UNANIJUA MIMI NI NANI?

NILIKUTANA kwa mara ya kwanza na marehemu Godfrey Mngereza (aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa BASATA) mwanzoni mwa mwaka 2020. Ilikuwa ni katika jengo la Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, ndani ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam.
Hatukuwa
tunafahamiana kabla, ingawa mimi kama mwandishi wa michezo na burudani,
nilimtambua kwa nafasi yake na mara kadhaa, nimewahi kuwasiliana naye kwa simu
nikihitaji ufafanuzi wa jambo.
Katika jengo hilo
linalotoa huduma bora kabisa kwa wagonjwa wa moyo hapa nchini, mimi nilikuwa
nimeenda kumpa 'hope' mke wa mdogo wangu, aliyekuwa amelazwa hapo akisubiri
kufanyiwa upasuaji siku tatu mbele. Katika hema ambalo wagonjwa na ndugu
hulitumia kusubiria, nilikuwa nimekaa na mdogo wangu mwenye mke.
Baadaye, wakatokea
watu wawili ambao sikuwafahamu wala kuwatilia maanani, wakasalimiana na mdogo
wangu huyo, dhahiri wakionyesha kufahamiana. Kisha akanitambulisha.
"Bro, huyu
hapa ni shemeji yangu, mdogo wake mke wangu na huyu ni mumewe, anaitwa
Mngereza. Huyu ni mtwasi."
Nikatabasamu,
tukapeana mikono kusalimiana. Tukawakaribisha vitini, mazungumzo ya pamoja
yakaanza. Muda wa kusalimia wagonjwa ulipofika, ni mtu mmoja tu kwa mgonjwa
ndiye anaruhusiwa, kwa hiyo mdogo mtu akapanda juu, sisi watatu tukabakia
hemani.
Mdogo wangu
akaibuka tena. "Bro, kwa kazi yako nadhani huyu utakuwa unamfahamu au
kumsikia, anafanya Basata, ni bosi pale. Mtwasi, kaka yangu ni mwandishi wa
habari, nyie watu kuna sehemu mnakutana."
Ghafla fahamu
zikanirudia, nikamkumbuka. Yeye hakuweza kunitambua, ingawa nilipomkumbusha
kuhusu ishu mbili tatu nilizowahi kumpigia, naye akakumbuka, tukawa sasa ni
ndugu...
Tukaendelea na
mazungumzo mengine ya kawaida. Tukaanza na jengo lile. Jinsi ambavyo Kikwete
alivyofanya jambo la maana kusimamia ujenzi ule. Kama unadhani tatizo la moyo
ni dogo hapa nchini, ukifika pale utatoa machozi ukiona umati wa watu wanaougua
magonjwa ya moyo na ndiyo utajua kama huduma hizi zilikuwa zinapatikana India,
ni kwa kiasi gani tumepoteza watu wengi waliokosa uwezo wa kifedha.
Wengi wa wagonjwa
wanaojazana pale, kimuonekano tu, hawawezi kugharamia shilingi milioni tisa
(kwa bei ya miaka miwili iliyopita) ya matibabu ya moyo kule India. Hapo ni
matibabu pekee, hujazungumzia kuhusu usafiri, chakula na malazi kwa siku si
chini ya 14. Bravo sana mzee wa Msoga.
Tukazungumza siasa.
Jinsi John Pombe Magufuli alivyokuwa 'ananyoosha' nchi, lakini wezi wa mali ya
umma wakiongezeka, licha ya nidhamu ya kazi kurejea.
Ni katika eneo hili
la nidhamu ya kazi kurejea, ndipo aliponieleza jambo lililonifanya kwanza
nimkumbuke leo, lakini pia nimsifu, kwa sababu katika miaka hiyo ya 'unanijua
mimi nani' linaonekana kama gumu kutokea.
Lilimhusu msanii
mmoja mkubwa kutoka nje ya Tanzania. Huyo msanii alikuwa amealikwa na kituo
kimoja cha redio kwa ajili ya tamasha ambalo walikuwa wameandaa. Kwa mujibu wa
taratibu, wenyeji hao walipaswa kupata kibali cha Basata kinachomruhusu
mwanamuziki huyo kufanya shoo nchini. Walifanya hivyo na Basata kupitia
Mngereza, ikaidhinisha kibali hicho..
