KWA NINI WATU WANASHANGILIA SABAYA KUSIMAMISHWA?


Haki Ngowi on Twitter: "MKUU wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole  Sabaya, akilia kwa uchungu wakati wa shughuli za kuuaga mwili wa Hayati Dk.  John Pombe Magufuli, Uwanja wa Jamhuri


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amemsimamisha kazi Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya kwa kile alichosema, kupisha uchunguzi juu ya tuhuma zinazomkabili.

Rais alichukua uamuzi huo jana na katika mitandao ya kijamii, habari hiyo imepokewa kwa hisia tofauti, wengi wakionekana kufurahishwa, ingawa hakuna popote palipotajwa tuhuma zinazomkabili ni zipi hasa.

Hata hivyo, kwa mujibu wa wachangiaji kwenye mitandao mbalimbali, Sabaya ambaye alikuwa mmoja kati ya viongozi vipenzi wa hayati Rais John Magufuli, anachukuliwa kama mtu aliyekuwa amejawa na jeuri ya kimamlaka.

Kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Hai, Sabaya analaumiwa kwa kutochukua hatua stahiki kwa matukio kadhaa yaliyotokea wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita, ikiwemo kushambuliwa kwa msafara wa aliyekuwa Mgombea Urais wa Chadema, Tundu Lissu.

Aidha, Sabaya pia alituhumiwa na Mwenyekiti wa chama hicho cha upinzani, Freeman Mbowe, kwa kitendo chake cha kumfuata eneo alilokuwepo, akiwa na silaha za moto wakati wa kampeni hizo, akiwa na nia ya kumdhuru, ambapo watu kadhaa waliokuwa karibu naye walikamatwa.

Baada ya hatua hiyo kuchukuliwa na mkuu huyo wa nchi, ambaye katika siku zake za mwanzo za uongozi wake anaonekana kuungwa mkono na wananchi wengi, wapo wanaotaka hatua kama hiyo ichukuliwe kwa viongozi wengine zaidi, ambao wanaonekana kushabihiana na Sabaya.

Wakuu wa mikoa miwili ambao bado wapo katika nafasi zao ndiyo wanazungumzwa zaidi, wakimtaka rais kuwachukulia hatua, kwani nao wanatajwa kutumia vibaya nafasi zao wakiwa katika ofisi za umma.

Ma RC hao vijana, wanadaiwa kuwa na kauli zisizo za kiuongozi, kujaa ubabe, wenye kebehi na wasio na staha kwa wananchi, ambao badala ya kuwaunganisha kuwa taifa moja, wao wamekuwa wakiwabagua na kuwagawa kwa misingi ya kiitikadi.

Licha ya wakuu hao wa mikoa ambao bado wapo ofisini, katika mitandao hiyo ya kijamii, wananchi pia wanataka wakuu wa mikoa mingine miwili, ambao kwa sasa hawapo ofisini, nao wachukuliwe hatua kwa makosa wanayodaiwa kuyafanya wakiwa katika utumishi wa umma.

Mabosi hao ambao nao ni vijana, pia walikuwa ni 'watoto wa mfalme' wakati wa uongozi wa Hayati Rais wa Awamu ya Tano, John Pombe Magufuli. Katika mitandao, viongozi hao wanadaiwa kuwa wakati wao, walijawa na jeuri, majivuno, kutoheshimu sheria na pia, waliendeleza dhambi kubwa ya kuligawa taifa kwa misingi ya kiitikadi.

Katika kundi la wanaotakiwa kusimamishwa na kuchunguzwa, pia wanatajwa viongozi wawili waliowahi kushika nafasi nyeti ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakidaiwa kuwa washauri wakuu wa Mwenyekiti. Kwa sasa makada hao hawako katika nafasi zao.

 

No comments