULIVYONIPONZA TWANGA PEPETA

 VIDEO MUSIC | Ally Choki Ft Jack Chant – Natamani | DOWNLOAD Mp4 SONG |  MTIKISO ENTERTAINMENT

 

NI wakati ule African Stars ipo katika ubora wake, ile Twanga Pepeta yenyewe ikiwa na nyota wake kibao, ikiwa imesheheni kila idara.

Ile Twanga ambayo kila mpenzi wa burudani ya muziki aliipenda na kuufanya uwanja wao wa nyumbani pale Mango Garden Kinondoni uwe haukauki nyomi ya watu kila Jumamosi. Jumapili watu pia walijaa sana viwanja vya Leaders Club nyakati za mchana na usiku ulimalizika kwa mashabiki wa Temeke na viunga vya jirani kujivinjari pale TCC Chang'ombe.

Twanga pepeta iliyokuwa ina -shine mbele ya bendi zingine kali kama FM Academia ya Nyoshi el Saadat, TOT ya Ramadhan Masanja 'Banzastone', Mchinga Sound ya Adolph Mbinga na Roggart Hegga, Akudo Impact ukiachilia mbali Msondo na Sikinde.

Asha Baraka 'Iron Lady' aliifanya bendi yake kuwa bora ambayo iligeuka na kuwa ndoto ya kila mwanamuziki kuitamani. Kumbuka ile safu kali ya uimbaji chini ya Ally Choki, Jessica Charles, Salehe Kupaza, Luiza Nyoni (Mbutu) na Hamis Amigolas.

Kulikuwa na mpiga ngoma anaitwa MCD na mpiga gitaa Abuu Semhando. Kama kuna eneo ambalo bendi ile ililipatia, basi ni katika ile unenguaji. Acha kabisa, kulikuwa na Aisha Madinda na Lilian Internet, walikuwa mastaa wakubwa sana enzi hizo.

Nilikuwa mwandishi wa habari za michezo na burudani wakati huo. Nilifahamiana na wanamuziki wengi na baadhi yao kujenga ukaribu hata katika maisha nje ya muziki. Miongoni mwa watu nilioelewana nao sana alikuwa ni Ally Choki mwenye majina mengi ya utani kama Mzee wa Farasi, Mzee wa Kijiko, Mwarabu wa Kibaha, Kamarade na kadhalika.

Kuna nyakati ambazo Choki ndiye alikuwa ni nyota mkubwa kabisa katika kundi hilo, licha ya wanamuziki wote wa bendi hiyo kuwa mastaa. Wanamuziki wote wangepanda jukwaani lakini Choki alikuwa wa mwisho na ndiye ambaye angetunzwa sana na mashabiki kuliko wenzake.

Kutokana na ukaribu huo, nami nikawa naandika mara kwa mara habari zake na za bendi yake, ingawa pia niliandika na za wanamuziki na bendi zingine. Kama ambavyo ilitokea katika kumbi zote, niliingia bure kwa sababu ya kazi yangu. Maana licha ya kuburudika, lakini pia ningetoka na habari ya kuweza kuandika kesho yake.

Ikatokea siku moja, Ally Choki alijiondoa Twanga na kuanzisha bendi yake, Extra Bongo 'Next Level' ambayo alisaidiwa uendeshaji na mtu mmoja anaitwa Fikiri Madinda. Japo ilikuwa ni bendi changa, lakini jina la Choki liliibeba.

Ikatokea kupata umaarufu mkubwa ghafla na hivyo kuonekana kama mshindani wa        African Stars. Baada ya Choki kuondoka African Stars, nikaanza kuona dalili za 'kufungiwa vioo' na Asha Baraka ambaye kabla ya hapo, tulikuwa tukielewana sana.

Ingawa nilijua ananinunia kwa sababu ya Choki kuhama, lakini sikuona mimi nahusika vipi na kuhama huko, lakini nikaamua na mimi kukausha, lakini maisha yanaendelea.

Sikuacha kuandika habari za Twanga wala wanamuziki wake, lakini pia niliandika kwa kasi ileile zile zilizoihusu Extra Bongo na wanamuziki wake.

Siku moja katika miaka ile ya katikati ya 2000, kama ilivyo desturi, Jumamosi usiku yapata kama saa nne hivi, nilienda Mango Garden. Kwa kuwa walinzi wengi wa pale walikuwa wananifahamu, waliniruhusu kuingia.

Lakini ndani, nikazuiwa. Aliyenizuia kuingia alikuwa ni kaka yangu, mzee Abuu Semhando. Akanishika kifuani kisha kwa upole kabisa akaniambia.

"Sikiliza ndugu yangu, Mkurugenzi ameagiza ukija tusikuruhusu kuingia, mimi sijui nini kimetokea, ila naomba unielewe."

Mkurugenzi aliyekuwa anasemwa ni Asha Baraka ambaye nilimuona akiwa amesimama pembeni akitutazama. Kwa namna uhusiano wetu ulivyokuwa unadorora, sikushangaa.

Lakini nikataka kuwa mbishi, nikamwambia Abuu. "Kwa hiyo kaka unanizuia mimi kufanya kazi yangu? Au unafikiri nimekuja kustarehe hapa?"

Akanijibu anatambua kama niko kazini, lakini yeye amepewa maagizo na hawezi kuyakiuka. Sikulazimisha, nikamwelewa nikatoka nje.

Sikwenda tena katika bendi hiyo hadi Ally Choki aliporejea katika bendi hiyo baada ya kundi lake kusambaratika. Wakati akijiandaa kurejea, nilimwambia sitakwenda kule kwa sababu bosi wake hanitaki.

Akaniambia yeye akiwepo nitaingia. Siku mbili kabla hajatangazwa kurudi Twanga, nilikuwa naye Mango Garden tunakula. Mara akatokea Da Asha (waandishi wengi humwita hivyo), akatufuata tulipokuwa. Akanisalimia 'hujambo wewe, za siku? Naona uko na rafiki yako.'

Maisha yakaendelea

 

 

No comments