Siku kadhaa mbele,
mdau mmoja wa muziki, kutoka kituo kingine cha redio, alifika ofisini kwa
Mngereza na kutaka kupata kibali cha msanii yuleyule kwa ajili ya onyesho
waliloandaa, mbaya zaidi, kwa siku ileile ambayo tayari kibali kilishatolewa
kwa redio ile ya kwanza.
Mngereza akakataa,
akitoa sababu za msingi kabisa kuwa jambo lile lisingewezekana kwa sababu
tayari ameshatoa kibali kwa watu wengine kwa msanii yuleyule na siku ileile.
"Jamaa
alinitazama kama anayeniuliza kama ninafahamu yeye ni nani. Nikamsisitizia kuwa
jambo lile halitawezekana. Aliniambia nisijali, mimi nitoe tu kibali mambo
mengine atayamaliza yeye, nikasema no, hayo mambo ya yeye kuyamaliza, mimi
ninao uwezo wa kuyazuia yasitokee," alisema Mngereza.
Basi, akasema jamaa
akatoka ofisini kwake lakini akimuahidi kuwa wangekutana tena ili kulimaliza
suala lile. Akasema usiku wake, akapigiwa simu na bosi wake (Kimuundo, BASATA
ipo chini ya Idara ya Maendeleo ya Utamaduni/Sanaa katika Wizara ya Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo), akimtaka
kufika ofisini kwake kesho yake.
Anasema alijua simu
ile ni matokeo ya msimamo wake kwa jamaa wa ile redio. Na kweli, kesho yake,
ofisini kwa bosi wake, alimkuta yule jamaa na ishu ikawa kama walivyozungumza
jana yake.
"Nilimweleza
ukweli bosi wangu kwamba jambo lile lisingewezekana kwa sababu zilezile
nilizompa jamaa jana, lakini bosi akasisitiza niandike tu kibali, mambo mengine
yatakayotokea watajua namna ya kuyamaliza.
"Kwa kuwa
maadili yanakukataza kubishana na mkubwa wako wa kazi nikamkubalia. Akaniambia
niende na huyo jamaa nikamwandikie kibali. Tukatoka, wakati tukiwa kwenye lifti
tunashuka, nikamwambia jamaa, siwezi kumpa hicho kibali kwa sababu mimi ndiye
nitawajibika endapo lolote litatokea," alisema Mngereza.
Jamaa akashtuka na
kuniuliza nasemaje, nikamwambia kama ulivyosikia. Akashuka haraka na kurudi kwa
bosi kusema, mara nikapigiwa simu nirudi ofisini, nilipofika akaniuliza
nimemwambia nini huyu mtu, nikasema bosi huyu ni kijana mwenzangu, nilikuwa
namtania nashangaa yeye amechukulia siriazi.
Nikatoka ofisini
hapo nikiwa na msimamo uleule. Pamoja na kuwa yule ni bosi wangu, lakini yeye
si mamlaka ya uteuzi wangu. Zilikuwa zimebaki siku mbili tu haya matamasha
yafanyike na redio zote zilikuwa zinamtaja msanii huyo kuwa atashiriki kwenye
tamasha lao ambalo bahati mbaya pia muda ulikuwa ni uleule.
Kwa kuwa nilijua
nitasumbuliwa, nikaamua kuzima simu. Huyo jamaa akatuma mtu ofisini kwangu
akiwa na bahasha, nikacheka sana nikamwambia mrudishie mwambie mshahara wangu
unanitosha. Wale jamaa wa ile redio ya kwanza wakaniuliza hili jambo liko vipi,
nikawaambia hata mimi sielewi, lakini mimi nimetoa kibali kwao tu.
Wale watu wa redio
wakapelekana mahakamani. Lakini Mngereza alisema kwa huzuni kubwa "Basi
bwana, siku zikawa zimeisha, yule msanii kweli akaja, lakini amini usiamini,
huyo msanii alienda kufanya tamasha kwa wale jamaa ambao sikuwapa kibali na
sijajua kesi ya madai ya fidia ya ile redio nyingine iliishaje."
Kuna watu katika
hii nchi hawana cheo chochote serikalini, lakini wanaweza kufanya chochote na
wasifanywe chochote.
Godfrey Mngereza
alifariki ghafla Desemba mwaka jana akiwa Dodoma kikazi ambako licha ya
kukimbizwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa huo, lakini juhudi za kumuokoa
hazikufanikiwa. Mungu mlaze mahala pema
peponi Amina.

Post a Comment